Kiungo wa zamani wa Simba , Ramadhani chombo 'Redondo'
Kiungo wa zamani wa Simba, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ anadai kuwa, viongozi wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara wanalichimbia kaburi na kulizika soka taratibu.
KUNA mambo kwa Tanzania yamesalia kuwa ndoto, mfano kwa timu ya Taifa kushiriki ama kutwaa Kombe la Dunia. Hili haliwezekani kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na mfumo wa soka letu.
Kiungo wa zamani wa Simba, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ anadai kuwa, viongozi wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara wanalichimbia kaburi na kulizika soka taratibu.
Redondo ambaye alisajiliwa Simba kwa mara ya kwanza 2007 akitokea Ashanti pia aliwahi kuichezea Azam FC, amejaribu kuweka wazi baadhi ya sababu hasa kwa klabu kongwe nchini Simba na Yanga kuwa mifumo yao ni mibovu huku akitoa mfano Simba kufukuza makocha watatu ndani ya miezi 12, jambo linalowafanya wachezaji kuanza upya kujifunza mifumo ya kocha na si kufanya kazi kama inavyotakiwa.
Vipaji vya soka Tanzania
Redondo anasema, Tanzania kuna vipaji vikubwa vya soka, lakini kutokana na mifumo mibovu ya uongozi ni ngumu mpira wa miguu kufikia hatua ya kushiriki michuano ya Afrika au Kombe la Dunia zaidi ya kuendelea kuwa mashabiki na kutazama mashindano hayo kwenye Runinga.
“Tatizo kubwa lipo kwenye uongozi, kila mmoja anataka kuonekana kwamba yupo juu ya mwingine, hivyo wanashindwa kusimama katika nafasi zao vizuri, mfano mzuri kocha anapaswa kuachiwa majukumu yake, lakini Tanzania unakuta meneja anataka kupanga timu, mashabiki pia wanampangia kocha, hilo linamfanya kocha ashindwe kuonyesha uwezo wake hasa kwa timu kongwe,” anasema Redondo.
Redondo anabainisha kuwa Tanzania hakuna uhaba wa watu wanaolijua soka vizuri bali wapo watu wenye ushabiki na siasa, kitu kinachozidi kudumaza mpira wa miguu nchini kwa sababu hakuna anayesimama kusema kitu juu ya hilo.
Wachezaji wa kigeni wa nini?
Redondo anashangazwa na kitendo cha viongozi wa klabu kushindwa kuthamini wachezaji wao wa ndani na badala yake kuhusudu wale wa kigeni na kusema kuwa kitendo hicho ni kama kujitengenezea sumu ya kujiua kwani wachezaji wa kigeni wanaopewa nafasi kubwa hapa nchini ndiyo wamekuwa mwiba kwa Taifa Stars pindi tunapocheza na timu zao.
“Mfano unaweza kukuta kiongozi anatamka bila aibu mpange fulani na huyu muache wanasahau kuwa hizo klabu ndizo zinazotoa wachezaji wanaounda timu ya taifa, hivyo sasa mkikutana nao wakiwa katika majukumu ya kulitumikia taifa lao timu yetu inaambulia kipigo kila wakati,” anasema.
Agoma kusujudia vigogo
Kiungo huyo anaeleza kuwa, kuna wakati mwingine mchezaji anaweza kuonekana hana nidhamu, lakini kilicho nyuma ya pazia wadau wanakuwa hawakielewi hivyo amewataka mashabiki wa soka kujua kuwa soka linatakiwa ushirikiano lakini siyo kusujudiana.
“Nimekumbana na mengi nikiwa katika harakati zangu za kufikia mafanikio, si rahisi lakini unatakiwa kuwa na moyo wa kishujaa, hilo linawashinda wachezaji wengi na kujikuta wakiwa wanatumikishwa kama vile hawana vipaji, utafikiri wameingia katika timu hizo kwa kubebwa,” anasema.
“Niligoma kufanya hivyo, siwezi kumsujudia mtu wakati natambua kazi yangu nini ipi uwanjani na ninapaswa kufanya nini.”
Atoa neno kwa Simba
“Unajua Simba ina wachezaji makini, tatizo viongozi wanapepesa macho katika kutibu tatizo lakini kutimua kocha na kuwatengenezea mizengwe wachezaji wazuri ni kudumaza tu soka.
“Kama kuna mchawi katika soka basi, mchawi huyo ni majungu, mkifikia hapo mfahamu timu kuweza kupata maendeleo na kufika mbali, itasalia kuwa ndoto, watu watabomoa badala ya kujenga,” anasema Redondo.
Mikakati yake
Kiungo huyo anasema kuwa Februari mwaka huu atatimkia Oman kucheza soka la kulipwa katika timu ya maofisa wa jeshi ya Ami baada ya kufuzu majaribio aliyokwenda kufanya mwishoni mwa mwaka jana na kwa sasa kiungo huyo anafanya mazoezi na Villa Squad inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
“Nafanya mazoezi na Villa Squad ili kulinda kiwango changu, lakini mimi nina malengo mengi katika soka kwa sababu naamini kwamba nina uwezo mkubwa, hivyo lazima nijitume kuhakikisha nafikia ndoto zangu na zitatimia, kikubwa naomba Mungu anipe uhai,” anasema.
Rai kwa wachezaji wenzake
Redondo anawataka wachezaji wenzake wapende kuthubutu kupanua mitandao ya kusaka timu za nje ili waweze kula matunda ya vipaji vyao kuliko kukaa sehemu moja na huku wakiendelea kuchanganywa na viongozi.
Anaeleza kuwa mchezaji anapokwenda kucheza nje heshima yake inaongezeka.
“Mfano mzuri Mwinyi Kazimoto anapokuja kuitumikia Taifa Stars, kuna heshima inakuwepo tofauti na yule ambaye hana uthubutu wa kujiamini kwamba anaweza kufanya jambo kubwa kuliko anavyojiona, hivyo waamke ili wawe kioo cha soka la Tanzania,” anasema Redondo.
Historia yake
Redondo alisajiliwa Ashanti United mwaka 2008 akitokea Norway ambako alikaa miaka minne, huko alipelekwa na kituo cha soka cha kukuza vipaji kwa vijana kiitwacho Dar Youth Olympic Centre (Dyoc), kilichopo Chang’ombe TCC, jijini Dar es Salaam.
Ulipofika usajili wa dirisha dogo mwaka 2010, Simba walivutiwa na mchezaji huyo na kuanza kusaka saini yake na walifanikiwa kumnasa ingawa aliichezea timu hiyo kwa msimu mmoja kisha kutimkia Azam FC, mwaka 2012/2013.
“Baada ya kuitumikia Azam FC, kwa muda huo nikarejea tena Simba mwaka 2014 baada ya hapo nikachana nao na kuendelea na maisha mengine, ambayo pia naamini kisoka nitafika mbali kwa sababu nimelelewa kituo kinachofundisha mchezo huo,” alisema.
Redondo anaeleza kuwa, mbali na timu hizo pia amewahi kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Ferraviaro Beira ya Msumbiji, lakini hakuweza kuichezea timu hiyo kwani walishindwa kufikia makubaliano na hivi karibuni alikwenda Uarabuni kutafuta maisha ya soka la kulipwa na amesema atarudi huko muda wowote kuanzia sasa.
“Katika soka kuna changamoto nyingi, kama mchezaji ninayejielewa lazima nisimamie kile ninachokiona ni sahihi juu ya maisha yangu siwezi kupelekeshwa na mtu, kwani bado ninajiamini kwamba nina kipaji na nitafanya vizuri,” anasema.
Credit:Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake