ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 3, 2015

MCHUNGAJI ANTHONY LUSEKELO‘MZEE WA UPAKO’ -4


KUSEMA MIMI NI TAJIRI WA KUTISHA NI KUNIONEA! Mpenzi msomaji wiki iliyopita tuliendelea na simulizi hii tamu ya MJUE HUYU ambapo mhusika mkuu ni Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) lenye makao yake makuu Ubungo-Kibangu jijini Dar, Anthony Lusekelo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako.

Baada ya kusimulia historia ya maisha yake, Mzee wa Upako aliishia pale alipokuwa akifafanua kwa nini hajiiti nabii wala mtume kisha akazama kwenye kusimulia juu ya huduma na makanisa ya kiroho.
 UNGANA NAYE…
Makanisa kama haya ya kwetu (ya kiroho ya hapa nchini) kule Kongo (DR) yalishaanza miaka mingi. Kenya walishaanza miaka mingi zaidi ya sisi. Marekani kule walishaanza. Lakini sisi ndiyo kwanza tunaanza moto wa Injili. Kwa hiyo tunapata changamoto nyingi ambazo zinatokana na uelewa mdogo wa jamii yetu.

Wanasema makanisa mapya, imani zimekuwa nyingi. Mbona makampuni ya simu sasa yapo mengi? Zamani tulikuwa na kampuni moja tu ya TTCL. Leo yapo zaidi ya matatu. Tulikuwa na redio moja tu, Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD). Leo maredio kibao. Tulikuwa na chama kimoja tu cha CCM (Chama Cha Mapinduzi). Leo vipo vyama vingi. Kwa hiyo wingi wa jambo si tatizo. Hata mabaa yalikuwa machache, leo yapo mengi.

Hata bendi zilikuwa ni chache leo bendi ni nyingi kila mtaa kwa sababu dunia inakua. Kwa sababu kuna mabaa mengi na makanisa nayo ni mengi. Ni vizuri sasa tufungue makanisa mengi zaidi kuliko kufungua baa nyingi zaidi.

Hivyo changamoto zote huwa nasema ukishakuwa bondia inabidi usiogope. Mimi changamoto hizo zote naona ni kelele za mlango tu. Watu wanasema nabii wa uongo, mara najiinua lakini kwangu ni kelele za mlango tu.
Kuhusu suala la kwamba mimi ni tajiri sana, nimezungukwa na watu wengi wasiojiweza, kwanza mimi nasema basi sisi ni maskini sana kama hata Lusekelo leo naonekana ni tajiri wa kutisha basi kweli sisi Watanzania ni maskini wa kupitiliza.

Mimi naamini katika watu wanaoishi maisha ya kawaida, ninalala vizuri, ninavaa vizuri, ni maisha ambayo kila mtu anataka kuwa nayo. Mimi ni miongoni mwao. Ninaishi maisha ya kawaida sana tena sana. Lakini sina fedha ya ziada. Lakini kwenye kauli hizi wanasema mwenye chongo kwenye vipofu anaona. Kwamba, mimi nina utajiri mkubwa wa kutisha? Sidhani. Mimi ndiyo miongoni mwa Watanzania wa kawaida sana, tena sana. Sisemi kuhusu wahubiri wengine maana wapo. Nasema Watanzania kwa ujumla wao au wenye hela, mimi simo.

Najua kuna Watanzania wana maghorofa, wana majumba, wana maakaunti benki, wana maakaunti mpaka nje ya nchi. Kusema leo mimi ni miongoni mwa matajiri wa kutisha ni kunionea. Kama vile miaka michache iliyopita tulikuwa tunasalia darasani, hata kujenga jengo tulikuwa hatuwezi, tulikuwa tunaazima majengo ya serikaki, tunaitwa hawa walokole maskini hawa, ona maskini hawa. Yale mambo Mungu alikuwa anaona, ameamua kulipa kisasi, ameamua kutubariki.

Moja, uchumi wa kila kanisa, wa msingi wa makanisa ikiwezekana makanisa yote, nguzo kuu ya uchumi ni sadaka. Kama siyo za Walutheri wa Tanzania, kwani mimi mwenyewe ni Mlutheri kwa asili, tena familia yetu ni ya wale Walutheri kabisa, wale ambao huwaambii kitu kabisa. Yaani familia ya Wamisioni.

Sasa utajiri wa makanisa ukiacha miradi ni sadaka za waumini. Dini zote zinajengwa, zinasimama, wananunua viti, magari ya wachungaji, fedha ya msingi ni sadaka. Kuna tofauti sana kati ya mchungaji wa kijijini ambako kuna watu maskini, hata akiwa nao wengi sana, bado ataonekana mchungaji wa kijijini kwa sababu uchumi wa mchungaji wa kanisa ni sadaka.

Hata ukiwa Dar es Salaam, mchungaji ambaye ana kanisa Oysterbay ni tofauti kwa sababu wanaosali kule ni matajiri. Vilevile mchungaji anachunga kanisa Marekani, nchi ya watu matajiri akiwa na watu 500 ni tofauti na mchungaji anayechunga watu 500 walioko Geita, Mwanza.
Mzee wa Upako ameanza kusimulia juu ya utajiri wake.

No comments: