Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Balozi Mpya wa India aliyepo Nchini Tanzania Bwana Sandeep Arya aliyefika Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Balozi Mpya wa India Nchini Tanzania Bwana Sandeep Arya aliyekaa kati kati katika azma ya kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa Kihistoria kati ya pande hizo mbili. Aliyekaa mwanzo kutoka kushoto ni Balozi Mdogo wa India aliyepo hapa Zanzibar Bwana Setandar Kumar. Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba yapo mambo mengi ambayo Zanzibar na India zinaweza kushirikiana katika kuimarisha ustawi wa Kiuchumi na Kijamii wa Wananchi wa pande hizo mbili.
Alisema ushirikiano katika sekta za Viwanda Vidogo vidogo,Kilimo cha umwagiliaji pamoja na taaluma kwa Watumishi wa Sekta ya Umma kupitia mfumo wa ubia unaweza kuanzishwa na pande hizo mbili kwenye Sekta ya uwekezaji ambayo Zanzibar imeshaimarisha miundombinu kwa hivi sasa.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Mpya wa India aliyepo Nchini Tanzania Bwana Sandeep Arya aliyefika Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi.
Alisema Mafunzo ya Kitaalamu katika kuendeleza Kilimo cha Mwagiliaji ni moja kati ya sekta iliyokusudiwa kuimarishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar licha ya uwepo wa mabadiliko ya Tabia Nchi Duniani ambayo India inaweza kusaidia Kitaalamu.
Balozi Seif alisema zaidi ya asilimia 80% ya Wananchi wa Zanizbr na Tanzania kwa ujumla wanategemea maisha yao katika sekta ya kilimo kiasi kwamba Serikali imelazimika kujenga miundo mbinu imara katika sekta hiyo ili kuwajengea uwezo Wananchi hao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuomba Balozi wa India Nchini Tanzania kutumia nafasi yake ya Kidiplomasia katika kuyashawishi Makampuni na Taasisi za Kibiashara za Nchi hiyo kuanzisha miradi yao Zanzibar kwa lengo la kuunga mkono jitihada za SMZ za kuimarisha uchumi.
Alisema Zanzibar inahitaji ViwandaVidogo vidogo ili kwenda sambamba na rasilmali pamoja na mali ghafi zilizomo zitakazokwenda sambamba na Viwanda hivyo ili kunyanyua uchumi wa Taifa pamoja na kupunguza changamoto ya ajira inayowasumbua vijana wengi wanaomaliza masomo yao.
Balozi Seif ameipongeza Serikali ya India kwa jitihada inazoendelea kuchukuwa za kuisaidia Zanzibar katika Nyanja za Kilimo, Elimu na Afya mambo ambayo yamewawezesha Wananchi wa Zanzibar kupiga hatua kubwa ya Maendeleo.
Mapema Balozi wa India Nchini Tanzania Bwana Sandeep Arya aliyeanza kazi karibu miezi Mitatu iliyopita alisema Tanzania India zina uhusiano wa mrefu wa kihistoria uliodumu kwa karibu miaka 200 iliyopita.
Bwana Sandeep alisema uhusiano huo unatokana na maingiliano ya Kibiashara kati ya pande hizo mbili ambapo wafanyabiashara wa sehemu hizo walikuwa wakitumia majahazi katika kusafirisha bidhaa zao.
Katika kuendeleza uhusiano huo Balozi wa India Nchini Tanzania alisema ipo haja ya kuwaunganisha pamoja wafanyabiashara wadogo wadogo wa India na Zanzibar kupitia Vyama vyao vya wafanyabiashara kwa nia ya kuongeza mapato.
“ Nitajaribu kuyashawishi mashirika, Makampuni na Taasisi za Uweakezaji Nchini India kuangalia fursa za Uwekezaji zilizopo Zanzibar ili zitumie nafasi hiyo katika kuanzisha miradi yao ya Kiuchumi hapa Zanzibar ”. Alisema Balozi Sandeep.
Alieleza kuwa ipo miradi ya Ubia ya uwekezaji ambayo tayari Taasisi za kiuchumi na Kijamii kati ya India na Tanzania zimeanza kushirikiana, akatolea mfano mradi wa Hospitali unaosimamiwa kwa pamoja kati ya Hospitali ya Apolo ya India na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF }.
No comments:
Post a Comment