ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 16, 2014

Sitti aiponza Miss Tanzania

Dar es Salaam. Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), wanatarajia kuifanyia tathmini Kamati ya Miss Tanzania kujua mapungufu yaliyopo ili kuchukua hatua stahiki.
Utata wa umri wa aliyekuwa mshindi wa taji la mwaka huu, Sitti Mtemvu, unaonekana kama chanzo cha kuibuka kwa matatizo mengine yaliyokuwa yakidaiwa kufanyika kinyume cha taratibu za mashindano hayo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza alisema kwa muda mrefu sasa wamepokea malalamiko tofauti kutoka kwa wadau yanayoashiria mapungufu makubwa dhidi ya waandaaji hao wa mashindano ya ulimbwende nchini.
Mngereza alisema yapo mambo ambayo yanaendelea yanayotakiwa kufanyiwa tathmini ili kupata picha halisi kabla ya kuyumba na kupoteza sifa kwa mashindano hayo miaka ijayo.
“Kwa taratibu zilizopo, Baraza ambalo ndilo lililotoa leseni ya kuendesha Miss Tanzania litafanya tathmini ili kujua tatizo ni nini na kupata maoni kutoka kwa wadau kuhusu nini kifanyike au kibadilike ili mashindano haya yasipoteze sifa, kwani nia yetu kama baraza ni kuhakikisha tunakuwa miongoni mwa nchi zinazotoa warembo wa dunia na si kila siku kuangukia pua,” alisema Mngereza.
Akizungumzia tuhuma zinazowakabili Kamati ya Miss Tanzania, kuhusu kutompa fedha za maandalizi na michango mingine kwa ajili ya kushiriki Miss World, Miss Tanzania 2013, Happyness Watimanywa, alisema ni taarifa mpya na watahakikisha wanazifanyia kazi.
“Hizi ni taarifa mpya kwa sasa, lakini tutahakikisha tunazifanyia kazi haraka iwezekanavyo na tutakachoangalia sisi ni mkataba baina yao unasemaje, tukibaini kwamba waandaaji walikiuka mkataba tutajua kwanini walifanya hivyo na taratibu zinasemaje hapo ndipo tutajua nini cha kufanya,” alisema.
Mama mzazi wa Happyness juzi alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akidai kuwa, mwanaye hakupewa fedha za maandalizi ya mashindano ya Miss World ilhali alitakiwa kuondoka nchini Jumamosi (jana).
Alifafanua kuwa waandaaji hao wameshindwa kumwandaa katika upande wa mavazi na mengineyo.
Alipotafutwa Hasheem Lundenga, Mkurugenzi wa kampuni ya Lino Agency, alisema: “Suala hilo halina ukweli wowote, tatizo vyombo vya habari macho yenu ni Miss Tanzania, na hata hao walioripoti hiyo habari hawajui ukweli kuhusu taarifa hizo,” alisema Lundenga.
MWANANCHI

No comments: