Muonekano wa nje wa Banda la Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania lililopo ndani ya Karume Hall wanaoshiriki katika Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam ya sabasaba yaliyoanza kurindima jana kwenye katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, barabara ya Kilwa, jijini Dar.(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog).
Afisa habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama akitoa maelezo ya taarifa mbalimbali zilizoorodheshwa kwenye jarida la vijana lililoandaliwa na Shirika linaloshughulikia idadi ya watu Duniani (UNFPA) kwa mmoja wa wakinamama aliyetembelea banda kwa ajili ya kufahamu shughuli mbalimbali na mchango wa shirika la Umoja wa Mataifa kwa serikali Tanzania.
Modewji blog team, Sabasaba
Shirika la Umoja wa Mataifa (UN), Tanzania wapo katika maonyesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar-es-salaam yaliyoanza kurindima mapema jana.
UN Tanzania ambao wapo katika banda la Karume ndani ya mabanda hayo ya Sabasaba, kutoa elimu inayolenga kuionyesha jamii mafanikio, changamoto na fursa zilizopo katika Umoja wa Mataifa ambapo mwaka huu unafikisha miaka 70 tangu shirika hilo lianzishwe.
“Huu ni mwaka muhimu sana kwani safari ya Umoja wa Mataifa ilianza mwaka 1945, hadi kufikia sasa kuwa umefikia wapi, tupo wapi na tunaelekea wapi katika kushughulikia changamoto za kidunia ikiwemo Amani na usalama, changamoto za maendeleo, changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, na changamoto zingine”, alieleza Afisa Habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama.
Aidha, alibainisha kuwa, UN ambayo imeweza kufikisha miaka 15 ya malengo ya Milenia yaliyokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja huo mwaka 2000, yanafikia kilele hapo Desemba 30, mwaka huu hivyo wakuu hao wanchi watakutana tena mwezi Septemba mwaka huu, kupanga malengo mapya ya Maendeleo endelevu (SDGs) ambayo yatakapokubalika yataanza kutumika mwakani.
“Huu ni mwaka muhimu sana. wa kuonyesha hayo mabadiliko, tumekuwa na miaka 15 ya milenia kuna vitu tumefanikiwa na tumekuwa na changamoto. Kwa hiyo malengo hayo yalikuwa ni shirikishi kutoka kwa kada zote”alieleza.
Pia alieleza kuwa katika mkutano mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi ambao utakuwa mkutano mkubwa wa 21, utakaofanyika Paris-Ufaransa Disemba mwaka huu. Wakuu wa nchi watakuja na makubaliano ya kuona watafanya nini hivyo makubaliano hayo ni muhimu sana.
Nchi zote duniani zimeona suala la mabadiliko ya tabianchi si la nadharia tena bali ni la wote kuungana kupambana nalo kwani wote tunaathirika.
Hivyo tunawakaribisha sana watanzania kutembelea katika banda letu kujionea na kufahamu na kujifunza na kwa Tanzania mwaka huu tunamalizia program yetu ya kwanza ambayo tunashirikiana mashirika yote kufanya kazi kwa pamoja (Delivering as one) katika kutatua changamoto zinazotukabili hapa Tanzania kwa kushirikiana na serikali.
Afisa habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama akisikiliza swali kutoka kwa raia wa kigeni mwenye asili ya asia aliyetembelea banda la Umoja wa Mataifa katika maonyesho ya sabasaba yaliyoanza kurindima jana katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, barabara ya Kilwa, jijini Dar.
Afisa habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama akiendelea kuwapiga msasa raia hao wa kigeni waliotembelea banda la shirika la Umoja wa Mataifa Tanzania.
Afisa habari wa kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC), Usia Nkhoma Ledama akisaidiana na mmoja wa wananchi aliyetembelea banda la Umoja wa Mataifa kwenye maonyesho ya sabasaba kukusanya machapisho na vipeperushi mbalimbali vinavyoelezea shughuli za Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania katika hatua za mwisho za kuandaa program mbalimbali zitakazokuwa zikitoa elimu kwa wananchi wakataotembelea banda hilo katika maonyesho ya sabasaba yaliyoanza kutimua vumbi jana katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, barabara ya Kilwa, jijini Dar.
Pichani juu na chini ni meza zilizosheheni ripoti, vitabu na majarida mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kwa ajli ya watanzania kujisomea na kuelimika kuhusiana na shughuli na taarifa mbalimbali za ustawi wa kidunia zinazofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment