ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 14, 2014

FAIDA, HASARA ZA WAPENZI KUFANYA KAZI OFISI MOJA -2

Mada iliyopo mezani ni faida na hasara za wapendao kufanya kazi ofisi moja ambayo tulianza kuijadili wiki iliyopita. Uhali gani msomaji wangu? Ni matumaini yangu kwamba unaendelea vizuri na majukumu ya ujenzi wa taifa. Karibu tena kwenye busati letu ambapo tunajuzana mambo mbalimbali yahusuyo mapennzi.

Wiki iliyopita, tulijadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wanandoa au wawili wapendanao wanaofanya kazi kwenye ofisi moja na mwisho, niliishia kukueleza nini kifanyike ili kuzuia matatizo yanayoweza kujitokeza.

NINI CHA KUFANYA?
Matatizo katika sehemu za kazi, hasa kwa wapendanao yapo na hayakwepeki lakini ukizingatia yafuatayo, utaishi vizuri na mwenzi wako, uhusiano wenu wa kimapenzi utaimarika na ufanisi kazini utaongezeka pia.

1. USICHANGANYE MAPENZI NA KAZI

Yawezekana usiku kucha wewe na mwenzi wako hamkulala, mmekesha mkipigana, kurushiana maneno makali au mlilala mzungu wa nne. Hata hivyo, unapaswa kujua kwamba ukifika kazini, mambo yote ya usiku unayaacha nyumbani na unamchukulia mwenzako kama mfanyakazi mwenzako wa kawaida.
Huna haja ya kununa, kuwa na kisirani au kuharibu kazi kwa sababu jana uligombana naye. Fanya kazi na muda wa kurudi nyumbani ukifika, kaendeleeni na migogoro yenu. Ni makosa makubwa kuhamishia matatizo ya nyumbani kazini.

Pia kama umekosana na mwenzi wako kazini kwa sababu za kikazi, huna haja ya kuendelea kununa hadi nyumbani, utakuwa unahatarisha uhusiano wako. Lazima kuwe na mipaka kati ya mambo ya kifamilia na mambo ya kizazi.

2. MWACHE AWE HURU

Haina maana kwamba kwa sababu ni mkeo, mumeo au mpenzi wako, basi hana haki ya kuzungumza au kucheka na watu wengine isipokuwa wewe tu. Mpe uhuru, hata kama anachanganyikana na watu wa jinsia tofauti, huna haja ya kukasirika au kujisikia wivu. Mwache abadilishane mawazo na watu wengine na akija kwako, atakuwa mpya kabisa.

Acha kumganda, siyo lazima kila mara aende na wewe ‘lanchi’, nafasi yako ni nyumbani lakini kazini kila mmoja anao uhuru wa kuchanganyikana na marafiki na wafanyakazi wenzake.

3. USIINGILIE MAMBO YAKE BINAFSI

Yawezekana mumeo, mkeo au mpenzi wako amekorofishana na mfanyakazi mwenzake kwa sababu za kikazi au nyinginezo, hayo ni mambo ya kawaida katika sehemu za kazi. Acha kuingilia ugomvi wake au kumtetea wakati mwenyewe hajakuomba kufanya hivyo. Muache amalize matatizo yake mwenyewe na hiyo itamfanya ajisikie huru zaidi. Kwa wanawake, kutongozwa sehemu za kazi ni mambo ya kawaida hivyo usikasirike na kupandisha jazba ukisikia kuna ‘njemba’ inammendea mwenzi wako.

Muamini na mpe nafasi ya kukabiliana na changamoto kama hizo kwani kwa mwanamke anayejiheshimu, lazima akulindie heshima yako hata kama uko mbali au hujui chochote.

4. KUWA NA NIDHAMU KAZINI

Ni vigumu kwa mtu anayejiheshimu, kukosewa adabu na wengine kwa urahisi. Ukishajua unafanya kazi na mwenzi wako ofisi moja, jitahidi kujiheshimu kwa kujiepusha na ubishi usio na msingi, masihara yaliyovuka mipaka au ugomvi kwani ni rahisi kufanyiwa tukio baya kama kutukanwa, kupigwa au kufanyiwa masihara mabaya mbele ya mwenzi wako, jambo ambalo lazima litaziumiza hisia zake.

5. ONESHA BIDII YA KAZI

Miongoni mwa mambo yanayoweza kumfanya mtu akaheshimika kazini, ni bidii na ufanisi katika kazi yake. Jitahidi kujielimisha kadiri uwezavyo kuhusu kazi unayoifanya na kuwa na bidii kwani kila mtu atakupenda na kukuheshimu.

Mwenzi wako pia atazidisha mapenzi kwako kwani atajisikia fahari jinsi watu wengine wanavyokutolea mifano mizuri.Ni matumaini yangu kuwa utakuwa umejifunza kitu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.

GPL

No comments: