Hapa namaanisha kwamba, miaka ya zamani, wapendanao au wapenzi waliyatumia sana maneno haya katika kuoneshana upendo wa dhati.
Ilikuwa sifa kubwa kumsikia msichana akimwita boyfriend wake ‘dear’au mpenzi!
“Niambie my dear! Upo mpenzi?” ndivyo ilivyokuwa.
WAMEANZA KUHARIBU WANAWAKE
Mara ya kwanza nilishangaa kumsikia mwanamke mmoja kwenye simu anamwita mwanamke mwenzake dear. Tena alisema: my dear, zile sabuni za kuondoa alama nyeusi usoni ulizinunua wapi?”
Kuna siku nilimsikia mwanamke mwingine kwenye simu akisema: “Nakuja mpenzi wangu jamani. Kwanza we umebeba na kile kitenge nilichokuagiza?”
AKILINI MWANGU
Awali niliamini wanaozungumza nao kwenye simu huenda ni wanaume, lakini meseji zilionesha upande wa pili ni wanawake wenzao. Kwa maneno ya sabuni za kuondoa alama nyeusi usoni na kitenge.
LIMESAMBAA
Baada ya hapo nilianza kufuatilia hatua kwa hatua nikaja kubaini waziwazi kwamba, wanawake wengi wameshapoka maneno hayo kutoka kwenye kuyatumia kwa wapenzi wao na kuwapachika mashoga zao.
MADHARA YAKE
Nilichobaini kwa harakaharaka siku hizi ni kwamba, baadhi ya wake za watu wamekuwa wakibebeshwa sifa ya umalaya kwa sababu ya matumizi ya maneno haya mawili. Mfano, mke wa mtu yuko ndani kwake, anapokea simu ya mwanamke mwenzake, anasema: Niambie my dear... we umefika kwani...basi na mimi naoga nakuja...haya mpenzi wangu nakuja sasa hivi.
Kwa majirani wanaomsikia mwanamke huyo, baadhi yao huamini alikuwa akizungumza na mchepuko kwa sababu ya my dear na mpenzi.
HAYANA MAANA TENA
Wiki iliyopita niliamua kufanya mahojiano na baadhi ya wanaume ambao wanafahamu kuhusu wanawake kuyatumia maneno hayo mawili kwa kuitana wenyewe.
Maoni yao yalisimama kwenye maana moja kwamba, maneno hayo kwa sasa hayana maana tena katika matumizi ya wapendanao.
“Sasa kama mke wangu anamwita mwanamke mwenzake dear au mpenzi, akiniita mimi kuna maana gani? Yaani mimi na shoga yake ni kitu kimoja?” alihoji baba Abdul, mkazi wa Mabibo jijini Dar.
Baba Steve wa Sinza-Mori, Dar: “Kusema ukweli wanawake wanavuruga mambo mengi sana ila hatujui tu. Ukiachilia mbali hayo maneno kuyatumia kuitana wenyewe kwa wenyewe we si unaona siku hizi kila mmoja anavaa suruali.”
“Ah! Mimi niliwahi kumuuliza mke wangu ni kwa nini anamwita mwanamke mwenzake dear, akasema haoni tatizo, lakini ukweli mimi naona tatizo lipo. Ipo siku na mimi nitampigia simu rafiki yangu anaitwa Sudi nitamwita honey, nimsikie mke wangu atasemaje,” alisema Abdallah Mkadala, mkazi wa Buguruni, Dar.
NI MBINU YA USALITI?
Baadhi ya wanaume walionesha wasiwasi wao kwamba, huenda wanawake wanaitumia fursa hiyo kuweza kusaliti!
Kivipi? Kumbe inawezekana mwanaume akakaa na mpenzi wake ambaye anaweza kupokea simu ya mchepuko akatumia neno dear au mpenzi kwa kumaanisha huku mwanaume huyo akijua anaongea na mwanamke mwenzake!
WANAWAKE WENYEWE WANASEMAJE?
Pia niliweza kuzungumza na baadhi ya wanawake kuhusu matumizi ya maneno hayo. Niliwalenga zaidi wale wanaopenda kuyatumia.
Mama Mwamtumu wa Makongo, Dar: “Kusema ukweli wanawake tumeshajiweka kwenye mazoea, hasa sisi wa mijini. Lakini kiusahihi kabisa si maneno mazuri kuyatumia sisi kwa sisi japokuwa maana ya maneno yenyewe ni upendo tu.”
Skola, mkazi wa Bunju B: “Dear na mpenzi ni neno moja jamani! Ni kuonesha upendo kwa mwenzako. Ila ni kweli kuna ukakasi. Mfano wanaume nao wakiamua kuitana sweet, darling naamini sisi wanawake hatutawaelewa hata kidogo.”
GPL
No comments:
Post a Comment