ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 1, 2015

Jerry Silaa ampa Magufuli mbinu za kushinda Urais

Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli akikagua ujenzi wa daraja la Chipogolo katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma katika ziara ya kutembelea na kukagua barabara ya Iringa - Dodoma. Picha na Maktaba

Dar es Salaam. Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa amemtaka Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha za Mfuko wa Barabara katika mkoa wa Dar es Salaam ili kujihakikishia kura ikiwa atagombea Urais kama anavyotajwa.
Silaa alitoa kauli hiyo juzi wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Uhuru iliyopo katika Manispaa ya Ilala. Alisema mkoa wa Dar es Salaam una wapigakura wengi wanaoweza kuamua kupita au kushindwa kwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Meya huyo kijana alibainisha kuwa Manispaa ya Ilala na zile za Temeke na Kinondoni, zimekuwa zikipata fedha kidogo kutoka Mfuko wa Barabara, licha ya kuchangia fedha nyingi kwenye mfuko huo.
“Nakuomba (Dk Magufuli) katika bajeti yako ya 2015/16 iangalie Dar es Salaam kwa jicho la huruma. Nikuhakikishie katika takwimu za makadirio ya Sensa za Watu na Makazi za mwaka 2012, jiji hili lina wapigakura 2.3 milioni sasa mzee kama yanayosemwa semwa na yenyewe yamo, hebu iangalie Dar es Salaam kwa jicho la huruma,” alisema Silaa, huku akishangiliwa na wakazi waliojitokeza katika hafla hiyo.
Silaa alisema manispaa yake inapata Sh 4.1 bilioni kwa mwaka, lakini barabara ya kilomita moja inajengwa kwa Sh2.95 bilioni, hivyo uwezo wa halmashauri hiyo kuzihudumia barabara zote ni mdogo mno.
Zungu apiga mkwara
Wakati huo huo, Mbunge wa Ilala, Azzan Zungu amewapiga mkwara wanaozengea jimbo lake, akisema kuwa hawataambulia chochote kwa kuwa yeye ni ‘dawa ya kuua wadudu.’
Zungu alisema hayo baada ya wakazi wa jimbo hilo kupongeza jitihada zake katika kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa uchaguzi.
Mwananchi

No comments: