Kufuatia adha ya usafiri wa majini inayowakabili wakazi waishio katika fukwe za Ziwa Nyasa, Mamlaka ya Bandari Tanzania kupitia kituo chake cha Kyela ipo mbioni kujenga meli ya abiria na mizigo ili kuwahudumia wakazi hao.
Hayo yaliwekwa bayana na Mkuu wa Bandari ya Kyela, Bw. Percival Ntetema wakati timu wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Tume ya Mipango ilipotembelea na kukagua bandari za Itungi na Kiwira zilizopo wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya.
Bw. Ntetema alisema kuwa Mamlaka imeshakamilisha mchakato wa manunuzi na tayari imempata mkandarasi M/S Songoro Marine Transport Ltd kwa ajili ya ujenzi wa meli yenye uwezo wa kubeba jumla ya tani 200 za mizigo na abiria 200.
“Mamlaka ipo kwenye hatua za mwisho za kuandaa mkataba unaotarajiwa kutiwa saini mwezi ujao na kazi itaanza mwanzoni mwa mwaka ujao,” alisema.
Bw. Ntetema aliongeza kuwa mpaka sasa Bandari ya Kyela imeshaanza maandalizi ya kuvuta umeme uliofadhiliwa na Wakala wa Umeme Vijijini pamoja na kuaanza kwa kujenga matishari mawili ili yaweze kurahisisha utoaji wa huduma mara meli hiyo itakapoanza kazi mwishoni mwa mwaka ujao.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri aliupongeza uongozi wa Mamlaka kwa hatua yake hiyo kwani itaongeza tija ya shughuli za kiuchumi katika kanda hiyo ya Ziwa Nyasa.
“Ninaupongeza uongozi wa Mamlaka ya Bandari kwa kuanza mchakato huu utakaofungulia fursa za kiuchumi na maendeleo kwenye ukanda huu, hivyo kuunga mkono jitihada za serikali za kupunguza vikwazo mbalimbali vinavorudisha kasi ya kusaka kupunguza umaskini nchini,” alisema.
Bibi Mwanri aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa za kuhudumia shehena na abiria kutoka mikoa ya Mbeya, Njombe, na Ruvuma. Pamoja na kuhudumia nchi za jirani ikiwemo Malawi, Msumbiji na Zambia.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) bandari ni mojawapo ya vipaumbele vitano vya kimkakati vyenye lengo la kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi wa uchumi kwa watu walio wengi.
Vipaumbele vingine ni Kilimo ambapo lengo kuu likiwa ni kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya kuuza nje ya nchi; Maendeleo ya viwanda: Msisitizo umewekwa katika kuvutia, kuanzishwa na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini (kama vile viwanda vya nguo, mbolea, saruji, makaa ya mawe, chuma na bidhaa za chuma) na pia sekta ya madini kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.
Pamoja na kipaumbele cha Maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi: Mpango unahimiza kuwekeza katika elimu (hasa katika elimu ya juu na vyuo vya ufundi) na huduma za afya (kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma) katika kujenga nguvu kazi itakayotuletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii; na Utalii, Biashara, na huduma za Fedha ambapo jitihada zimewekwa kwenye uendelezaji uwezo wa kuuza katika masoko ya ndani na nje, kuongeza idadi ya watalii na matumizi yao wawapo nchini, na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha.
Mkuu wa Bandari ya Kyela, Bw. Percival Ntetema akiwakaribishia wakaguzi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofika ofisini kwake.
Kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence (kulia) akihoji masuala mbalimbali yanayohusiana na shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na Bandari ya Kyela.
Mkuu wa Bandari ya Kyela, Bw. Percival Ntetema akifafanua jambo kwa Timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Mkuu wa Bandari ya Kyela, Bw. Percival Ntetema akifafanua jambo kwa Timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango.
Kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence (Mbele) akiwaongoza wajumbe wa Timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango kupanda boti ili kwenda kushuhudia lango la kuingilia Gati la Bandari ndogo ya Itungi. Itungi ni bandari ya kipekee nchini kujengwa mtoni.
Mkuu wa Bandari ya Kyela, Bw. Percival Ntetema (Kulia) akiwaonesha kitu wajumbe wa Timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakati wakishuhudia lango la kuingilia Gati la Bandari ndogo ya Itungi.
Mkuu wa Bandari ya Kyela, Bw. Percival Ntetema (Aliyevaa tai) akiwaonesha kitu wajumbe wa Timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo sehemu inapojengwa gati mpya (halionekani) katika Bandari ya Kiwira.
Wajumbe wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango walipata fursa ya kujionea meli pekee inayotoa huduma ya kusafirisha abiria na mizigo (MV Songea) katika Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania.
Wajumbe wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango walipata fursa ya kujionea meli pekee inayotoa huduma ya kusafirisha abiria na mizigo (MV Songea) katika Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania.
PICHA ZOTE NA SAIDI MKABAKULI
No comments:
Post a Comment