ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 27, 2015

Dk Shein, Maalim Seif wapishana kauli waliosusia Baraza la Wawakilishi


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akikagua gwaride kabla ya kulivunja Baraza la Wakilishi katika Viwanja vya Baraza Chukwani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana. Picha na Mwinyi Sadllah

Zanzibar/Dar. Wakati Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, ameunga mkono kitendo cha mawaziri na wajumbe wa CUF kususia baraza, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amekipinga.
Kauli tofauti za viongozi hao wa ngazi ya juu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), zimekuja baada ya mawaziri na wawakilishi wa CUF kutoka ndani ya Baraza la Wawakilishi, wakisusia kujadili muswada wa Sheria wa Bajeti Kuu ya matumizi ya Serikali ya mwaka wa fedha 2015/2016.
Akizungumza na Mwananchi jana, Maalim Seif alisema wajumbe waliona njia sahihi ya kufanya ni kutoka ndani ya baraza, kwa sababu walikuwa hawasikilizwi kila wanapozungumzia mchakato unaoendelea kwa sasa wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura.
Maalim alisema anashangazwa na wajumbe wa baraza kushindwa kujadili hoja iliyojitokeza, kiasi cha kusababisha baadhi ya wajumbe kususia kikao cha bajeti.
Alisema alisema kwamba tangu kuanza kwa uandikishaji, kumekuwa na mambo yanayofanyika kinyume kabisa na sheria, yakiwamo watoto chini ya umri wa miaka 18 kuandikishwa katika daftari la wapiga kura, vyombo vya ulinzi na usalama kutumika kutisha watu huku wakiwa wamevaa ‘kininja’, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
“Ni wazi inaonyesha kwamba kuna kasoro kwenye uandikishaji wananchi kwenye daftari la kudumu na usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibar mkazi,” alisema.
Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa, SUK, Maalim Seif alisema kwamba haiwezi kuvunjika, kwa sababu hakuna wa kuivunja kwa kuwa ilipitishwa kwenye Azimio la Baraza la Wawakilishi.
Hivyo, ikiwa inatakiwa kuvunjwa ni lazima, Serikali ifuate sheria ya kuanza mchakato wa Kura za Maoni, kuuliza wananchi watoe maoni yao na kisha kufikisha tena kwenye Baraza la Wawakilishi waijadili.
Pia alisema wanasiasa wanaojadili suala la kuendelea au kutokuendelea kwa SUK, wanastahili kujiuzulu au kufukuzwa ndani ya vyama vyao.
Alisema kuwa, hoja ya CCM kutaka kufuta SUK inapaswa kulaaniwa kwani italeta machafuko Zanzibar.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa si ya CCM wala CUF tu, ni ya wananchi wote, ni makosa makubwa kudhani kuwa Serikali hiyo ni ya vyama hivyo viwili. Ilifanyika hivyo ili kutokuendelea umwagaji damu,” alisema.
“Tangu asubuhi kwa hapa Zanzibar ilifahamika kabisa kwamba nitazuiwa kuingia kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi hata watoto walijua ‘’alisema.
Alisema kisheria hatakiwi aingie kwa sababu yeye siyo mjumbe wa baraza hilo na anachotakiwa ni kupatiwa mwaliko tu,
Dk Shein avunja Baraza
Akizungumzia kutoka nje kwa wajumbe na mawaziri wa CUF, alisema haikuwa mwafaka hasa kwa kuzingatia hoja waliokuwa wakiilalamikia haikuwa na uhusiano na muswada uliokuwa ukijadiliwa, uliohusu kupitisha matumizi ya bajeti kuu ya Seikali kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Akihutubia baraza hilo kabla ya kulivunja jana Dk Shein alisema, kitendo cha kususa baraza hakikuwa cha ufumbuzi hakikuzingatia umoja wao, SUK na maslahi ya Zanzibar na kuwataka wajumbe kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba na sheria.
Rais huyo wa Zanzibar alisema matarajio yake makubwa ni kuona wajumbe wanarejesha heshima kwa chombo hicho ikiwa ni pamoja na kuwatimizia matarajio wananchhi ili waendelee kushuhudia maendeleo na ufumbuzi wa matatizo yao.
Alisema pia kuwa SMZ itahakikisha kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura, anapewa haki yake na kuwataka wanasiasa wasiwapotoshe wananchi juu ya haki ya raia ya kuchagua na kuchguliwa, na badala yake waiacha Tume ya Uchaguzi ifanye kazi yake.
Hata hivyo, Rais huyo alisema ni wajibu kwa kila mtu kuheshimu sheria na kutoa ushirikiano kwaTume ya Uchaguzi na kuhakiksiha Zanzibar inakuwa na uchaguzi huru na wa haki, huku akionya kuwa Serikali yake haitasita kumchukulia mtu yeyote hatua za kisheria ili kulinda amani ya wananchi wake.
Akizungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Dk Shein alisema mapendekezao ya Katiba inayopendekezwa itafungua mlango mpya wa uchumi kupitia uchimbaji wa nishati ya mafuta na gesi na kuwataka wananchi kujitokeza wakati wa kura ya maoni wakati ukifika.
Kabla ya kulivunja baraza, Dk Sheina alielezea mafanikio ya Serikali yake katika miaka mitano iliopita katika sekta ya miundombinu, anga, kilimo, utalii, uvuvi na uwekezaji na kueleza maeneo hayo yalioanishwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM yalielezwa kwa upana wake.
Kamati Kuu ya CCM kukutana leoShangwe ndani ya ukumbi huo ziliibuka baada ya Spika Pandu Ameir Kificho kuwatambulisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, ZEC, Salim Jecha Salim na Mkurugenzi wake, Salum Kasim Ali na wajumbe wa baraza hilo kuchukua muda mrefu kupiga makofi huku ulinzi ukiimarishwa katika Viwanja vya Baraza hilo.
Viongo wa kitaifa walioalikwa kuhudhuria hafla hiyo ni pamoja na mabalozi wadogo wa India, Italia,Uingereza, China na Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya UNDP, UNFPA,Unicef, WHO, ILO,wakiwemo wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama, viongopzi wa dini, wanasiasa na Naibu Msajili wa vyama vya siasa Zanzibar Rajabu Baraka
Mwananchi

No comments: