Wenyewe wanaita Krismas. Ni kipindi ambacho pia akina baba wanapunguza idadi ya michepuko kutokana na wingi wa mahitaji na akina mama nao wanaongeza orodha ya ATM ili wanone zaidi!
Uongo?
Kama utaamua kunikatalia sitakulaumu kwa sababu huenda wewe ni mmoja kati ya watu wachache ambao hawawasaliti wenza wao, lakini ninaamini pasipo shaka kwamba idadi kubwa ya wapendanao, kwa namna moja au nyingine, wanawaibia wenzao katika uhusiano wao!
Lakini hiyo siyo mada yangu ya leo, kwa sababu kuna jambo moja nimejifunza kutoka kwa jamaa zangu, hasa ninapokutana nao wakiwa na wake au wapenzi wao na wakati mwingine hata kwa uzoefu ambao ninaupata nikiwa nyumbani na mama chanja wangu.
Kuna watu wako siriaz sana na maisha, yaani hadi anapoteza muonekano wa kirafiki usoni mwake, fulltime amekunja sura. Huwezi kujua ni wakati gani anavaa sura yenye tabasamu, maana hata akiwa na mke au mume wake, ni ndita hadi unakwazika!
Ni kweli, maisha ni magumu maana hela inaadimika, ingawa viongozi wetu wanazo hadi wanaboa. Si unajua wao mamilioni ya fedha walizonazo wanaziita vijisenti?
Tunapaswa kutenganisha vitu na matukio. Ni kweli kwamba muda mwingi tunaotafuta fedha tunakuwa bize, yaani bosi anazingua, ama wateja wanaleta za kuleta na kadhalika, lakini hatimaye siku inakuwa imeisha, unarejea nyumbani kwako ambako unakutana na mwandani wako.
Sasa hasira za kazini unazihamishia nyumbani? Eti au wengine utawasikia wanakuambia, yaani mama Ojuku ndivyo alivyo, hapendi kabisa kuchekacheka!Mapenzi ni sanaa inayohitaji tabasamu na upendo ndani yake. Huwezi kuwa mtu wa kukunja sura halafu ukamdanganya mwenzako kwamba una furaha na maisha mnayoishi. Inakupasa kuonyesha hivyo ukiwa naye.
Tuelewane, simaanishi uwe mtu wa kuchekacheka ukiwa na mpenzi wako, isipokuwa tabasamu ni lazima liwe na nafasi kubwa sana mkiwa pamoja. Ni sawa, kwamba wewe unafikiria sana kuhusu maisha, kwa sababu kuna leo na kesho, huwezi kujua itakuwaje, lakini hilo ndilo la kukufanya ukunje ndita?
Ukiweka tabasamu usoni mwako, unatoa nafasi ya mwenza wako kukueleza kilicho ndani yake bila kuwa na mashaka. Usijidanganye, eti mtu wako atakuzoea kuwa wewe si mtu wa masihara na kwa hiyo akiwa na kitu chake anaweza kuniambia, hapana!
Huwezi kuwa huru kuzungumza kilichomo moyoni mwako, ambacho wakati mwingine ni cha manufaa kwa maisha yenu, kama mwenza wako amenuna muda wote. Kununa kwake kunaashiria kwamba mawazoni mwake hali si shwari na kwa hiyo unamtia wasiwasi.
Niwape siri kwamba uso wenye tabasamu, humpa uhakika mwenza wako kuwa mambo ni shwari. Hapa anaweza kukueleza hofu aliyonayo, iwe ni juu ya mapenzi yenu au hata maisha. Kama wewe ni mwanaume, mkeo au mpenzi wako anaweza kukupa wazo la kuwafanya muongeze kipato chenu akikuona ni mwenye furaha.
Au mke vilevile, kama ni mtu wa kununa muda wote, unamnyima mumeo nafasi ya kuwa wazi kwako, kimapenzi au hata kimaisha, maana anaweza kuogopa kukuambia kuhusu kibarua alichokipata sehemu, akihofia huenda utamkaripia, kwa vile hakina hadhi anayoihitaji.
Kifupi ni kwamba uso uliovaa tabasamu unakaribisha mambo mema, maana hata adui yako anaweza kuishiwa nguvu akiona muda wote wewe ni mtu unayeonyesha furaha, hata kama katika uhalisia wake, moyo wako unalia!
GPL
No comments:
Post a Comment