ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 26, 2014

Majina ya wapiga kura yachomwa moto Dar kupinga kituo hewa

Kasheshe iliibuka katika zoezi la uandikishaji la wakazi katika Mtaa wa Mbondole katika Kata ya Msongola Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam baada ya makarani kuandikisha majina kwenye kituo bubu cha Shule ya Msingi Mbondole.

Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi baada ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) tawi la Mbondole kubaini mbinu hiyo kuwa inaweza kutumika kuandisha majina watu ambao siyo wakazi, hivyo kuamuru kituo hicho kisitishwe na kuhamia kituo cha Sekondari ya Mbondole.

Wanachama hao wa CUF walikuwa wamejiandaa wakiongozwa na mgombea wao wa nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Mbondole, Mrisho Jogoo huku wengine wakisikika wakisema kuwa wamezoea kuongeza majina na kuwa siku hiyo pangechimbika.

Baada ya purukushani hizo, Jogoo aliiambia NIPASHE kuwa baada ya kufika katika kituo hicho alfajiri walikuta majina yameshaandikishwa, hivyo kwa pamoja wafuasi wa CUF na Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikubaliana kuyachoma moto ili zoezi lianze upya.


Jogoo alisema kuwa walikubaliana kuwa bila kufanya hivyo, vurugu zingetokea.

“Hata karani Mary Sanga tulipoongea naye hakuonyesha kubisha, hilo lilisaidia sana kuepusha shari na kukiri kuwa walifanya kosa kuandikisha kwenye kituo ambacho hakijaruhusiwa kisheria. Pia alituambia kuwa kilichosababisha ni mawasiliano kutokuwa mazuri,” alisema.

Alisema katika Mtaa wa Mbondole kikako kiliamua kutenga kituo kimoja cha uandikishaji cha shule ya sekondari.

Afisa Mtendaji Kata wa Msongola, Omari Ally, alisema pamoja na tukio la kuchanganya kituo, kilichotokea katika Mtaa wa Mbondole, lakini zoezi la uandikishaji zinakwenda vizuri.

“Hakuna tatizo kubwa lililotokea kama ni kuchoma majina yalikuwa ni maamuzi ya hekima ili kila upande kuondoe hofu kuwa walioandikishwa hawakuwa wakazi wa Mtaa wa Mbondole,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: