ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 17, 2015

Ujumbe Maalum wa Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwenda kwa Sultan Qaboos wa Oman

Mhe. Bernard K. Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania akimkabidhi Mhe. Yousuf bin Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Ujumbe Maalum kutoka kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kwa Mhe. Sultani Qaboos bin Said Al Said, Mtawala wa Oman.
Makabidhiano yakiendelea huku Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Ali Ahmed saleh akishuhudia.
Waziri Membe akiwa kwenye mazungumzo na Mhe. Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman

Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa amekabidhi ujumbe maalum kutoka kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kwa Mhe. Sultani Qaboos bin Said Al Said, Mtawala wa Oman.

Ujumbe huo maalum ulikabidhiwa kwa Mhe. Yousuf bin Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje na mwenyeji wa ziara ya Waziri Membe nchini Oman, kwenye ofisi za Wizara hiyo jijini Muscat, Oman Alhamisi Aprili 16, 2015.

Makabidhiano hayo ya kihistoria nchini hapa, yalishuhudiwa na Mhe. Dkt. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Zanzibar , Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania Oman, na viongozi wengine wa nchi zote mbili na waandishi wa habari.

Baada ya makabidhiano, viongozi hao wawili na ujumbe wao walitumia fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Oman.

Viongozi hao waliahidi kukuza uhusiano na utamaduni wa nchi hizi mbili ambao unafanana kwa sababu za kihistoria. Mhe. Membe alimuelezea mwenyeji wake nia ya Serikali kujenga Ofisi za Ubalozi kwenye kiwanja chake hapa Mascut kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuwa na majengo ya Tanzania kwenye nchi mbalimbali duniani.

Aidha mradi mkubwa wa bandari ya Bagamoyo pia ulizungumzwa na viongozi hao ambapo Serikali ya Oman ni mojawapo ya mdau wa mradi huo. Wahusika wengine wa mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni Serikali ya China na Tanzania.

Mhe. Yousuf bin Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Omani alimuhakikishia mgeni wake ushirikiano wa Serikali yake kwenye hatua zote hizi muhimu za kuendeleza na kukuza uhusiano wa muda mrefu wa nchi hizi mbili.

-Mwisho-

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, 
Dar es Salaam
17 Aprili 2015


No comments: