ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 7, 2015

MAGUFULI AOMBA KURA ZA PIPOZ ALETE MABADILIKO


Mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli akiwahutubia wakazi wa Manispaa ya Morogoro na vitongoji vyake katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, jana. Picha na Juma Mtnada

Morogoro. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesema anataka kuwa rais wa Watanzania wote na kuwataka wafuasi wa kaulimbiu ya peoples inayoitikiwa power (nguvu ya umma), akimaanisha Chadema, wampe kura ili alete mabadiliko.

Katika kampeni zake, Chadema, kilichoungana na vingine vitatu kuunda Ukawa, kimekuwa kikisisitiza mabadiliko katika uchaguzi huu kwa kumchagua mgombea wake, Edward Lowassa.

“Kuna hawa watu wanatumia neno peoples halafu wanaitikia power... sasa nipeni hiyo power nifanye kazi. Uwe Chadema, CUF au ACT – Wazalendo, mimi kwangu ni kazi tu kwa maendeleo ya watu wote,” alisema na kuongeza: “Hivyo wale wa Chadema wanaosema ‘people’s power’ wanipe hiyo ‘power’ (nguvu) ili niwe rais wao, CUF nao huwa wanakunja ngumi wakimaanisha tano, wanipe hiyo miaka mitano nikawaletee maendeleo na wale CCM wanaonyesha dole gumba kubwa basi wanipe kura nyingi niweze kuleta mabadiliko bora, “ alisema.


Kauli hiyo ya Dk Magufuli imekuwa ikichagizwa mara kwa mara na wito kuwa maendeleo ni changamoto na hayana chama, dini wala kabila akiwataka vijana wasiharakie mabadiliko yasiyokuwa na tija.

Makamba awashukia Lowassa, Sumaye

Aliyekuwa Katibu wa CCM, Yusuph Makamba amemshukia mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa kuwa alikataliwa kuwa mgombea wa chama hicho tangu mwaka 1995.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kwenye majukwaa ya kampeni mwaka huu, Makamba aliyesema alikuja kwa kazi moja tu ya kuwaelezea anavyomfahamu Lowassa alisema hakutosha kuwa rais wakati huo na hata sasa.

Akimzungumzia, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye alisema Rais Benjamin Mkapa alikuwa mvumilivu kwa kuwa alimpa wadhifa huo kwa hisani na alitumia madaraka yake kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi.

Kabla ya mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kupanda jukwaani, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete aliwataka wananchi kutodanganyika kwamba yupo aliyeonewa kwenye mchakato uteuzi wa chama hicho akisema hata Lowassa alipiga kura kupitisha jina la Dk Magufuli baada ya mchakato wa awali kupita.

“Tulijadiliana tukakubaliana tukatoa watu watano na Lowassa alipiga kura, Magufuli alipata kura nyingi, hata walipoingia kwenye tatu bora alipata kura zaidi ya 2,000 anakubalika anazo sifa zote na kutosha kuwa rais, nikistaafu nikamkabidhi Magufuli nakwenda kulala kwa amani,” alisema.

Dk Magufuli na mabadiliko

Akizungumza na wakazi waliofurika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dk Magufuli alisema Tanzania ina watu milioni 50, lakini ni wachache wanaobana uchumi na kuahidi kupambana nao.

Alisema Watanzania wanataka mabadiliko ambayo yatapatikana ikiwa tu watafanya kazi kwa bidii na kuleta maendeleo.

“Hata mimi ninataka mabadiliko, ninataka kuona Watanzania wafanya kazi, siyo wanaoingia saa 2.00 asubuhi na kutoka saa 3.00 asubuhi... ninataka wananchi waishi kwa raha, mabadiliko yao wayafurahie,” alisema na kuongeza:

“Tanzania inahitaji mabadiliko siyo bora mabadiliko, nimekuwa waziri kwa miaka 20 sijawahi kufukuzwa wapo wengine wakijaribu miaka miwili tu wanafukuzwa, ninafahamu nini cha kufanya hasa katika kuwashughulikia mafisadi na wengine wameanza kukimbia. Ninaitwa Magufuli ili kuwafunga mafisadi.

“Hii inawezekana ingawa wengine wanasema inawezekana mimi nisiwe mwanasiasa mzuri mimi kwangu ni kazi, baraza la mawaziri litakuwa baraza dogo lakini hao mawaziri watakuwa hiiiiii.... watachapa kazi.”

Aliwavunja mbavu wananchi waliohudhuria mkutano huo alipotaja idadi ya mifugo mbalimbali wakiwamo mbwa na kusema idadi yao ni zaidi ya milioni 4.5, hivyo anajua mahitaji ya ardhi yaliyo makubwa katika mikoa mingi ikiwamo Morogoro ambako kuna migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Awali, akiwahutubia wakazi wa Ruaha, Kilosa jana Dk Magufuli aliahidi kuongeza idadi ya viwanda vya sukari akisema: “Unapokuwa na kiwanda kimoja tu cha sukari, kinaanza kujidai na kujiona chenyewe ni chenyewe, katika serikali ya Magufuli nitajenga viwanda vikubwa, vya kati na vidogovidogo.”

“Hakuna sababu miwa inalimwa hapa halafu bei ya sukari inauzwa sawa na Dar es Salaam. Kama kiwanda kiko hapa kwa nini bei ya sukari isiwe ya kiwandani? Hii ni kwa sababu sukari inatoka hapa inakwenda Dar es Salaam na tena kurudishwa hapa, kwenye serikali yangu hilo halitakuwepo, “ alisema na kushangiliwa.

Bila kuwataja majina, Dk Magufuli aliahidi kuwashughulikia vigogo wenye mashamba makubwa yasiyofanyiwa shughuli zozote za kiuchumi katika mikoa ya Morogoro na Tanga huku wananchi wakitaabika kwa kukosa ardhi.

Alipoingia Mikumi alipokewa kwa shangwe katika eneo hilo ambalo upinzani unaonekana kuimarika baada ya msanii wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Haule ‘Profesa Jay’, kujitosa kugombea ubunge kupitia Chadema akipambana na Jonas Nkya wa CCM.

Akiwa hapo, Dk Magufuli alisema kazi yake kubwa ni kupambana na mafisadi ambao ni wachache lakini wana fedha nyingi wakati wengine hawana hata kidogo.

“Hata wakati huu wa kampeni kuna watu wameweza kununua mabasi 30 wamepata wapi fedha kama hawajaiba humuhumu serikalini? Nikipata urais nitawashughulikia wote,” alisema mgombea huyo.

Kama ilivyo ada, mgombea huyo ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, akiwa Kilosa aliahidi kujenga kwa lami Barabara ya Kilosa - Mikumi na ile ya Dumila - Handeni, Tanga ili wafanyabiashara wanaotoka Arusha kwenda Nyanda za Juu Kusini wasipitie Chalinze mkoani Pwani.

Mmoja afariki kwa msongamano

Wakati huohuo, mtu mmoja amefariki dunia na wengine wasiopungua 15 kuumia baada ya kutokea msongamano wakati wa kutoka nje ya Uwanja wa Jamhuri baada ya kumalizika kampeni hizo jana.

Muuguzi wa zamu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Fatuma Hassan alisema watu saba walipatiwa matibabu akiwamo mtoto mmoja alijeruhiwa kichwani na kwamba hali yake ni mbaya.

Nyongeza na Lilian Lucas

MWANANCHI

6 comments:

Anonymous said...

Anawadangaya huyo, mfupa uliowashinda waliopita yeye atauweza, yaani hawa watanzaia shida na tabu zote wanazozipa na mateso yote yanayowakabili leo wamesahau? ama kweli sisi ni vichwa vya ujinga

Anonymous said...

1) Wananchi wanaambiwa km hawana hela ya kulipa kwenye kivuko wapige mbizi
2) kitanda kimoja wagonjwa 5
3) Hospital dawa hakuna
4) Kina mama wanajifungulia chini
5) Ukidai haki yako serikali lazima uhukumiwe kwa kipigo
6) Usomi wako peleka huko,utakaa na vyeti vyako mpk vitaliwa na mende
Hakuna ajira.


Ni baadhi na shida tu za wananchi wakitanzania, lakini leo wamesahau wanasema funika kombe mwanaharamu apite

Anonymous said...

Mmm usisatajabu ndugu yng vijikanga, vitenga, t-shirt na elfu tano tano ndio vinatusaulisha yote hayo.

Anonymous said...

Magufuli ni suluhisho la matatizo yote ya kiuongozi na maendeleo yanayoikabili Tanzania na kamwe dk magufuli hakuwahi kumdanganya mtu siku zote amekuwa ni mtu mkweli na mwenye kutenda anachokisema la kujiuliza hapa kama kweli watanzania wapo tayari kuongozwa na kiongozi mwenye kiwango cha juu cha utendaji kama magufuli au la? Tuwe wakweli watanzania si watu tunaopenda kiongozi anaetutaka tutimize majukumu yetu kikamilifu . Kwetu sisi kiongozi kama huyo ni adui na tupo tayari kumfanyia kila aina ya mizengwe atimuliwe. Mfano mzuri angalia wale makocha wakizungu wanaokwenda kufundisha soccer kule nyumbani na jinsi wanavyoondoka kimizengwe kwa malalamiko ya wachezaji kuwa ni wakali si ajabu kila mchezaji anaejaribu majaribio nje ya nchi anafeli. Sisi tumezoea kudanganya na kudanywa hata mtu akija kutuambia ukweli ni vigumu kumuamini. Ulaya kumekuwa kuzuri si kwa njia ya mkato bali wananchi wao walijitolea kufanya kazi kwa bidii kuanzia raisi wa nchi hadi mtu wa manispaa wote wanafuata kanuni na sheria za kazi kikamilifu. kama masaa yako ya kazi ni manane basi hapana ubabaishaji hapo kila sekunde na kila dakika unatakiwa kuifanyia kazi. Labda tuseme ndio siasa na hiki kitu tunachokiita democracy kila mwenye wazo lake la kufikiri mwaache afanye hivyo kwa uhuru wake lakini kati ya lowasa na magufuli? Watanzania tutafanya vichekesho vya dunia kama itakuja kutokea kumchagua lowasa. Tumeshatoa maoni yetu hapa kama ingelikuwa nchi zinazojitambua basi lowasa hata udiwani asingepitishwa kukogombea kutokana na tuhuma zinazomtuhumu za ubadhirifu wa mali ya uma . Na tunaposema tuhuma kwa nchi kama marekani inakuwa tuhuma kweli lakini tunaposema tuhuma kwa nchi kama Tanzania inamaanisha hilo jambo ni la kweli hasa ukichukilia huyo mtu alikuwa waziri mkuu wa nchi alizungukwa na nguvu nyingi kuizuia mikondo ya sheria kutofanya kazi yake kikamilifu.

Anonymous said...

Wewe ndugu hapo juu, off course ni vizuri kutoa maoni yako as you want but for most part if not all, I totally disagree with you. Unavyotaja Lowasa kuwa mbadhirifu wa mali ya umma, naomba urudi nyuma kidogo na kujiuliza swali hili moja TU. Je alikuwa peke yake?? Yeye alijiwajibisha na kujiondoa na kwa taarifa yako kwa ustaarabu alio nao katika kampeni anazozifanya sasa hivi bado hataji timu nzima iliyojihusisha na huo ubadhirifu. Ila aligusia wakati mmoja kuwa yupo mkubwa aliyejihusisha ambaye alikuwa ndiye mpiga kipenga. ccm wanachoomba sana Mungu kwa sasa hivi ni Lowasa asipite ili asije kuwawajibisha wale wakubwa waliojihusisha na ubathirifu na bado wako vipambe vya ccm kwa maneno mengine ccm inawafunika kwa kila hali. Ukija kwa ndugu yetu Magufuli, don't give me wrong he's at least a good guy, lakini nikuulize swali moja hapa je Mwinyi, Mkapa na Kikwete walipokuwa wakigombea urahisi during their first times, hawakuitwa ni waadilifu, watiifu, wachapa kazi na kila aina za sifa??? Tell me what happened after they became presidents?? Wengine wameiuza na kuozesha nchi to the lowest level. So unaponitajia hizi sifa zote za Mr. Magufuli, endelea tu lakini ubaya kwake bado yuko kwenye uozo wa ccm with all the terrible things ccm has done to this innocent country. Na watu wengi wamechoka nayo. Tanzania deserves ANYTHING better than ccm at this time.

Anonymous said...

Tatizo sio CCM hata kidogo kwani unafikri Dk slaa kakimbia upizani tatizo chadema au ukawa hapana , isipokuwa baada ya kubaini kuwa amezungukwa na watendaji wa hovyo na kuongezeka ufisadi ndipo dk slaa alipo fanya maamuzi magumu ya kuinusuru heshima yake. Na hakuna chama chenye misingi imara barani Africa kama CCM na kama huamini fanya research alafu tukutane hapahapa. Na magufuli ni zalio jipya la kuisafisha CCM na Tanzania kwa ujumla sio lowasa. Tatizo watendaji wasio waadilifu kama akina lowasa. Nashangaa vijana wengi tunawategemea kuwa smart generation wanapoteza muda wao kumtetea lowasa baada ya kupinga kwa nguvu zote lowasa kuinunua chadema na kukiuka misingi ya kidemokrasia kwa kujipigia kura yeye mwenyewe binafsi kuwa atakuwa mgombea pekee wa upizani...just wanna say shame on every body who think that was the right thing for him to do lol. Na mara tu lowasa alipojiunga na ukawa tayari chadema na washirka wake wameshakuwa( corrupted) na walishapoteza ground point ya kwamba wao ni wapamabanaji juu ya ufisadi kitu ambacho ndicho kilichowafanya waaminike na wananchi. And in reality once you start losing a grip in your long time fighting strategies you're about losing the battle as well no doubt bout it.