Tuesday, August 18, 2015

MFUMO DUME NI HAKI YA MWANAUME-2

Karibuni tena Jumanne ya leo ambapo tunakutana kuzidi kupeana elimu mbalimbali kuhusu maisha na mapenzi. Mada yetu inasema; wanaume wana haki na mfumo dume?’

Mada hii inatoka wiki iliyopita ambapo tuliishia pale wanaume wanagombana na wake zao, kwa hasira wanawamwagia maji ya moto mpaka kuwaunguza vibaya sana. Nikasema huo si mfumo dume. Ni unyama uliopitiliza. Na nikasema hata mimi napinga vikali.

Wiki hii ninaendelea kwa kusema kuwa, wanaharakati kibao, vikiwemo vyama na taasisi za wanawake, zinapigana kuumaliza mfumo dume lakini hauishi.Hauishi kwa sababu gani? Kwa sababu wanachopambana nacho sicho. Wao wanapambana na ukatili wa kijinsia lakini si mfumo dume.

KWA NINI NASEMA HIVI?

Nasema hivyo kwa sababu; mfumo dume ni mamlaka ya utawala katika uumbaji wa Mungu. Ndiyo maana wakati naanza mada hii wiki iliyopita niliweka wazi kwamba, ndani ya kueleweshana nitatumia na maneno kutoka vitabu vya Mungu.

Wakati Mungu anaumba binadamu, aliweka utaratibu wa kiutawala. Aliamua mwanaume atakuwa msimamizi mkuu wa maisha yanayomzunguka na mwanamke atakuwa msaidizi wake.

LENGO LAKE

Aliamua kufanya hivi ili kuondoa msuguano. Hata leo hii, mahali popote penye msuguano chanzo kinakuwa kukosekana kwa msimamizi mkuu au msemaji wa mwisho.Mola kwa uamuzi wake mwenyewe, aliamua kumpa mwanaume mamlaka hayo kwa sababu ndiye aliyekuwa wa kwanza kumuumba tena kwa mikono yake. Mwanamke alimuumba lakini si kwa mikono yake. Hapo pana tofauti.Hivyo basi, uamuzi wake wa mwanaume awe mkuu ulitokana na ukweli kwamba, yeye ndiye aliyekuwa na mamlaka ya kuamua lolote juu ya tawala za duniani.

TULIPOFIKA SASA

Dunia ilipofika sasa ni kipindi cha mageuzi. Wanasema nusu kwa nusu. Au 50 kwa 50. Kwamba, katika nyanja mbalimbali, wafanyakazi wakiwa wanaume hamsini, wanawake nao wawe hamsini. Hili si tatizo kwangu.
Mimi kikazi sina sababu ya kusema sana ila nasema sana maisha ya wawili. Wawe wachumba, mke na mume au wapenzi, hapo ndipo kwangu kwenye mada hii.

Nimeongea na mama Mwantumu wa Mwenge, Dar. Yeye alisema hakubaliani na wanaume kuwa wao ndiyo vichwa vya nyumba. Ulimwengu wa sasa ni wa usawa.

WANAWAKE WANAWEZA WAKIWEZESHWA

Ni msemo ambao baadhi ya taasisi za kupigania haki ya mwanawake zimeanza kuupiga vita zikisema kuwa, wanawake wanaweza bila kuwezeshwa. Awali walisema wanaweza wakiwezeshwa. Msemo huo wa mwanzo ulitokana na kujikubali lakini baadaye wakiwa katika mkakati mzito wa kupiga vita mfumo dume, ndipo wakatumia msemo mpya; wanaweza bila kuwezeshwa. Nakubaliana nao pia. Wanawake wanaweza bila kuwezeshwa.

Lakini kundi lolote lile duniani, ili liwe salama lazima kuwe na mkuu au mtu mwenye mamlaka ya mwisho. Yeye ndiye anakuwa msemaji wa mwisho bila kujali ameshauriwa na akaukataa ushauri huo.

NAKUMBUSHIA
Wakati namaliza mada hii, napenda kusema kuwa nimejitahidi sana kukwepa matumizi makubwa ya maandiko, kama ningeyatumia ingebidi nitumie muda mrefu kwa ufafanuzi.

Lakini napenda kurudia maneno yangu ya awali kwamba, kinachopigwa vita na taasisi za kutetea haki ya mwanamke si mfumo dume, ni ukatili wa kijinsia ambao wanaume wengi wamekuwa wakitumia ubabe kujeruhi, kuua, kubaka na mambo kama hayo kwa sababu tu wameumbwa kiasili wana nguvu nyingi.

Kulinganisha mfumo dume ambao ni utawala na ukatili wa kijinsia siyo sawasawa. Ukatili wa kijinsia utabaki kuwa hivyo, mfumo dume utabaki kuwa hivyo.Mwanaume anapoamua jambo ndani ya nyumba yake, anafanya hivyo kwa sababu ya mamlaka aliyopewa na Mungu kuwa yeye ndiye kinara wa maisha. Hata kama tutabisha lakini ndiyo asili hiyo. Lakini inapotokea akatofautiana na mkewe, akachukua kisu na kumchinja huo ni ukatili wa kijinsia. Anapomwona binti mdogo akambaka kwa maguvu yake, huo ni ukatili wa kijinsia.

WITO WANGU

Wito wangu kwa wanaume, tuache matumizi ya mabavu kwa wanawake na watoto. Tuache kuwapiga wake zetu, kuwanyanyasa wake zetu, maisha yawe haki sawa kwa tote. Kwenda kinyume na hivyo, matokeo yake ndiyo hayo, tunaambiwa ni mfumo dume wakati ukweli ni kwamba, mfumo dume ni mamlaka na haki ya uzawa.

GPL

No comments: