Unga na bomba
Kasisi mmoja raia wa Australia amefichua na kuthibitisha kuwa kuna idadi kubwa ya wafungwa wenye asili ya Afrika katika magereza ya Hong Kong, wengi wao wakiwa ni kutoka Tanzania. Kasisi huyo John Wortherspoon ambaye kwa sasa anafanya ziara maalum Tanzania, amesema yeye ndiye ambaye amekuwa akisambaza barua zinazodaiwa kuandikwa na wafungwa wanaoshikiliwa kwenye magereza hayo ambapo baadhi yao wametaja majina ya watu wanaodaiwa kuwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliowatuma kusafirisha dawa hizo. Padre Wotherspoon amefika kuonana na familia za wafungwa hao pamoja na idara za serikali zinazohusika na mapambano dhidi ya biashara hiyo hatari ya dawa za kulevya. Mwandishi wetu Ben Mwang'onda anasimulia zaidi kutoka Dar Es Salaam.
Kwa muda sasa barua zimekuwa zikichapishwa kwenye mtandao zikielezea maisha ya wafungwa walionaswa na mamlaka za Hong Kong. Sasa Padre Wotherspoon amejitokeza hapa Tanzania na kusimulia zaidi maisha aliyowakuta nao wafungwa hao ambao amekuwa akiwatembelea gerezani na kuwaunganisha kwa mawasiliano na ndugu zao.
Akizungumza na BBC, Padre Wotherspoon, ambaye anajitolea kazi ya kuelimisha vijana kuhusu madhara ya biashara hiyo haramu na hatari, amesema zaidi ya Watanzania mia moja wanashikiliwa katika magereza za mamlaka ya Hong Kong kwa makosa ya kuingiza dawa za kulevya katika eneo hilo licha ya adhabu ya kifungo cha maisha au kifo kwa watu wanaokamatwa, lakini ni kwa nini aliamua kubeba jukumu hilo?
"Waafrika wengi walinyongwa katika kipindi cha miaka miaka mitatu iliyopita. Ni idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na kunyongwa. Kwa hiyo niliogopa sana. Nilijaribu kuwapata wahusika wenyewe wawambie watu kwamba wasijaribu kupeleka dawa za kulevya Hong Kong, Macau, China. Lakini waliendelea kuja.Wiki moja mwezi Julai 2013, saba walikamatwa uwanja wa ndege wa Hong Kong katika wiki moja. Katika hali hiyo nilipata ruhusa kutoka mamlaka ya magereza kuwawezesha baadhi ya wafungwa kuandika barua katika website yetu kuwaonya watu nchini Tanzania na sehemu nyingine barani Afrika kuhusu hatari ya kusafirisha dawa za Kulevya kwenda Hong Kong.
Baada ya kubaini hali hiyo Father John aliwatembelea magerezani huko Hong Kong na kuwaonya juu ya hatari inayowakabili vijana wengi barani Afrika. Lakini huwa anawaambia nini vijana hao mara anapowatembelea.
Ninawaambia andikeni kwa marafiki zenu, familia zenu, makanisa yenu, wanasiasa wenu vyombo vyenu vya habari waambieni watu waache kuleta dawa za kulevya Hong Kong kwa sababu wengi walidanganywa, waliambiwa kuwa ni rahisi kuingiza dawa za kulevya Hong Kong. Lakini ukweli ni kwamba ni vigumu sana na waliambiwa ukikamatwa utafungwa kifungo cha miaka miwili lakini ukweli ni kwamba kifungo cha chini ni miaka saba au nane.
Hata hivyo Father Wotherspoon anasema alichobaini ni kwamba licha ya tamaa ya utajiri wa haraka haraka, wengi wa vijana hao au wote walirubuniwa na vigogo wa biashara hiyo kwa kuwabebesha dawa za kulevya ili tu wakidhi mahitaji yao ya lazima kama kutunza familia zao. Amesema baada ya kuanza kampeni hiyo mwaka 2013 idadi ya vijana wanaokamatwa imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na baadhi ya vyombo vya habari nchini Tanzania kunasa habari kutoka tovuti ya Father John ya v2catholic.com
na habari hizo kusambaa haraka, ambapo amesema badala ya kuwakamata watu watatu wanne,watano kwa wiki, kwa kuanzia miezi minane 2013, ni mtu mmoja tu alikamatwa kwa karibu miezi minane katika uwanja wa ndege wa Hong Kong.
Father John anasema vigogo wa biashara ya dawa za kulevya wamekuwa wakibuni mbinu mpya kwa kuwatumia watu kutoka vijijini badala ya mijini kwa sababu watu wa vijijini hawajui hatari ya biashara hiyo au waliambiwa dakika za mwisho wakiwa uwanja wa ndege kuwa ni nchi gani walitaiwa kwenda na dawa hizo.
Baada ya kuwasili Tanzania amekutana na familia mbalimbali za wafungwa wa magereza za Hong Kong. BBC imekutana na Kamishna wa kikosi cha kudhibiti dawa za kulevya nchini Tanzania, Godfrey Nzowa ambaye amesema jitihada zinazochukuliwa na makundi mbalimbali pamoja na watu binafsi katika kuwaelimisha watu hatari ya dawa hizo ambapo mwaka jana pekee walikamata kilo mia nne za dawa za kulevya aina ya heroin na kuokoa maisha ya watumiaji karibu milioni saba ili wasiweze kuzipata na kutumia.
1 comment:
mtoto wa mfalme kijasho chembamba
Post a Comment