ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 13, 2015

Balozi Seif azindua mradi wa uchimbaji wa visima Chumbuni

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuzindua mradi wa uchimbaji Visima vya Maji Zanzibar unaofadhiliwa na Mtawala wa Ras Al - Khaimah hapo Chumbuni.
Balozi Seif akishuhudi kasi ya maji inayotoka miongoni mwa Visima 50 vilivyochimbwa maeneo mbali mbali ya Zanzibar hapo Chumbuni ndani ya iliyokuwa zamani studio ya Sauti ya Tanzania Zanzibar.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Rak Gas ya Ras Al-Khaimah Bwana Kamal Ataya aliyemuwakilisha Mtawala wa Nchi hiyo katika uzinduzi wa Visima vya Maji hapo Chumbuni Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Rak Gas ya Ras Al-Khaimah Bwana Kamal Ataya wa kwanza kulia akiambatana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwenda kukagua Tangi la kuhifadhia maji lililojengwa ndani ya eneo la zamani la Studio ya Sauti ya Tanzania Zanzibar Chumbuni.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Dr. Mustafa Garu aliyevaa kofia ya Buluu akimkaguza Balozi Seif kwenye Tangi kubwa la kuhifadhi Maji Chumbuni.
Muonekano wa Tangi Kubwa la kuhifadhia Maji safi na salama ujazo wa Lita Laki 200,000 katika eneo la Chumbuni Mjini Zanzibar.

Picha na –OMPR – ZNZ

Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameagiza kuanzia sasa kila Mwananchi ana wajibu wa kutambua kwamba analo jukumu la kulinda Vianzio vya Maji katika maeneo wanayoishi ili visichafuliwe kwa shughuli yoyote ile isiokuwa ya Mamlama ya Maji Zanzibar.

Alisema licha ya kwamba upatikanaji wa huduma za Maji safi hapa Nchini sio mbaya, lakini Jamii inapaswa kuwa na tahadhari katika matumizi ya huduma hiyo kwa vile ifikapo mwaka 2030 nusu ya watu Duniani kote watakabiliwa na upungufu wa Maji.

Akizindua Mradi wa Uchimbaji wa Visima Zanzibar unaofadhiliwa na Serikali ya Ras Al- Khaimah hapo studio ya zamani ya Sauti ya Tanzania Zanzibar Chumbuni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika kipindi hicho itakuwa mbaya zaidi katika Nchi za Kiafrika hasa zile zilizomo ndani ya Janga la Sahara.

Balozi Seif Alisema kwamba maji ni muhimu kwa maisha ya Viumbe hasa Binaadamu. Hivyo ni vyema wana jamii wanapaswa kukumbushana juu ya umuhimu wa matumizi bora ya maji.

Alisema wapo baadhi wa wananchi wanaojaribu kurejesha nyuma juhudi za Mamlaka ya Maji kwa kuharibu kwa makusudi miundombinu ya maji tabia inayorejesha nyuma juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutoa huduma bora ya maji safi na salama kwa Wananchi.

Alieleza kwamba upotevu wa huduma ya maji katika maeneo mengi hapa nchini haikubaliki hata kidogo jambo ambalo Serikali Kuu inatoa onyo kali kwa wahalifu wanaohusika na tabia hiyo na watakapopatikana waakiharibu miundombinu ya Sekta hiyo watachukuliwa hatua za Kisheria.

Hivyo katika kuipa nguvu ya uzalishaji Mamlaka ya Maji iweze kutoa huduma bora za maji safi na salama Balozi Seif alifahamisha kwamba Wananchi hawanabudi kujenga utamaduni wa kulipia huduma hiyo ya maji.

Balozi Seif alifahamisha kwamba malipo ya huduma hiyo muhimu ndiyo itakayoiwezesha na kuipatia nguvu na uwezo Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } kutoa huduma zake kwa ufanisi zaidi.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Chama cha Afro Shirazi (ASP) na sasa Chama cha Mapinduzi ilikuwa ikitoa kipaumbele suala la kuwapatia wananchi wake maji safi na salama mijini na vijijini.

“ Wengi wetu hapa wenye umri mkubwa ni mashahidi kabla ya Mapinduzi huduma ya maji safi na salama ilikuwa ni huduma ya wachache hasa wale waliokuwa wakiishi mji mkongwe ”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa hali hiyo imeondolewa na hivi sasa huduma ya maji safi na salama imekuwa ni haki ya wananchi wote wa Zanzibar bila ya kubaguwa maeneo wanamoishi.

Balozi Seif kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanmzibar amemshukuru Mtawala wa Nchi ya Ras Al Khaimah Emir Saud Bin Saqr Qasimi kwa msaada wake mkubwa wa Dola za Kimarekani Milioni Tano zilizosaidia uchimbaji wa Visima 50 vya Awamu ya kwanza kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar ili wapate huduma za maji safi na salama.

“ Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunamuomba Mwakilishi wa Mtawala wa Ras Al Khaimah atufikishie pongezi za wananchi wa Zanzibar kwa ukarimu wake. Maji ni uhai. Mtu anayekusaidia kupata maji hakika ni rafiki wa kweli ”. Alifafanua Balozi Seif.

Akitoa Taarifa ya Kitaalamu ya Uchimbaji Visima uliotekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Ras Al- Khaimah na SMZ Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Gharu alisema lengo la mradi huo ni kuimarisha huduma za maji safi na salama Unguja na Pemba katika Maeneo yote Mijini na Vijijini.

Dr. Garu alisema Visima 50 vilivyochimbwa katika awamu ya kwanza vimehusisha Mikoa yote Mitano ya Zanzibar chini ya Wataalamu wa Kampuni ya Chimba Wellding Construction Limited ya Mjini Dar es salaam vikienda sambamba na ujenzi wa Matangi 6 ya ujazo wa Lita Laki 200,000 kila moja yatakayounganishwa kwenye mtandao uliopo hivi sasa.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar alifahamisha kwamba kazi za ujenzi wa Visima hivyo Hamsini kwa Awamu ya Kwanza imekwenda kwa mafanikio makubwa.

Akitoa salamu za Mtawala wa Ras AL Khaimah Emir Saud Bin Saqr Qasimi Mkurugenzi wa Kampuni ya Rak Gas Bwana Kamal Ataya aliipongeza Serikali ya Mainduzi ya Zanzibar kutokana na mashirikiano iliyotoa katika kufanikisha mradi huo katika awamu ya kwanza.

Bwana Kamal aliahidi kwamba Serikali ya Ras Al Khaimah kupitia Kampuni hiyo imeahidi kukamilisha kugharamia awamu ya pili ya Uchimbaji wa Visima 50 vilivyobakia kutokana na Mkataba uliofungwa.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Rak Gas ambae pia ni Mwakilishi wa Mtawala wa Ras Al Khaimah alifahamisha kwamba juhudi za sasa ni kukuza mashirikiano yaliyotiwa saini na Mtawala wa Ras Al Khaimah Emir Saud Bin Saqr Qasimi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein alipofanya ziara Nchini humo Novemba 10 Mwaka 2011.

Mapema Mkurugenzi wa Kampundi ya Rak Gas Tawi la Zanzibar Bwana
Ishengoma alisema katika kuimarisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kwa karne kadhaa zilizopita Ras Al Khaimah itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha miradi ya Maendeleo na kustawisha maisha ya Watu wake.

Bwana Ishengoma alisema Mradi huo wa uchimbaji Visima 100 vinavyokadiriwa kugharimu Dola za Kimarekani Kati ya Milioni Tano na Sita utakwenda sambamba na utekelezaji wa makubaliano ya kupatiwa fursa za masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa Zanzibar itakayogharamiwa na Nchi hiyo.

Mkataba huo wa utekelezaji wa Sekta ya elimu utaogharimu Dola za Kimarekani Milioni Nne utatekelezwa kwa pamoja na Sekta ya Afya kwa kuishirikisha Jumuiya ya Al Rahma.

Mapema akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuuzindua mradi huo wa uchimnbaji Visima Zanzibar Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Zanzibar Mh. Ramadhan Abdullah Shaaban alisema kwamba Wizara hiyo inakusudia kuona tatizo la huduma ya maji safi na salama hapa Nchini litabakia kuwa Historia.

Waziri Shaaban alieleza kwamba mradi huo wa Visima unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Ras Al Khaimah kupitia Mtawala wake Emir Saud Bin Saqr Qasimi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010.

Visima 50 vilivyochimbwa kwenye mradi huo katika awamu ya kwanza kila kimoja kina uwezo wa kutoa maji Lita 17,000 kwa saa moja wakati Matangi Sita yaliyojengwa ndani ya mradi huo yana uwezo wa kutunza Maji Lita Laki 200,000 kwa kila Tangi.

No comments: