Lile jimbo lililo gumzo la
mjini hivi sasa lawika tena.
Leo Mkanyia akiwa na timu
kamili ya Swahili Blues Band wameipagawisha jumuiya ya kimataifa
iishiyo jijini Dar es Salaam jumatano hii. Haya yametokea kwenye
ukumbi wa Alliance Francais katika onyesho kabambe lililo andaliwa na
Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa. Onyesho hilo maarufu kama Barazani
ni la mwisho katika mwaka huu wa 2014. Swahili Blues Band pamoja na
wasanii kadhaa walipewa heshima ya kupiga mshindo katika show hii
kabambe ya kufungwa mwaka.
Swahili Blues Band
walipiga nyimbo zao kadhaa zikiwemo zile maarufu kama vile Che Maria,
Afrika na Ewe Mwana. Kadamnasi iliyobahatika kuhudhuria show hiyo
kabambe ilikuwa ni sehemu ya historia baada ya kushirikishwa kuimba
kiitikio cha wimbo ambao kwa sasa umejizolea umaarufu mkubwa katika
medani za kimataifa yaani ‘Pamoja’. Wimbo huu mahususi
wakuhamasisha jamii ya kimataifa kuungana na kuushambulia ugonjwa
mkubwa sana kwa sasa yaani Ebola, ulipigwa kwa mara ya kwanza mjini
Nottingham Uingereza. Jumatano hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa
wimbo huo kucharazwa live ndani ya ardhi ya Bongo. Leo
aliwasherehesha na kuwaimbisha umati mkubwa ulio hudhuria kuimba
kiitikio cha pamoja kwa pamoja.
Mdau wa Vijimambo alipata
fursa ya kukutana na kumuuliza Leo,kulikoni mbona wewe shughuli zako
zote mara Nottingham, mara Derby, kila ijumaa kwenye hoteli ya nyota
tano ya Serena na sasa hapa Alliance Francais?je huu si aina fulani
ya ubaguzi kwa Watanzania wenzako wa kawaida?au wewe muziki wako si
kwa ajili ya Watanzania wakawaida?
Huku akitabasamu, Leo
alijibu “La hasha, si ubaguzi hata kidogo.”
Pengine hao ulio wataja
wamechukua muda mfupi zaidi kuelewa ninachotaka kuwaambia
wasikilizaji wangu.
Pengine hao wamekuwa
wepesi zaidi katika kutuunga mkono kwenye harakati zetu za kujaribu
kuurudisha muziki wetu wa Tanzania katika asili yake.
Pengine hao wamegundua kwa
haraka zaidi kuwa nina vitu vya kuwaambia jamii na muziki ni njia tu
yakufikia azma hii. Vile vile Leo aliendelea kwa kusema kuwa “Nikutoe
shaka ndugu yangu, hapa nyumbani tumeanza
kupata ushirikiano mkubwa
kutoka kwa wadau mbali mbali.” Aliendelea kwa kutoa mifano
ifuatayo.
EA Radio wameshatuita kwa
mahojiano mara kadhaa na wanacheza sana nyimbo zetu.
City Radio Fm nayo hali
kadhalika nyimbo zetu zimekuwa maarufu hadi kufikia kuombwa mara kwa
mara na wasikilizaji wao.
Radio One tumesha fanya
nao mahojiano na nimepata taarifa kuwa wimbo wenu kipenzi wa Che
Maria umeingia katika top ten show yao.
Bongo5 nao tushafanya nao
mahojiano kabambe sana.
Jumamosi ya wiki hii saa 6
hadi 7 za mchana tutakuwa wageni wa Radio Tumanini.
Leo aliendelea “hivyo
mdau utaona kwa hakika tunavyo shirikiana na wadau mbali mbali hapa
nchini kwetu. Sidhani kama bado utatuita sisi ni wabaguzi dhidi ya
Watanzania wenzetu.” Mwisho kabisa Leo akapenda kumalizia kwa
kusema kuwa “kwa sasa tuko katika jitihada za kupata sehemu hapa
mjini ili tuweze kupiga mara kwa mara kwenye sehemu ambazo wanachi wa
kawaida wanaweza kutufika kwa urahisi . Tuna nafasi ya kupiga siku
za Alhamis, Jumamosi na Jumapili. Haya yote ni katika kuhakikisha
tunampatia Mtanzania mwenzetu muziki wake wa asili anaoupenda yaani
Swahili Blues.” Alimalizia Leo Mkanyia.
Ruksa kwa kila mtu akiguswa na milindimo mambo huwa hivi hata ukiwa na na viatu virefu ruksa.
No comments:
Post a Comment