Mvua
zinazoendelea kunyesha nakusababisha mafuriko na hasara kubwa jijini Dar es
Salaam na maeneo mengine nchini zimetajwa kuwa ni moja ya ushahidi wa udhaifu
wa miundombinu ya kweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo
ni janga kubwa duniani kwa sasa. Haya yalisemwa na FORUMCC; shirika
linalijihusisha na masuala ya mabadiliko ya Tabianchi.
Watu zaidi
ya 12 wameripotiwa kupoteza maisha mpaka sasa kutokana mafururiko hayo ambayo
yameibua hisia na maswali mengi kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali wa
mazingira wengi wakihoji nani wa kulaumiwa kutokana na mafuriko hayo.
Afisa
Miradi, Fazal Issa kutoka shirika la ForumCC ameitaka serikali na watu binafsi
kuchukua hatua thabiti katika kukabiliana na mafuriko haya ambayo
yanasababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema
kuwa serikali na taasisi zake imekuwa na kawaida ya kuchukua hatua mara baada
ya madhara kutokea badala ya kuweka mikakati ya muda mrefu ya kukabiliana na viashiria
vya athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Taasisi zenye
majuku ya kutoa tahadhari na kushughulikia majanga hasa ya mafuriko, mamlaka zinazohusika
na ujenzi wa miundombinu katika jiji la Dar es Salaam, ukusanyaji na utoaji wa
taka zinapaswa kufanyakazi kwa kushirikiana ili kutafuta suluhisho la kukomesha
maafa haya kabla hayajaleta athari kwa watu” alisema Issa.
Alisema
hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwani utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini
unaonyesha kuwa mvua kubwa zitaendelea kunyesha hadi Mei 20 mwaka huu, hivyo kuwataka
wananchi kutotupa taka hovyo na kufanyia usafi mifereji katika maeneo yao.
“Badala ya
kulalamika na kuhoji nani wa kulaumiwa kutokana na mafuriko yanayojirudia jiji
la Dar es Salaam, ni jambo la busara sasa kwa kila mwananchi kuwajibika katika nafasi
yake katika kuzuia au kupunguza kutokea kwa mafuriko hayo” alisema Issa.
Kwa upande
wake Afisa Habari wa ForumCC, Tajiel Urioh Aliwataka Watanzania kutambua kuwa mvua
na mafuriko makubwa yanayoendelea kutokea Dar es salaam na maeneo mengine
yanamahusiano mkubwa na ongezeko la Joto duniani.
“Watu
wanapuuza na kuchukulia mzaha mabadiliko ya tabianchi lakini wanapaswa
kujifunza kutokana na mafuriko haya ambayo mbali na kusababisha vifo pia
yameharibu miundombinu ya barabara, nyumba, madaraja” alisema Urioh
Tafiti
zinaonyesha kuwa joto limeongezeka kwa 0.850C duniani huku kwa
Tanzania Joto likiongezeka kwa 10C tangu mwaka 1961 jambo ambalo linasababisha
baadhi ya maeneo kupata mvua zinazozidi kiwango na kuwa na majanga kama vile mafuriko,
vimbunga na ukame.
Hata hivyo,
repoti ya Jopo la wanasayansi duniani (IPCC 2007) inaonyesha, ili kukabiliana
na uharibifu unaosababishwa na mafuriko, inategemea sana na mipango thabiti ya
mipango miji, jinsi ya kutumia ardhi, ubora wa kuweza kutabiri kutokea kwa mafuriko,
utoaji taarifa na jinsi ya kuchukua hatua.
Mafuriko ya
namna hii yaliyoleta athari kubwa ni yale yaliyotokea mwaka 2011 katika Jiji la
Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu
arobaini (40) huku yakiharibu vibaya miundo mbinu ya barabara, madaraja
na makzi ya watu.
2 comments:
Tunaweza kusema pia inachangiwa na aina mojawapo ya UFISADI unaojiendeleza nchini Tanzania. Viongozi husika hawafanyi kazi zao wakati engineers wengi tunao na kila kitu tunacho. Wananchi nao washauriwe kutotupa taka hovyo nazo zinaziba sana mkondo wa maji hasa ya mvua kali kama za masika. WATU WAWAJIBIKE.
Hayo mabadiliko ya tabia nchi yanatokea Tanzania peke yake??? Mbona hayatokei Nairobi? Ifike mahali watanzania tukubali kuwa miundo mbinu yetu ni mibovu, tuche kusingiazia mabadiko ya tabia nchi. Nchi zilizoendelea hawana mafuriko kwani huko kwao hawana mabadiliko ya tabia nchi??
Post a Comment