ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 15, 2014

Daktari aliyembusu mgonjwa wake asakwa

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, ameliagiza Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Lucas Mweri, kumchukulia hatua daktari anayetuhumiwa kumbusu mgonjwa wake wakati akimtibu.

Gambo alitoa agizo hilo jana baada ya kupokea malalamiko ya tukio hilo na kueleza kuwa ni la ukiukwaji wa maadili ya kidaktari na aibu kwa wilaya.

Aliliagiza jeshi la polisi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa mtaalamu huyo na wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali ilidaiwa kuwa daktari huyo, Ally Naah anayefanyakazi Hospitali ya Wilaya ya Korogwe ya Magunga, anadaiwa kumbusu mwanamke aliyekwenda kupata matibabu hospitalini hapo.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema siku ya tukio mwanamke huyo aliambatana na mumewe hadi hospitalini hapo kwa ajili ya kupata matibabu na baada ya kufika daktari huyo alimtaka aingie ndani kumfanyia uchunguzi.

Ilidaiwa kuwa, mume wa mwanamke huyo aliyekuwa nje akimsubiri mkewe alipata hofu baada ya kuona muda mrefu umepita bila mkewe kutoka, ndipo alipochungulia dirishani na kumuona daktari huyo akimbusu.

“Yule bwana hakuamini alichokiona, hakuvumilia na alipiga kelele akiomba msaada…Kwa kweli jambo hili ni aibu na limetuondolea uaminifu,” alisema mmoja wa shuhuda wa tukio hilo.

Hata hivyo, habari za kipolisi zinaeleza kuwa tayari tukio hilo limeshaanza kufanyiwa kazi ikiwamo kufuatiliwa eneo lilipotendeka kosa hilo kwa hatua zaidi za kisheria. Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Dk Olden Ngasa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema mtuhumiwa alitoroka baada ya tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: