Kikosi cha Olympic Stars cha nchini Burundi kilichochuana vikali na Stend United ya Shinyanga Tanzania.
Na Dixon Busagaga, Shinyanga.
Kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Acacia iliingia mkataba wa miaka miwili na timu ya Stend United ya Mkoani Shinyanga kwa ajili ya kushiriki ligi kuu ya Vodacom ambayo inategemewa kuanza tutimua vumbi katikati ya mwezi huu. Stand United ni moja kati ya timu bora kabisa katika kanda ya ziwa ambayo imeshiriki katika ligi kuu msimu uliopita 2014/2015 na kumaliza ikiwa nafasi ya tisa.
Udhamini wa ACACIA katika misimu hii miwili ya ligi kuu itasaidia katika kuifanya timu ya Stand United iweze kufanya vizuri katika michezo yake, pamoja na kusaidia katika kuboresha programu mbalimbali za timu na kuendeleza vipaji pamoja na masuala ya Utawala.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Makamu wa rais wa Acacia aneshughulikia masuala ya kampuni, Deo Mwanyika, amesema “Kwa takriban mwaka mmoja, tumekua tukifanya kazi pamoja na Stand United. Kwa muda huo tulianzisha mchakato wa kutambua namna nzuri ya kuboresha ushirikiano wetu ili kunufaisha watu wa Shinyanga na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.
Bwana Deo amesema Msimu uliopita uliwapatia fursa nzuri ya kushuhudia uwezo wa timu hiyo hasa ukizingatia ilikua mara yao ya kwanza kushiriki ligi kuu, “Baada ya tathmini ya kina, tunadhani huu ni muda muafaka wa sisi kusaini makubaliano au mkataba wa kuidhamini na kufanya kazi pamoja ya kuikuza timu hii ya nyumbani maarufu kama “Chama la wana”.
Hivyo, Leo, Acacia tunasaini mkataba na timu ya Stand United kwa udhamini wa misimu miwili ya ligi kuu, wenye thamani ya Shilingi bilioni moja. Udhamini huu unajuamuisha shughuli za uendeshaji wa timu, kuboresha uongozi na kukuza vipaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Stand United Amani Vincent, amesema udhamini huo wa miaka miwili utakuwa chachu kwa timu yake kufanya vizuri katika ligi kuu, “Msimu uliopita tulimaliza tukiwa nafasi ya nane na kipindi hicho hatukuwa na fedha ya kutosha kuendesha timu, lakini kwa udhamini tulioupata kutoka kwa ndugu zetu wa Acacia vijana wetu safari hii watafanya vizuri zaidi.
Kampuni ya Acacia ni kampuni inayoongoza kwa shughuli za uchimbaji wa madini hapa Tanzania huku ikiwa na Migodi mitatu katika kanda ya ziwa, kupitia mradi wa “Acacia Maendeleo Fund” ambao ndio pia umetoa udhamini wa timu ya Stend umekuwa pia ukitekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo kwa Jamii hapa nchi huku kampuni hiyo ikieleza kuwa dhamira yake ni kuendelea kufanya kazi na Jamii zinazowazunguka katika kuwaletea Maendeleo wenyeji.
|
No comments:
Post a Comment