ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 17, 2015

Chadema yatoa mabati 850 kwa waathirika mafuriko Kahama

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa msaada wa mabati 850 ikiwa ni ahadi iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kusaidia waathirika wa mafuriko katika kijiji cha Mwakata wilayani Kahama.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa (pichani), alisema msaada huo una thamani ya Sh. milioni 12.

Dk. Slaa alifafanua kuwa kati ya kiasi hicho cha fedha zilizonunua mabati, Sh. milioni 10 ni sehemu ya ruzuku inayotolewa na serikali kwa chama hicho na kiasi kingine ni michango iliyopatikana katika mikutano ya hadhara ya chama hicho iliyofanyika mjini Kahama.

Alisema waliamua kununua mabati hayo kutokana na kamati ya mkoa inayoratibu maafa hayo ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga, kupendekeza vinunuliwe vifaa vya ujenzi kutokana na chakula kuwapo cha kutosha.

Dk. Slaa aliwataka viongozi kuhakikisha wanasimamia vema ujenzi wa nyumba za kuduma za makazi ya wananchi wa kata ya Mwakata kama ilivyopendekezwa na Rais Jakaya Kikwete, alipotembelea waathirika hao kwani mara nyingi serikali imekuwa ikishindwa kutekeleza kwa wakati majanga kama hayo.

“Niwaombe viongozi wa mkoa kusimamia waathirika hawa wajengewe nyumba kwa muda mwafaka…Watanzania wengi tanawakatisha tamaa kutokana na kushindwa kutimiza ahadi zinazotolewa kama kule Kilosa hadi leo bado watu wanaishi kwenye mahema, tangu nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, naomba sana Shinyanga muwe wa mfano,” alisema Dk. Slaa.

Katika hatua nyingine, misaada imeendelea kutolewa kwa waathirika hao baada ya Kampuni ya Simu (TTCL), kutoa chakula na vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh. milioni tatu.

Meneja wa TTCL Mkoa wa Shinyanga, Peter Kuguru, alisema kampuni yake imeungana na Watanzania wengine walioguswa na maafa hayo kutoa msaada wa kibinadamu na kuyaasa mashirika mengine na watu mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wananchi hao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: