KWA mara nyingine, nchi imejikuta katika aibu nyingine ya mauaji ya kutisha dhidi ya mtoto mdogo mwenye ulemavu wa ngozi, wanaojulikana kama Albino, Yohana Bahati (1) siyo pichani yaliyotokea huko Geita hivi karibuni.
Huu ni mwendelezo wa mauaji ya jamii hii ya watu, ambao kwa miaka mingi sasa, wanasadikika kuwa chanzo cha unafuu wa maisha kwa baadhi yetu.Yapo madai kwamba baadhi ya viungo vya Albino, vinawapa utajiri au nafasi za kisiasa kwa wanaohitaji, ndiyo maana wako tayari kuondoa uhai wa wenzao ili kiu yao itimie. Siyo walemavu wa ngozi tu, bali kuna mauaji pia ya ndugu zetu wanaotafutwa kwa ajili ya viungo vyao vingine na mambo haya yametokea kwa miaka mingi sasa.
Vyombo vyetu vya usalama vinafahamu kuhusu uhalifu huu, lakini kwa namna ya kusikitisha, vimeshindwa kuukomesha, licha ya ukweli kwamba uko ndani ya uwezo wake. Jeshi letu la Polisi, ambacho ni chombo chenye intelijensia ya hali ya juu, haliwezi kuwa halijapata dawa ya kulitibu tatizo hili, ambalo hutokea kwa namna ileile, kwa watu walewale na mara nyingi, katika maeneo yaleyale.
Tunajua kuwa uhalifu huu unaandamana na imani za kishirikina na kwa maana hiyo, wahusika wakubwa walio mstari wa mbele ni hawa wanaojiita waganga wa jadi. Kama jeshi letu lingekuwa na nia thabiti ya kudhibiti genge hili la mauaji, bila shaka lingeanza na kundi hili ambalo lingewaongoza kuwapata matajiri na wanasiasa wanaotajwa kunufaika na mauaji haya.
Ni vipi Jeshi la Polisi kwa miaka yote limeshindwa kukomesha mauaji haya yanayotokea katika mikoa ya kanda ya ziwa pekee? Maana kila siku tunasikia kuhusu Albino kuuawa au kukatwa viungo vyao katika M ikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinganya na maeneo ya jirani.
Kama kwa miaka yote tumeshindwa kuwabaini waganga feki wanaodanganya watu, pamoja na wale wanaotumika kuua, basi hakuna jinsi ambavyo hatuwezi kuacha kuhisi kuweko kwa ushirika wenye shaka baina ya watu walio katika mamlaka na wauaji hawa.
Na hawa wenye mamlaka ndiyo wanaolifanya jambo hili lionekane la kawaida, ambalo linashughulikiwa kikawaida, jambo ambalo ni lazima tupige kelele za hapana kwa nguvu kubwa!
Credit:GPL
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake