ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 5, 2015

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI MHE. MATHIAS CHIKAWE AZINDUA RASMI HUDUMA ZA "DUTY FREE SHOP" GEREZA KUU LILUNGU, MKOANI MTWARA

Na, Lucas Mboje, Mtwara
Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza nchini wametakiwa kutumia fursa ya maduka yenye bidhaa nafuu "Duty Free Shop" zilizofunguliwa katika Magereza mbalimbali ili kupata vifaa vya ujenzi na kujenga makazi yaliyobora na ya kudumu kabla ya kustaafu Utumishi wao Jeshini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe alipokuwa akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Magereza "Duty Free Shop" ya Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara.

Amesema kuwa Maafisa na Askari wakitumia vizuri fursa ya maduka haya kwa kununua bidhaa za vifaa vya ujenzi itasaidia kukwepa aibu inayowapata baadhi ya Maafisa na Askari baada ya kustaafu hivyo kukosa nyumba za kuishi wakitegemea kujenga kwa kutumia Mafao baada ya kustaafu.

"Serikali iliidhinisha utaratibu wa Maafisa na askari wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kusogezewa Huduma hizo za bidhaa muhimu katika maeneo yao kwa gharama nafuu kwa lengo la kuwapunguzia makali ya maisha". Alisema Waziri Chikawe.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja amesema kuwa Jeshi la Magereza limejipanga kuhakikisha kuwa linasambaza huduma hizo nchi nzima kwa ajili ya kutoa huduma kwa Maafisa na askari nchini.

Hadi sasa Jeshi hilo limekwisha kuzindua "Duty Free Shops" Nane katika Mikoa ifuatayo Dar es Salaam - Ukonga na Keko, Mwanza - Butimba, Tabora - Uyui, Kingolwira - Morogoro, Mbeya - Ruanda, Dodoma - Isanga na Mtwara - Lilungu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe(kulia) akifurahia kwenye jiwe la Msingi mara tu baada ya kuzindua rasmi duka hilo lenye bidhaa zisizo na tozo la Kodi(wa pili kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, John Casmir Minja(kushoto) ni Mkurugenzi wa Transit Military Shop, Bw. Alfazar Meghji. Uzinduzi huo umefanyika Julai 5, 2015 katika Viwanja vya Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara.
Bidhaa mbalimbali zinazopatikana katika Magereza "Duty Free Shop" ya Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara kama inavyoonekana katika picha. Duka hilo limezinduliwa rasmi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe(hayupo pichani).
Muonekano wa nje wa Magereza "Duty Free shop" ya Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara kabla ya kuzinduliwa rasmi leo Julai 5, 2015.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe akitoa hotuba fupi ya uzinduzi wa Magereza "Duty Free Shop" Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara leo Julai 5, 2015 katika Viwanja vya Lilungu, Mkoani Mtwara.



Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Magereeza kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Magereza "Duty Free Shop" Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja(kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mhe. Christopher Magala(kushoto) kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa Magereza "Duty Free Shop Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mathias Chikawe(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye uzinduzi wa Magereza "Duty Free Shop" Gereza Kuu Lilungu, Mkoani Mtwara(wa tatu kushoto) ni Kamishna Jenerali wa Magereza, John Casmir Minja(wa tano kulia) ni Mkuu wa Magereza Mkoani Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Mussa Kaswaka(wa pili kushoto) Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mhe. Christopher Magala(wa kwanza kushoto) ni Mkurugenzi wa Transit Military Shop, Alfazar Meghji.

No comments: