ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 20, 2015

Suluhu yatakiwa haraka kuhusu wahamiaji




Boti ya Italia iliyokuwa katika Operesheni ya kuokoa wahamiaji ikiwa imebeba wahamiaji walikuwa wakisafiri kwenda Ulaya

Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi ametoa wito wa kufanyika kikao cha dharura cha viongozi wa umoja wa ulaya kujadili swala la wahamiaji wanaoangamia kwenye bahari ya Meditarenean wakijaribu kuingia ulaya. Inafuatia ajali ya hivi punde ambao karibu watu 700 wanahofiwa kufa maji baada ya boti kuzama baharini kaskazini mwa Libya, kilomita 200 kutoka kisiwa cha Lampedusa, nchini Italia.
Manusura 28 wa janga la hivi punde kwenye bahari ya Meditaranean walitarajiwa kufikishwa kisiwani Sicily alfajiri ya Jumatatu. Hadi kufikia usiku, ni miili 24 iliyokuwa imeopolewa, na maafisa wa usalama kwenye pwani ya Italia, wakaipeleka kisiwani Malta.

Ni vigumu kuhakikisha idadi ya watu walioanza safari kwenye boti hiyo kutoka pwani ya Libya. Lakini walionusurika wanasema walikuwa kati ya watu 500 na 700 kabla ya kupinduka kilomita mia mbili kutoka Lampedusa, kwenye maji ya Libya.

Ikiwa idadi hiyo itathibitishwa basi hii itakuwa ndio ajali mbaya zaidi kati ya nyingi ambazo zimekuwa zikitokea karibuni kwenye bahari ya mediteranean, huku watu wakifanya safari za hatari kutafuta maisha bora ulaya.

Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi amesema zaidi ya mawakala 900 wa kusafirisha watu wamekamatwa. Alisema suluhu la tatizo la wahamiaji si kutafuta manusura baharini, bali kuwakabili mawakala hao wa kusafirisha watu, akiwaita wafanyabiashara wa watumwa wa leo. Ametaka kikao cha umoja wa ulaya ndani ya wiki moja kujadili tatizo hili kubwa.

Papa Francis kwenye misa ya Jumapili alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua ya haraka kuepuka janga lingine kama hilo.

Meli pamoja na helikopta za Italia na Malta ziliendelea na shughuli ya kusaka miili usiku kucha. Mamlaka za Sicily zinasema wengi wa abiria kwenye boti iliyozama walikuwa ni kutoka mataifa ya Algeria, Misri Somalia, Senegal na hata Zambia.

No comments: