ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 14, 2014

Guinea ya Ikweta kuandaa AFCON 2015

Shirikisho la soka la Afrika CAF limeichagua na kuipatia nafasi Guinea ya Ikweta kuandaa fainali za kombe la Afrika 2015 kuchukua nafasi ya Moroko iliyojitoa wiki iliyopita. Awali Rais wa CAF Issa Hayatou alikuwa na majadiliano yenye manufaa na Rais wa nchi hiyo tajiri ya mafuta Teodoro Obiang Nguema mjini Malabo kabla ya kufikia hatua ya kuikabidhi nchi yake dhamana hiyo.

Taarifa ya CAF imethibitisha leo ijumaa kuwa Guinea ya Ikweta mojawapo ya nchi ndogo barani Afrika imepewa jukumu hilo kubwa la kuokoa jahazi la michuano hiyo na itashiriki fainali hizo kama ilivyo kawaida ya mwenyeji.

Nchi hiyo yenye kutumia kihispaniola kama lugha ya Taifa iliandaa fainali za Afrika za mwaka 2012 kwa pamoja na jirani yake Gabon. Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Januari 17- Februari 8 mwakani kwenye miji ya Bata, Ebebiyin, Mongomo na mji mkuu Malabo. Mwaka 2012 walitumia miji miwili tu ya Bata na Malabo.

Ratiba kupangwa Malabo

Sherehe za kupanga ratiba ya mechi za fainali hizo itafanyika mji mkuu wa Malabo mnamo Desemba 3 mwaka huu. Taarifa ya CAF imesema kuwa Shirikisho hilo linawashukuru watu wa Guinea ya Ikweta, Serikali pamoja na Rais Ngwema mwenyewe kwa utayari wao wa kuokoa mashindano hayo. Moroko ilijitoa kaandaa fainali hizo baada ya kuomba CAF isogeze mbele mashindano kwa ajili ya hofu ya ugonjwa wa Ebola ambao umeenea kwenye nchi kadhaa za Afrika Magharibi ambazo kwa kawaida hupeleka timu nyingi Zaidi katika fainali za Afrika.

CAF ilikataa mpango huo kwa madai kuwa haijawahi kuahirisha wala kufuta fainali hizo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957. Moroko walipewa hadi jumamosi iliyopita kuthibitisha utayari wao wa kuandaa mashindano hayo lakini walishindwa kufanya hivyo na CAF ikaamua kufanya mchakato wa kutafuta nchi ya kuokoa na hatimaye imepatikana hii leo.

Shirikisho hilo limeipa adhabu Moroko ya kutoshiriki fainali zijazo za huko Guinea ya Ikweta.

BBC

1 comment:

Anonymous said...

waandishi wa habari. "nchi hiyo tajiri ya mafuta" au nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta. si kweli nchi hiyo ni tajiri bali ina utajiri wa mafuta.