ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 15, 2014

Maswali kumi kwa mbunge wangu:Said Barwani

Mbunge wa Lindi Mjini, Said Barwani

1.Mwajuma Awadh, mkazi wa Matopeni Lindi mjini.
Wakati unaomba ubunge ulituahidi kuwa tukikuchagua utahakikisha unasimamia sera ya afya na kwamba wanawake wajawazito wanapewa huduma, lakini hivi sasa wanalazimika kununua vifaa vya kuwasaidia kujifungua.
Jibu: Nimefuatilia na ninaendelea kufuatilia ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa bure kabisa bila kulipia kitu kama sera inavyosema.
2. Yusra Mkola, mkazi wa Mnazi Mmoja Lindi mjini.
Una mpango gani wa kuwasaidia kina mama wajasiriamali wa kokoto na wale wanaotengeneza bidhaa za mikono kupata soko la uhakika?
Jibu: Tatizo la soko ni kubwa lakini najitahidi kuwatafutia masoko ya nje ya mkoa likipatikana nitawajulisha, ila nimewashauri wajishirikishe kwenye maonyesho ya biashara kwa ajili ya kupata uzoefu na masoko.
3. Robert Amandus, mkazi wa Mpilipili, Lindi.
Wakati unaomba kura uliahidi kuwasaidia vifaa watu wenye ulemavu na wazee ili wapate huduma za afya bure, kwa uanzisha dirisha la wazee katika vituo vya afya na hospitali,umefikia wapi?
Jibu: Nimeanza kugawa baiskeli za walemavu zaidi ya 100 na mafuta kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
4. Ismail Ndembo, mkazi wa Mitwero Lindi mjini.
Wakati unaomba ubunge ulisema utasimamia haki za wapigakura wako, leo wananchi wa Mitwero wanadhulumiwa ardhi yao na mradi wa UTT na Manispaa ya Lindi kwa kulipwa fedha kidogo je, unawasaidiaje?
Jibu: Nimesimamia kwa kushirikiana na baadhi ya madiwani mpaka mradi wa UTT umesimamishwa kutokana na kutoeleweka kwa jamii na fidia kuwa ndogo.
5. Kulwa Bahati, mkazi wa Kariakoo Lindi.
Wakati unaomba ubunge uliahidi kuboresha michezo kwa vijana kwa kuanzisha timu za michezo pamoja na viwanja. Je, mpango huo umefikia wapi?
Jibu: Nimeandaa ligi ya mbunge ambayo itakutanisha vijana kwa lengo la kubaini vipaji.
6. Ibrahimu Kasim wa Ngapa Lindi.
Wakati unaomba ubunge uliahidi kuwasimamia wakazi wa Ngapa kulipwa fidia baada ya kukatwa kwa minazi yao kupisha mradi wa umeme, umefikia wapi?
Jibu: Nimefuatilia Wizara ya Nishati na Madini nimeambiwa suala hilo limeanza kufanyiwa upembuzi yakinifu ili kuwalipa fidia watu watakaoathirika na mradi huo.
7. Musa Abdu, mkazi wa Raha Leo.
Ulipokuwa unaomba ridhaa ya kuwa mwakilishi wetu mwaka 2005, alisema kuwa ukipata nafasi hiyo hutaishi Dar es Salaam wala Dodoma, bali utakuwa jimboni karibu muda wote lakini sasa imekuwa sivyo.
Jibu: Unajua ninakaa Dar es Salaam kwa sababu mambo yote na mipango yote iko hapo Nikikaa Lindi mambo mengine hayatakwenda, lengo ni kuwasaidia wapigakura wangu kupitia fedha za jimbo na wafadhili ambao wanapatikana Dar es Salaam.
8. Mohamedi Bakari, mkazi wa Lindi mjini.
Uliahidi kusimamia upatikanaji wa fedha za wajasiriamali vijana na wanawake. Umefikia wapi na muda wako wa kuwa madarakani unakaribia kuisha?
Jibu: Mpango huo unasuasua kutokana na viongozi na watendaji walio chini ya Chama cha Mapinduzi kutonipa ushirikiano. Pia fedha hizo za vijana zinatumika kwenye shughuli nyingine zinapoingia katika halmashauri.
9. Ibrahimu Kaisi, mkazi wa Lindi mjini.
Wakati unaomba kura za ubunge 2010, uliahidi kuwa katika siku 90 za uongozi wako utahakikisha Mji wa Lindi unakuwa msafi kuliko Moshi. Mpango huo umekwama wapi mbona sasa Lindi ni chafu kuliko zamani?
Jibu: Usafi wa manispaa umeboreka kutoka asilimia 10 niliyoikuta hadi 45 na ninafanya jitihada za kufikia asilimia 85 kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa
10. Mariamu Saidi, mkazi wa Lindi
Ulituahidi kwamba utaboresha huduma za jamii ikiwamo upatikanaji wa majisafi na salama. Mpango huo umeishia wapi kwani wananchi wako wanaendelea kuteseka
Jibu: Nilitafuta wafadhili kutoka Sweden kuja kufanya utafiti wa vyanzo vipya vya maji, lakini uongozi wa wilaya uliwazuia na kusababisha kukwama kwa mradi huo ambao ungeweza kuondoa tatizo la maji katika manispaa.
Mwananchi

No comments: