ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 15, 2015

Dk Slaa atoa ushahidi, azungumza na mtuhumiwa baada ya kesi

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa (kushoto) akizungumza na Abeid Adam Abeid nje ya Mahakama ya Wilaya ya Hai jana. Picha na Dionis Nyato

Hai. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa ameiambia Mahakama ya Wilaya ya Hai kuwa Abeid Adam Abeid (22) aliyejifanya ni Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, alijitambulisha kwake ni Ofisa wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Wilaya ya Ulanga Abeid Kibasa.

Dk Slaa ambaye ni shahidi wa nane wa upande wa mashitaka, alitoa ushahidi huo mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Denis Mpelembwa.

Dk Slaa aliwasili katika viwanja vya Mahakama saa 4.20 asubuhi na kupanda kizimbani saa 4.41.

Moja kati ya mambo yaliyokuwa kivutio mahakamani hapo ni pale Dk Slaa alipozungumza kwa dakika kadhaa na mshtakiwa nje ya chumba cha Mahakama baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake.

Dk Slaa alidai kuwa awali mshtakiwa huyo alijitambulisha kama Jaji lakini kubaini kuwa amegundua anadanganya, ndipo akadai yeye ni ofisa.

Akitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na wakili wa Takukuru, Susan Kimaro, Dk Slaa alidai baada ya kufanya uchunguzi na kugundua mshtakiwa siyo Jaji Samatta wala Kibasa bali ni tapeli, aliamua kumtumia ujumbe usemao: “The Game is Over” akimaanisha mchezo umekwisha.

Alidai kuwa baada ya kutuma ujumbe huo Aprili 13,2012, mtuhumiwa huyo alimjibu akisema ameamini Chadema kinafuata misingi ya haki na siyo kununua haki na kutangaza kukiunga mkono.

Dk Slaa alisema baada ya mawasiliano hayo, aliwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea na kumueleza mlolongo wa tukio hilo.

Katika ushahidi wake huo, Dk Slaa alisema Aprili 10,2012 alipokea meseji kutoka kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema akimweleza kuwa Jaji Samatta alikuwa akiomba kumsalimia Dk Slaa.

Alidai kuwa alimuomba Lema namba ya Jaji Samatta na kuipiga lakini simu hiyo haikupokelewa, ila kesho yake mtu huyo aliyekuwa akijifanya ni Jaji Samatta alimtumia ujumbe usemao;

“Hali yako Bwana Slaa. Nimezungumza na Jaji Rwakibarila amesema anataka kuongea na nyie. mnasemaje?” baada ya kupata meseji hiyo alimpigia simu lakini hakupokea.

Kesi hiyo inayoendelea leo, Mahakama itatoa uamuzi mdogo endapo mshtakiwa katika kesi hiyo anayejitetea mwenyewe kortini ana kesi ya kujibu au la.

MWANANCHI

No comments: