Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akizungumza bungeni wakati wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki wa Mwaka 2014 na Sheria wa Makosa ya Mtandao wa Mwaka 2015 mjini Dodoma, juzi usiku. Picha na Anthony Siame
Dodoma. Hoja 22 za kupinga vifungu Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015 zilizotolewa juzi na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu jana zilisababisha kikao cha 14 cha Bunge kuvunja rekodi ya kutumia muda mrefu baada ya kumalizika saa 6.15 usiku.
Marekebisho yaliyowasilishwa na Lissu yaliungwa mkono na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika ambaye pia alikuwa na marekebisho yake katika muswada huo, hivyo wote wawili kuichachafya Serikali bila mafanikio baada ya muswada huo kupitishwa kwa sauti kubwa ya “Ndiyooo” ya wabunge wa CCM.
Kuanzia saa 12.30 jioni, Bunge lilikaa kama kamati kupitisha muswada huo baada ya kumaliza kuupitisha muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ambao haukuwa na mvutano mkali.
Mvutano wa kisheria kati ya Lissu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, naibu wake, January Makamba ulianza saa 12.30 jioni hadi saa 5.30 usiku na baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akatumia muda uliosalia kuahirisha Bunge.
Mpaka inafika saa 5.00 usiku wabunge wa upinzani waliokuwapo bungeni walikuwa 12 tu, akiwamo Lissu na Mnyika na hivyo kufanya idadi ya wabunge wote kuwa 86, wakiwamo wa CCM na mawaziri.
Kuna wakati Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge alilazimika kusimama kutoa ufafanuzi wa kina, ikiwa ni pamoja na namna ya kuvitamka kwa ufasaha vifungu vya sheria ili kukubalika na pande mbili zilizokuwa zinavutana.
Mapendekezo yote yaliyotolewa na Chenge ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaliungwa mkono na Lissu pamoja na Masaju na Wizara ya Mawasiliano.
Wakati mnyukano huo ukiendelea, Pinda alikuwa kimya akisubiri kusoma hotuba yake ya kuahirisha Bunge.
Pinda alianza kusoma hotuba hiyo saa 5.30 usiku mpaka saa 6.00 usiku, ikiwa ni baada ya Bunge kuupitisha muswada huo. Baada ya dakika 15 za kutoa matangazo mbalimbali na kuwashukuru wabunge, Spika Makinda aliahirisha mkutano huo.
Kuna wakati Lissu aliwataka wabunge kutochoka kutokana na hoja anazozitoa kusababisha kikao hicho kuwa kirefu, huku Makinda naye akiwaeleza wabunge kuwa ‘zege halilali’, akimaanisha kuwa Bunge haliwezi kuahirishwa mpaka muswada huo upitishwe na Pinda atoe hotuba ya kuahirisha Bunge.
Kati ya marekebisho 22 yaliyowasilishwa na Lissu, ni matano tu yaliyokubaliwa na Serikali huku Lissu akikubali vifungu viwili tu vilivyofanyiwa marekebisho na Serikali, akivisifia kuwa vimeandikwa kama sheria inavyotaka, lakini vingine akiviita vya ovyo na sheria inayotungwa ni mbaya yenye malengo ya kuwakomoa baadhi ya watu.
Ilivyokuwa
Hoja kubwa iliyozua mabishano ya kisheria ni muswada huo kutokuwa na tafsiri ya baadhi ya maneno yakiwamo, ‘matumizi ya mfumo wa kompyuta kinyume cha sheria’, ponografia ambayo yanatengeneza kosa kwa mujibu wa sheria hiyo.
Vilevile, ulitokea ubishi katika hoja ya kuingilia mawasiliano kinyume cha sheria ambacho adhabu yake ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua Sh5 milioni, ikipendekezwa kuwa yaingizwe maneno ‘kwa nia mbaya au kwa makusudi’, ili kuwalenga wenye nia ovu na kuwaacha wale watakaoingilia mawasiliano kwa bahati mbaya.
Mbunge huyo wa Singida Mashariki alikipinga kifungu cha 14 kinachozuia utazamaji wa filamu za ngono, akitaka kifutwe chote kwa maelezo kuwa kinawazuia watu wazima kutizama filamu hizo, isipokuwa kwa watoto.
“Filamu hizi zinaonyeshwa katika majumba ya sinema na hii ni biashara halali. Kifungu hiki kinasema ukionyesha hiyo filamu ukikutwa unatozwa faini Sh30 milioni au kifungo cha miaka 10,” alisema Lissu na kufafanua kuwa sheria hiyo inalenga kuwageuza Watanzania kuwa watawa na mapadri na si kupiga marufuku makosa ya mtandao.
Hoja ya Lissu ilitolewa ufafanuzi na Profesa Mbarawa, Makamba na Masaju, huku Lissu akisisitiza kuwa neno ‘ponographia’ halijatolewa ufafanuzi katika sheria, lakini ilipingwa na kifungu hicho kupitishwa.
Lissu pia alipinga kifungu cha 19 kinachozungumzia mauaji ya kimbari akitaka kifutwe kwa maelezo kuwa muswada huo haujaeleza mauaji ya kimbari ni kitu gani.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment