ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 13, 2015

KAENI, ZUNGUMZENI, KAMA KUACHANA IJULIKANE MOJA!

NI Jumanne tena, naamini wapenzi wasomaji wangu mpo sawasawa kiafya, kiakili na zaidi sana kimapenzi. Mwaka 2015 ndiyo kwanza bado mbichi, ni nafasi ya kila msomaji wangu kujipanga katika mwaka huu ili kujua namna ya kutimiza malengo, hasa ya kimapenzi.

Naamini wasomaji wangu walio wengi ni watu wenye miaka inayokubalika kujitambua na kujiamulia mambo bila kuongozwa.Leo katika mada yangu nimependa kuzungumzia wapendanao kwa maana ya wanandoa au wapenzi ambao wapo kwenye misukosuko ya muda mrefu ndani ya uhusiano wao.

KWA MWAKA MZIMA
Kuna wale ambao kwa mwaka mzima wa 2014, ndani ya uhusiano kulikuwa na moto mkubwa uliotishia kuvunjika kwa uhusiano au kuishi mbalimbali kwa muda, lakini kila walipojaribu kukaa pamoja walikosa suluhu ya amani na moto kuendelea kuwaka kwa sana!

KUNDI JINGINE
Kundi jingine ni lile ambalo, uhusiano ulitibuka lakini wakashindwa kuachana kwa sababu ya uvumilivu au kutunza heshima. Hapa nazungumzia zaidi wanandoa.

Wapo wanandoa walitibuana sana lakini ‘talaka’ kwao ikawa haina nafasi kutokana na watoto au heshima katika jamii hivyo ikawabidi wavumiliane lakini mpaka mwaka huu unaingia bado wana kazi kubwa ya kutengeneza ndoa ambapo inaonekana kushindikana.Wanandoa wa kundi hili wanaishi kwa matumaini nikiwa na maana ndani ya ndoa kuna machungu mengi lakini kuachana hakupo!

KUOGA, KULA, KILA MTU KIVYAKE
Juzi nilibahatika kuzungumza na mwanandoa mmoja ambaye alisema ndani ya mwaka mzima wa 2014, ndoa yake ilikuwa kila mtu kivyake. Huyu niliyeongea naye ni mwanamke. Anasema kwa muda wote wa mwaka, mumewe anajiwekea maji ya kuoga, anakokula anajua mwenyewe, akifika nyumbani ni kulala tu!

Mwanamke huyo, mkazi wa Mabibo-Jeshini, Dar anasema:
“Nimekuwa nikivumilia hali hii kwa sababu hata nikipika chakula na kukitenga mezani, akija hali, nikiweka maji ya kuoga akirudi anajiwekea ya kwake ya kwangu anayaweka kando.
“Nimevumilia mengi lakini nadhani kwa mwaka huu wa 2015 lazima nijipange vingine ili na mimi niishi kwa amani.”

KAENI, ZUNGUMZENI, KAMA KUACHANA IJULIKANE MOJA!
Nilimshauri mwanamke huyo kwamba, ni muhimu wakakaa na mumewe, wakazungumza ili amani au mapenzi kama zamani yarejee, lakini kama itashindikana basi kila mmoja aishi kivyake ili ile amani ya moyo ihusike.

Hapa nazungumza hata kwa wanandoa wengine, kama kuna mtiti ndani ya ndoa kwa mwaka mzima, ni muhimu kwa mwaka huu kukawa na kikao hata cha familia ili mambo yazungumzwe mwanzo mwisho ili kama hakuna mwafaka basi ijulikane moja,

kwani hakuna kitu kibaya kama kuishi na presha!
Ni kwa nini wanandoa washikilie kitu ambacho kila siku kinasababisha mapigo ya moyo kudunda katika mpangilio usiotengenezwa na mwili? Wako watu wanalazwa kwa presha kwa mwaka mara saba, kisa ndoa, hapa pana jambo la kujiuliza, ndiyo maana nasema kwa mwaka huu kuzungumza kuwepo ili ikishindikana ijulikane moja!

GPL

No comments: