ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 13, 2014

uwepo mfumo wa kutuwajibisha sote watoaji na wapokeaji wa misaada -TANZANIA

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha Dorothy Mwanyika, akielezea uzoefu wa Tanzania katika eneo la Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA). Naibu Katibu Mkuu alikuwa mmoja wa wanajopo waliojadili mada kuhusu umuhimu wa ODA katika utekelezaji wa Malengo Maendeleo Endelevu baada ya 2015.
Sehemu ya washiriki wa mkutano ambao ni sehemu na maandalizi ya Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu uwezeshwaji wa raslimali fedha kwa maendeleo endelevu baada ya 2015 mkutano unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani huko Addis Ababa , Ethiopia, Naibu Katibu Mkuu Dorothy Mwanyika anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu , ujumbe ambao umeshiriki kikamilifu katika majadiliano yanayoendelea hapa Umoja wa Mataifa.

Na Mwandishi Maalum, New York

Wakati hali ikionyesha wazi kupungua kwa misaada ya  kimaendeleo na uwekezaji wa moja wa moja kutoka nchi zilizoendelea  kwenda nchi zinazoendelea. Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania  imesema ,  pamoja na kulitambua hilo,  ingependa kuona panakuwapo na mpango wa wazi  na wa muda mrefu wa kuziandaa nchi zinazoendelea kukabiliana na hali hiyo.
Naibu   Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bibi Dorothy  Mwanyika ametoa ushauri huo siku ya jumatano wakati wa majadiliano ya mada  kuhusu  nafasi ya misaada  ya maendeleo (ODA) katika kufikia malengo  ya    Maendeleo Endelevu baada ya  2015
Naibu Katibu Mkuu  alikuwa mmoja wa wanajopo  walioijadili mada hiyo  ambapo ameelezea uzoefu wa Tanzania  katika eneo hilo la misaada ya kimaendeleo, faida zake na changamoto zake kuelekea utekelezaji wa malengo mapya ya maendeleo  endelevu baada ya  2015
Pamoja na  kutoa ushauri huo, Naibu Katibu Mkuu, amekiri  kwamba  misaada ya   maendeleo ambayo Tanzania imekuwa ikiipata kutoka  kwa wadau mbalimbali  imechangia sana katika kuiongezea uwezo serikali  wa kutekeleza  mipango yake ya maendeleo ikiwamo ya utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wake.
“Misaada ya  Maendeleo ( ODA) ni muhimu sana katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania. Misaada hii ya  fedha kutoka nje  imechangia sana katika kusaidia jitihada za serikali  ya Tanzania katika mikakati yake ya kupunguza umaskini na utekelezaji wa mipango ya maendeleo, uboreshaji wa huduma za afya, elimu  na ujenzi wa miundo mbinu” amesema  Naibu Katibu Mkuu
Na kuongeza kuwa, kwa  muda mrefu  misaada kutoka nje imekuwa ikichangia kwa asilimia 40 ya bajeti ya serikali na asilimia 80  kwenye bajeti za maendeleo. Na kwamba kiwango hicho cha misaada kwa bajeti  ya Taifa  ya  mwaka 2014/15 ilikuwa ni asilimia 21  kwa mujibu wa mpango wa serikali wa kujiondoa taratibu na utegemezi kutoka misaada ya nje.

Bibi. Mwanyika amesema katika mchango wake kwamba, ingawa Tanzania  inatambua na kuthamini mchango wa ODA lakini na wakati huo huo imeanza kujipanga  kwa kuna na vyanzo mbadala vya upatikanaji wa fesha zikiwamo za biashara na uwekezaji kutokana na ukweli  kuwa misaada hiyo ama inapugua au kutotabirika.
 Hata hivyo akasema  Tanzania  ingependa kuona panakuwapo na utaratibu unaozianda nchi kama Tanzania kujiandaa na  hatua hiyo ya wahisani wa misaada ya maendeloe kujiondoka  ili  iweze kujipanga vizuri badala ya kushtukizana.
Akizungumzia zaidi kuhusu ODA,   Naibu Katibu Mkuu  ameueleza mkutano huo ambao ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu uwezeshwaji wa raslimali fedha katika utekelezaji wa  malengo  ya maendeleo endelevu baada ya 2015 utakofanyika mapema mwakani huko Ethiopia. Kuwa   kadiri siku zinavyokwenda mchakato wa ODA unazidi kuwa  wenye changamoto  nyingi.
Kwa mfano anasema , nchi zinazoendelea  Tanzania ikiwa moja wapo,  imejikuta ikilazimika kuweka  taratibu za kusimamia misaada hiyo ambayo inaambatana na usimamizi mkali kutoka kwa wadau wa  ndani na wa nje.
Amezitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja nchi zinazopokea  misaada ya maendeleo  kutokuwa na uwezo wa  kuzidhibiti nchi zinazotoa misaada hiyo.
Naibu Katibu Mkuu amesisitiza kuwa  Tanzania ingependa kuona kunakuwapo na mfumo  unaowawajibisha wadau wa maendeleo kama ule unaoziwajibisha nchi zinazopokea misaada hiyo ya maendeleo.
“Tufikie mahali  sasa kwamba, uwajibikaji uwe kwa pande zote mbili sisi tunaopokea misaada hiyo na wale wanaotupatia misaada. Lakini hali ilivyo hivi sasa serikali  yetu  ndiyo inayowajibika zaidi kuliko ilivyo kwa wahisani  na haina kauli  juu  ya kile kinachotolewa na wafadhili na kinatumiakaje  jambo ambalo si sahihi”. Amesema  Naibu Katibu Mkuu.
Aidha  akizungumzia kuhusu  usaidizi wa moja kwa moja kwenye  bajeti  kuu ya serikali ( GBS) Bibi Mwanyika alikuwa na haya ya kusemea.
“ Mfumo wa GBS ndio  ulio bora zaidi kwa nchi zinazoendelea Tanzania   ikiwa moja wapo katika utoaji wa misaada rasmi ya maendeleo ( ODA).  Hili limethibitishwa wazi na  utafiti uliofanyika  katika nchi saba kati ya mwaka 2010 na 2014, utafiti ambao umeonyesha wazi kwamba GBS inayotumia mfumo wa nchi husika unasaidia sana katika kupunguza pengo la  bajeti za kitaifa”.
 Amesisitiza kuwa Tanzania imekuwa ikisimamia katika  GBS hasa kutokana na ukweli kwamba baadhi wa wafadhili wamekuwa wakielekeza ufadhili wao katika sekta  Fulani  kama vile za nishati na kuacha sekta nyingine muhimu.
Ni kwa sababu hiyo Naibu Katibu Mkuu anasema kupitia  GBS  unasaidia sana kuzifikia sekta  nyingine ambazo ni vipaumbele vya serikali.
Katika hatua nyingine  Naibu Katibu Mkuu amesitiza haja na umuhimu wa  nchi kuwa mmiliki wa vipaumbele vyake vya maendeleo  kama njia mojawapo ya  kuondokana na umaskini na utegemezi.
Katika  majadiliano hayo wazungumzaji wengi walikubali ama kukiri kuwa  licha ya changamoto mbalimbali bado ODA  inamchango mkubwa katika uchagizaji wa maendeleo   kwa nchi nyingi. Vile vile baadhi ya wazungumzaji walielezea wajibu wa nchi zinazoendelea  wa kutokwepa wajibu wao na hasa  katika kutekeleza hadi zao wenyewe walizotoa za kuzisaidia nchi zinazoendelea katika kuboresha  uchumi na   maendeleo.

No comments: