JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA
MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Nukushi: 255-22-2116600 |
|
20 KIVUKONI FRONT,
P.O. BOX 9000,
11466 DAR ES SALAAM,
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali kuwarudisha nchini
Watanzania waliopo Yemen
Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ametangaza hatua ya Serikali kuwarudisha
Watanzania waishio nchini Yemen, kufutia mapigano yanayoendelea nchini humu ya
vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Akizunguza na Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa
Tanzania nchini Oman siku ya Alhamis tarehe 16 Aprili 2015, Waziri Membe
amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania hao ambao wengi wao
ni wanafunzi, wanarejea nyumbani salama.
Zoezi la kurudisha Watanzania hao lilianza
siku chache zilizopita ambapo familia ya watu watano ilisaidiwa na kurudi
nyumbani kupitia Oman, wakati zoezi la kuwatambua na kuwaandikisha Watanzania
likenddelea.
“Nimeruhusu matumizi ya fedha ya dharura ili
kuhakikisha ndugu zetu walioko kwenye hatari na machafuko ya Yemen wanarejeshwa
salama nyumbani mara moja” alisema Mhe. Membe.
Watanzania hao ambao wengi wao hadi sasa
wameshafika kwenye miji midogo ya Sarfat na Al-Mazyouna kwenye mkoa wa Salala
mpakani mwa Oman na Yemen, walituma maombi ya dharura (distress call) kwenye
Ofisi za Ubalozi Oman, kuelezea mazingira ya hatari yanayowakabili, na kuomba
kurudishwa nyumbani.
“Kulingana na maelekezo ya Waziri Membe, zoezi
la kuwarejesha Watanzania limeanza. Nimewapeleka maafisa wa ubalozi kule Salala
ni kilometa takriban elfu moja kutoka Muscut, ambapo watahakiki na kukabidhiwa
Watanzania wote sitini na nne (64) na wataruhusiwa kuingia nchini Oman na
kuelekea Tanzania” alimaliza Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini
Oman.
Mgogoro wa Yemen unaoendelea baina ya maafisa
wa polisi waaminifu kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ali Abdullah Saleh, na
makundi ya usalama yanayomuunga mkono rais wa sasa, Abed Rabbo Mansour Hadi,
umeua mamia ya watu na kujerui maelfu.
Mhe. Membe ametoa rai kwa Watanzania wote
wenye ndugu au jamaa nchini Yemen kuchukua tahadhari na kuwataarifu watafute
msaada kupitia Ubalozini Muscat ili kujihakikishia usalama wao. Aidha ametoa
tahadhari kwa Watanzania wanaotegemea kusafiri kwenda Yemen, kusitisha safari
zao hadi hali ya usalama itakaporejea.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
16 Aprili, 2015
No comments:
Post a Comment