Kuna tatizo moja la msingi sana limekuwa likisemwa kuhusu uhusiano wa kimapenzi na wanawake wenye uwezo wa kifedha, kwamba mapenzi yao mara nyingi yamejaa dharau.
Sina uhakika na hili ndiyo maana nimeuliza hapo juu, lakini katika maisha halisi, zipo dalili za ukweli zinazoakisi jambo hili, hasa kutokana na uzoefu wa maisha ya kibantu yalivyo. Katika jamii yetu, tumeukuta utamaduni wa mwanamke kuwa tegemezi kwa mwanaume, kwamba kila kitu kitafanywa naye.
Ndiyo maana utakutana na maneno kama vile, mwanaume ndiye kichwa cha nyumba. Lakini taratibu, kadiri dunia inavyobadilika, akina mama sasa wanadai usawa toka kwa wanaume, wakidai nao wanastahili kuwa ‘vichwa’ vya nyumba, ingawa usawa huu unakuja polepole sana.
Wanawake hivi sasa ni wakurugenzi wa kampuni walizozianzisha, zikiwa imara na zenye faida kubwa. Wanaume wanapokea maagizo kutoka kwa mwanamke mwenye mali na usishangae, siku hizi kukutana na wasichana wengi wajasiriamali. Zamani walisema wanawake wakiwezeshwa wanaweza, lakini siku hizi wanasema wanaweza bila hata kuwezeshwa!
Na utamaduni huu umewafanya baadhi yao kutowapa tena wanaume heshima waliyokuwa nayo, kwa sababu kama suala ni fedha, hata wao wanazo. Fedha imepunguza sana heshima, siyo tu mwanamke kwa mwanaume, bali hata watoto kwa wakubwa zao. Unakutana na kijana mdogo mwenye fedha nyingi, adabu yake ni ndogo kwa wakubwa, ambao ni hohehahe.
Wanaume wengi hawapendi kuoa wanawake wenye fedha kwa sababu wanajua watanyanyasika. Wanaowapenda akina mama wenye nazo ni vijana wanaotaka urahisi wa maisha, lakini tunajiuliza, je, ni kweli kwamba fedha ndizo zinawafanya akinadada wawe na dharau kwa wapenzi wao?
Wapo wanazuoni wanaodai kwamba maisha ya manyanyaso wakati wa utoto yanachangia kwa kiasi kikubwa kumpa nguvu ya kutafuta fedha msichana kwa kile anachoamini kuwa kutendwa kwake kunatokana na umaskini wake.
Hivyo, anajitahidi kwa kadiri anavyoweza ili aweze kuepuka manyanyaso anayokutana nayo. Naye kwa kuamini kuwa fedha zitamfanya kuwa huru, hutumia njia zozote anazozijua ili aweze kuzipata. Umewahi kusikia wanawake majambazi? Hawa ni miongoni mwao!
Na wengi tunakubaliana kwamba mwanamke hawezi kujingiza katika vitendo vya kihalifu kama vile ujambazi bila ya sababu maalum. Wengi wao huwa na tamaa au dhiki za kawaida za maisha ambao sana sana huishia kwenye uchangudoa.
Hawa ndiyo wale wanaoleta taabu na hela zao. Lakini mwanamke aliyepata pesa kwa elimu yake, kwa ujasiriamali wake na kadhalika, hulichukulia penzi kama kitu spesho kabisa, ambacho hakina uhusiano na uwezo wake. Heshima kwa mumewe hubaki kama ilivyo na bado, maamuzi mengi ya msingi kuhusu familia hutoka kwa mwanaume.
Tatizo kubwa linalokuja kusababisha wanawake wenye uwezo kuonekana kama wenye majivuno na fedha zao, linatokana na kubadilika kwa staili ya maisha ya sasa, ambayo yanaziweka pesa katika nafasi ya kwanza kwa kila kitu. Wanaume wenye fedha huzitumia kuwadanganya watoto wadogo na kuwarubuni kimapenzi huku wenye nazo wakizitumia kudhulumu haki.
Mwanamke anayedharau watu kwa sababu ya fedha zake anaonekana tu, kwa sababu hata ongea yake, matendo yake na kadhalika na mara nyingi, wanawake wenzake wanakuwa wa kwanza kumchukia.
Na lazima tukumbuke, kuna tofauti kati ya dharau ya fedha na ile ya asili, kwa sababu wengine kiasili wamezaliwa tu kuwa na dharau. Wanaotumia fedha kama kinga watajionyesha hata kwa mtu asiyewajua atafahamu anayejigamba mbele yake ana fedha.Wakati namalizia kwa kusisitiza kuwa mapenzi hayajali kipato, nimeshuhudia wanawake wengi wenye fedha nyingi, lakini wakiwa na heshima kubwa kiasi cha kukutia woga.
GPL
No comments:
Post a Comment