ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 25, 2014

TUME YA MIPANGO YATEMBELEA BANDARI YA MBABA BAY

Na Saidi Mkabakuli, Mbaba Bay
Timu wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Tume ya Mipango imetembelea Bandari ya kimkakati ya Mbaba Bay iliyopo wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Bandari hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alisema kwamba Bandari hiyo ni muhimu kwa uchumi wa nchi kwa kuzingatia eneo la kijiografia la bandari hiyo.

“Bandari hii ni muhimu kwani kijiografia inaweza kuzifikia nchini nyingi zilizo kusini mwa nchi yetu hivyo inaweza kutumika kama lango la kibiashara miongoni mwa jirani zetu licha ya uhaba wa miundombinu yake,” alisema.

Aliwasihi wafanyakazi wanaoihudumia Bandari hiyo kufanya kazi kwa bidii bila ya kuchoka ili kuweza kuvutia wafanyabiashara na watumiaji wengine kuendelea kuitumia bandari hiyo.

Kwa upande wake, afisa bandari ya Mbaba Bay, Bw. Jarome Urio aliutaarifu ugeni huo kuwa Mamlaka ya Bandari ipo katika mkakati wa kuindeleza bandari hiyo ili kuweza kuihudumia wateja wengi zaidi.

Pia, Bw. Urio aliwashukuru wajumbe wa timu hiyo ya ukaguzi kwa kwenda kuitembelea na kujionea maendeleo ya bandari hiyo.

“Tunafarijika sana kuona viongozi wa serikali wanapokuja kututembelea kwani hali hii uongeza hamasa ya utendaji kazi wetu,” alisema.

Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) bandari ni mojawapo ya vipaumbele vitano vya kimkakati vyenye lengo la kufungulia fursa za ukuaji uchumi wa nchi ili kuweka misingi wa uchumi kwa watu walio wengi.

Vipaumbele vingine ni Kilimo ambapo lengo kuu likiwa ni kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya kuuza nje ya nchi; Maendeleo ya viwanda: Msisitizo umewekwa katika kuvutia, kuanzishwa na kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini (kama vile viwanda vya nguo, mbolea, saruji, makaa ya mawe, chuma na bidhaa za chuma) na pia sekta ya madini kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali.

Pamoja na kipaumbele cha Maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi: Mpango unahimiza kuwekeza katika elimu (hasa katika elimu ya juu na vyuo vya ufundi) na huduma za afya (kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma) katika kujenga nguvu kazi itakayotuletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii; na Utalii, Biashara, na huduma za Fedha ambapo jitihada zimewekwa kwenye uendelezaji uwezo wa kuuza katika masoko ya ndani na nje, kuongeza   idadi ya watalii na matumizi yao wawapo nchini, na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha.
Baadhi ya wajumbe wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakiingia kwenye gati la Bandari ya Mbaba Bay iliyopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Mratibu wa shughuli za ukaguzi wa miradi ya maendeleo, Bw. Senya Tuni (Wapili kulia) akieleza jambo mara walipoingia kwenye eneo la gati la Bandari ya Mbaba Bay. Wanaomsikiliza ni Mkuu wa msafara huo, Bibi Florence Mwanri (Kulia), Afisa mazingira wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bw. Julius Edward (Watatu kulia). Na kushoto ni Bw. Jordan Matonya ambae ni Mchumi kutoka Tume ya Mipango.
Afisa bandari ya Mbaba Bay, Bw. Jarome Urio (Wapili kushoto) akitoa maelezo kwa wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango walipofanya ziara kwenye bandari hiyo. Timu hiyo iliongozwa na Bibi Florence Mwanri (Kushoto).
kwa picha zaidi bofya soma zaidi
Kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence kushoto akionesha kitu kwenye sehemu ya gati la Bandari ya Mbaba Bay (halionekani).
Baadhi ya vijana wa Mbaba Bay wakijivinjari kwenye fukwe za Ziwa Nyasa
Afisa bandari ya Mbaba Bay, Bw. Jarome Urio (Watatu kushoto) akionesha sehemu ya gati iliyoofanyiwa matengenezo.
Baadhi ya utajiri unaopatikana kwenye Ziwa Nyasa. Dagaa wa Ziwa hili ni maarufu kwa utajiri wake wa lishe. Kwa mujibu wa wakazi wa Mbaba Bay, dagaa hao uuzwa hadi nje ya nchi.

No comments: