ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 29, 2015

Profesa Lipumba avuruga Bunge

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam jana baada ya kusomewa shtaka la kuhamasisha wafuasi wa chama hicho kutenda kosa la jinai. Juu kulia- Spika wa Bunge Anne Makinda akizungumza baada ya wabunge wa upinzani (kushoto), kusimama mfululizo wakipinga kuahirishwa kwa hoja ya kujadili suala la Profesa Lipumba kukamatwa. Picha na Edwin Mjwahuzi na Anthony Siame.

Dodoma. Kwa mara ya pili, Spika Anne Makinda jana alilazimika kuahirisha kwa muda shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kukataa kukaa, wakishinikiza kitendo cha polisi kumpiga na baadaye kumkamata Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kijadiliwe kwa masilahi ya Taifa.
Profesa Lipumba, ambaye pamoja na wanachama wengine 32 walikamatwa juzi eneo la Mtoni Mtongani wakati alipokuwa akielekea Zakhem, Mbagala jijini Dar es Salaam kuwataka wafuasi wa CUF kutawanyika kwa amani baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano, jana alikamatwa tena akiwa nje ya Kituo Kikuu cha Polisi muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana, akidaiwa kuongea na waandishi wa habari wakati akiwa mtuhumiwa.
Wakati akiwa mbaroni, Profesa Lipumba alijisikia vibaya na hivyo kupelekwa hospitali kabla ya kufikishwa Mahakama ya Kisutu jioni, akishtakiwa kwa kufanya maandamano bila ya kibali.
Jana bungeni, Spika Makinda alijikuta akipambana na nguvu ya wabunge wachache wa upinzani ya kuzuia kuendelea kwa shughuli za Bunge kama ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka jana wakati walipotumia staili hiyo ya kusimama wakati wote kushinikiza Bunge kusikiliza matakwa yao kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya wahusika kwenye sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Wakati huo ilibidi Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi, Sera na Utaratibu wa Bunge, William Lukuvi kumfuata mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuzungumza naye kabla ya Bunge kuahirishwa.
Tafrani ya jana iliyodumu kwa dakika 12 na sekunde 8 ilianza baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu. Baada ya kumalizika kwa kipindi hicho, wabunge zaidi ya watano wa upinzani walisimama kutaka kutoa hoja na Spika Makinda alimpa nafasi ya kwanza James Mbatia, ambaye ni mbunge wa kuteuliwa, aliyeomba mwongozo akitumia Kanuni ya 47 inayohusu kuahirishwa kwa shughuli za Bunge ili kujadili jambo la dharura.
Mbatia, ambaye aliisoma kanuni yote ya 47 yenye vipengele vinne, aliomba kutoa hoja ya kutaka kitendo cha kupigwa kwa Profesa Lipumba wakati akiwa katika mkutano wa hadhara, kijadiliwe.
Mbatia alisema: “Jana (juzi) tarehe 27 mwezi Januari mwaka huu wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba alikuwa na ratiba ya kufanya mkutano wa hadhara pamoja na maandamano na walifuata taratibu zote za kisheria na za kikatiba za kujumuika, kuandamana na kuweza kubadilishana mawazo.
“Cha kushangaza, dakika za mwisho polisi walikataza jambo hilo lisiendelee na Profesa Lipumba akaonyesha ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoendelea na jambo hilo, lakini Jeshi la Polisi likafika baadaye kidogo kuamua kutumia nguvu dhidi ya raia ambao hawafanyi fujo yoyote, raia ambao wameonyesha ushirikiano na utii kwa Jeshi la Polisi.”
Mbatia alisema pamoja na ushirikiano huo polisi waliamua kumpiga Profesa Lipumba na raia wengine wa Tanzania hata watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano, kauli ambayo ilifanya wabunge wampigie makofi mwenyekiti huyo wa Chama cha NCCR-Mageuzi.
Aliendelea kusema waandishi wa habari walipigwa virungu na kudhalilishwa, jambo ambalo alisema linaondoa utulivu, amani nchini.
“Mimi binafsi nilisikitika sana baada ya vyombo vya habari kuonyesha moja kwa moja. Nilichukua hatua ya kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kuwa mambo ya aina hii yalipokuwa yakitokea huko nyuma, sisi vyama vya siasa tuliwahi kumuhusisha hata Rais.”
Alifafanua kuwa walimhusisha “Rais na Jeshi la Polisi na IGP mstaafu, (Said) alituhakikishia kushirikiana na sisi kwa maazimio na Rais akatoa kauli yake, mawaziri wakashiriki. Sasa jana polisi ilitoa kauli kwamba wana maagizo kutoka juu na kuongeza:
“Sasa Spika, tusipoziba ufa, tutakuja kujenga ukuta.”
Huku wabunge wa upinzani wakipiga makofi, Mbatia aliendelea kusema: “Mwaka juzi waandishi wa habari waliuawa, Jeshi la Polisi likawa linaua raia, raia wanaua polisi, viongozi wa dini wakaingizwa huko kuuawa nchi ikafikia hali ya sintofahamu na sasa imeanza kujirudia tena kwa kasi kubwa, kwa dharau kubwa na kwa kudhalilishwa.”
Huku akipigiwa makofi, Mbatia alibainisha kuwa Profesa Lipumba ni mwenyekiti wa chama chenye wabunge wengi bungeni ambao ni zaidi ya 35 pia ni mwenyekiti wa chama ambacho kinaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, hivyo kama anaweza kudhalilishwa kiasi hicho basi haijulikani raia wengine wa kawaida wanaweza kudhalilishwa namna gani.
Jambo hilo likiachiwa liendelee, litasababisha matatizo hivyo kwa kuwa Jeshi la Polisi lilisema limepata maagizo kutoka juu katika tukio hilo, ni muhimu hilo agizo likajulikana limetoka kwa nani, kwa sababu gani na masilahi gani, alisema huku akipigiwa makofi na wabunge wenzake.
“Nilimuuliza waziri jana aniambie ni agizo kutoka juu kwa nani na kwa malengo gani,” alisema Mbatia na kuongeza: “Kwa nini tusiwekeze kwenye amani na utulivu wa taifa letu wakati tulishakubaliana viongozi wote wa (Kituo cha Demokrasia Tanzania) TCD na Rais alishiriki mwaka juzi tarehe 9 na 10 mwezi wa saba, sasa leo hii naona limeanza kujirudia na tunaona giza mbele ya safari.
“Sasa, Spika naomba kutoa hoja tuahirishe shughuli za Bunge ili tujadili (suala hili) kwa maslahi mapana ya Taifa letu, tulijadili jambo hili ili tuweze kupata majibu sahihi na tuhakikishe kwamba jambo hili halitajitokeza tena.”
Baada ya kutoa hoja hiyo wabunge wote wa kambi ya upinzani kwa ujumla walisimama kama ishara ya kuunga mkono, lakini Spika Makinda alisimama na kusema: “ Naomba mkae, naomba mkae. Hoja hii haiungwagi mkono (wabunge wakaguna aah aah aah). Jamani eeh mimi siyo kangaroo court, ninachosema hoja namna hii huwa haiungwagi mkono someni kanuni.”
Spika Makinda aliendelea kusema: “Someni kanuni na ameisoma vizuri mheshimiwa na nimefurahi ameisoma sehemu ya kanuni hiyo inasemaje, inasema hiyo kanuni ya 47(4) inasema Spika atakavyoona kwa kuzingatia mazingira ya suala lililojadiliwa.
“Kwa mazingira hayo naiagiza Serikali kesho (leo)… mimi ni Spika naomba tuelewane kesho (leo) itoe kauli kamili ambayo sisi tutaelewana halafu kesho (leo) nitaruhusu mjadala, lakini siyo leo (jana).”
Baada ya hapo Spika aliruhusu kuendelea kwa shughuli za Bunge, lakini wabunge wa upinzani walisimama na kusababisha Spika kusimama tena.
“Nimesema kesho ndiyo tutajadili na kama mnataka nendeni (kelele zikaaanza kutoka upinzani) jamani muwe na busara,” alisema huku wabunge wa vyama vya upinzani wakipiga kelele na kufanya hali ya kuelewana kupungua.
Kelele zikaendelea huku Spika akisema “hatuwezi kuanza kutukanana hapa kama mnataka kufanya mnachotaka kufanya, fanyeni… watu wazima tumieni busara mnachotaka kufanya, fanyeni lakini hamtumii busara.”
Zogo likiwa linaendelea, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Muhagama walisogea kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kujadiliana. Spika aliendelea kusisitiza kuwa Mbatia alisema vizuri kwamba suala hilo linataka amani na mshikamano. Pamoja na Spika kusema hivyo, wabunge wa upinzani walionekana kuwa wakali na muda wote wakiwa wamesimama.
Spika Makinda bila kujali kusimama kwa wabunge wa upinzani, alitangaza kuendelea kwa shughuli za Bunge kwa kumtaka katibu kusoma kinachofuatia, lakini ilishindikana kwani alipotaja hoja za Serikali hasa ya Kamati ya Hesabu za Serikali, mwenyekiti wake hakutokea huku wabunge wakiwa wameendelea kusimama na Spika akawaonya kwamba huo siyo mtindo wa kanuni.
Tafrani iliendelea huku wabunge wakisema; “Haiwezekani, haiwezekani, lazima jambo hilo lijadiliwe.” Hata hivyo, Spika alikataa kwa maelezo kuwa siyo utaratibu wa Bunge. Hali ya kutoelewana na kelele bungeni iliendelea na kila mbunge wa upinzani akisema chake huku wakiwa wamesimama.
Spika Makinda alisimama na kuwaambia tena, “Mnajua tatizo mlilonalo ninyi ni dogo sana, jambo hili ni kubwa sana,” alisema na kuamsha kelele wa wabunge wakisema, “Ndiyo maana tunataka lijadiliwe, ndiyo maana tunataka lijadiliwe.”
Spika Makinda alisisitiza akisema: “Ninachosema jambo hili ni kubwa sana na kama ni kubwa sana, hatuwezi kuzungumza kama mnavyozungumza sasa ni vizuri wabunge wote wakaelewa na kwamba mimi ndiye niliyeruhusu hoja hii ije baada ya kujadiliana na Mbatia, Tundu Lissu na Mohamed Mnyaa.”
Kelele ziliendelea na kusababisha Spika kuahirisha shughuli za Bunge hadi leo lakini akabadili na kusema tena hadi jana saa 10:00 jioni.
Akizungumzia kitendo hicho nje ya Bunge, Mbatia alisema alitegemea baada ya kutoa hoja yake Spika angeruhusu mjadala na Serikali kutoa majibu, lakini haikuwa hivyo.

“Niletegemea Waziri Mkuu asimame kutoa majibu ya Serikali, lakini haikuwa hivyo sasa hatuna jinsi (ya kufanya),” alisema Mbatia.
MWANANCHI

3 comments:

Anonymous said...

Muheshimiwa Mkinda hakufanya busara yeyote hasa baada ya Mbatia kutoa hoja kwa maana kubwa ya kunusuru amani ya Watanzania na wananchi kwa ujumla.
Hakuna sababu ya kuingiza maslahi binafsi jamani. kuna mambo mengine ni "common sense". Kwanini tunakumbatia vitendo viovu na vyenye hadhari kwa taifa? eti kwa sababu tu ya kulindana. Huu siyo uongozi bora.
Hatuna mwelekeo mzuri kwenye siku za usoni. Tunapanda chuki na hasira miongoni mwetu na hili litaangamiza Taifa la kesho. Mwalimu alisema, kwa hali hiyo, Nchi itakuwa haitawaliki.

Anonymous said...

Ama kweli maneno ya Pinda yametimia.....Piga!, Piga!
Kumbuka kwamba apigae, mwishowe naye hupigwa!, Mwenyenzi Mungu atafanya kazi yake.
So sad! Waziri Mkuu, Waziri wa mambo ya ndani mko wapi?, Amiri jeshi mkuu!

Anonymous said...

Inasikitisha saana kuona wanainchi wanapigwa fimbo kama wanyama, hata wanyama wa kisasa hawapigwi. kiongozi mkuu waziri mkuu anasubutu kusema PIGA TU...that's to bad. Hasitaili kua kiongozi hata kidogo. Sielewi alisomea wapi hiyo hana huruma kwa wanainchi wako. Hasitaili kua mkuruu.