Akizindua operesheni hiyo katika viwanja vya Nyampande wilayani Sengerema juzi, katibu wa Chadema Kanda ya Ziwa, Robert Bujiku, alisema watazunguka mikoa yote ya kanda hiyo kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari hilo pale zoezi litakapoanza maeneo yao.
“Ili tuweze kufanya mabadiliko lazima tujiandikishe katika daftari la kudumu la wapiga kura na kupata shahada ya kupigia kura vinginevyo hatutafanikiwa, twendeni kujiandikisha kwa wingi,” alisema Bujiku.
Naye mwanachama wa chama hicho, Hamis Tabasamu, alisema ziara hiyo iliyoanza katika kijiji cha Nyampande ilienda sambamba na uzinduzi wa ofisi 78 za kata na vijiji za chama hicho wilayani hapa ili kuimarisha utendaji wa kazi za chama.
“Hakuna kata wala kijiji kitakachobaki bila kuwa na ofisi ya chama hapa Sengerema, hii itawezesha viongozi wetu kufanya shughuli zao kwa umakini na kuimarisha chama,” aliema Tabasamu.
Hata hivyo, Alphonce Mawazo, alisema chama hicho pamoja na vile vinavyounda Ukawa vilijipanga kutoshiriki upigani kura ya maoni ya Katiba pendekezwa ambayo serikali imebahatika kuahirisha zoezi hilo.
Katibu wa vijana (Chadema) kata ya Ibondo, John Dotto, aliwaasa vijana na wanachama wengine kuacha fikra potofu kuwa siasa ni wizi na kumnufaisha mgombea na kuhamasishana kutoshiriki uchaguzi wakati ni haki ya kimsingi kwa kila Mtanzania aliye na umri wa miaka 18.
“Vijana ndiyo wenye nguvu ya mabadiliko nchini…imani ya kusema siasa ni wizi acheni fikra hizo, tujitokeze ili kufanya mabadiliko,” alisema Dotto.
Operesheni Tigitigi ikiwa na maana ya kusambaratisha kabisa CCM itajumuisha mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Simiyu, Shinyanga na Tabora itakayozunguka kata kwa kata pamoja na vijiji vyote kwa kutumia ‘chopa’.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment