ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 12, 2015

Magufuli atangaza kiama.

Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli, amesema akichaguliwa kuwa rais atakomesha tabia ya kuhamisha watendaji wabovu walioharibu sehemu moja kwenda nyingine na badala yake atawafukuza kazi moja kwa moja.

Aliyasema hayo jana kwa nayakati tofauti wakati akiwahutubia wananchi wa Nyamongo na Tarime Mjini wilayani Tarime mkoani Mara ikiwa ni siku yake ya pili ya ziara ya kampeni mkoani hapa.

Alisema tabia hiyo imekuwa ikichangia kwa kiwango kikubwa kuchelewesha maendeleo ya wananchi na kuahidi kuwa utaratibu huo utafika mwisho iwapo atachaguliwa kuingia Ikulu.

“Unakuta mtu kaharibu Tarime anapelekwa Mwanza, akiharibu Mwanza anahamishiwa Tanga, kwenye serikali yangu hakutakuwa na utaratibu mbovu kama huo, ukiharibu sehemu moja ujue umeharibu maisha yako yote, kwangu ni kazi tu, ukiondoka umeondoka hakuna kuhamishwa,” alisema na kuufanya umati uliokuwa ukimsikiliza kulipuka kwa shangwe.

Wakati huo huo, mgombea ubunge jimbo la Tarime, (CCM), Christopher Kangoye, amepata wakati mgumu mbele ya Dk. Magufuli, baada ya baadhi ya wananchi kumkataa wakati akimtambulisha kwenye mkutano.

Tukio hilo lilitokea jana kwenye moja ya vijiji vya Nyamongo wilayani Tarime mara baada ya Dk. Magufuli kumtambulisha mgombea huyo wa ubunge na wale wa udiwani kupitia CCM.

Dk. Magufuli alimshika mkono na kumwombea kura Kangoye akisema ni mtu mchapakazi na mwadilifu ambaye aliamua kuacha kazi yake ya ukuu wa wilaya ili kuwatumikia wananchi wa Tarime.

Kauli hiyo ilisababisha miguno na kelele za hapana kutoka kwa baadhi ya wananchi hao hali iliyomfanya Dk. Magufuli kuingilia kati na kuwasihi wamchague kutokana na rekodi yake nzuri ya utendaji ndani ya chama na serikalini.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti wakati Dk. Magufuli alipowauliza wananchi hao ni wangapi watamchagua yeye kuwa rais wa awamu ya tano kwani umati huo uliokuwa ukimsikiliza ulilipuka kwa shangwe na vigelegele huku wakiimba nyimbo za jembe, jembe, jembe wakiwa wamenyoosha mikono juu kuonyesha kuwa watampigia kura za ndiyo.

Kangoye wa CCM ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, anachuana vikali na mgombea wa Chadema, John Heche, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Vijana wa Chadema (Bavicha).

Mgombea huyo wa CCM aliwahi kuwania ubunge kupitia chama hicho na kufanikiwa kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, lakini aliangushwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, marehemu Chacha Wangwe.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliibua shangwe na nderemo baada ya kummwagia sifa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, marehemu Chacha Wangwe.

Mgombea huyo wa urais alisema marehemu Wangwe alikuwa mchapakazi na mtu anayejali na kufuatilia kwa karibu shida na matatizo ya wananchi wa jimbo lake na kwamba haoni shida kumsifu licha ya kwamba alikuwa chama cha upinzani.

Dk. Magaufuli alimwuliza kaka yake Peter Wangwe ambaye ni mwanachama wa NCCR- Mageuzi kama yuko tayari kurejea CCM na ndipo alipokubali na kuwa anarudi kwasababu alichokifuata upinzani hakipo.

“Ulipoteuliwa wewe kuwa mgombea urais wa CCM nikajua hoja za wapinzani zimekwisha maana unajulikana kwa uhodari na uchapakazi wako hivyo natangaza kurudi CCM,” alisema.

Akiwahutubia wananchi wa Musoma, Dk. Magufuli alisema hataogopa lawama wala kumwonea mtu haya wakati wa kuwashughulikia watumishi wazembe wanaoshindwa kuwahudumia wananchi kwa wakati.

Alisema wanaomchukia washindwe na walegee kwasababu ana uhakika Watanzania wengi wanampenda na watampa ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu.

Alitoa ahadi hiyo jana ikiwa ni siku yake ya pili ya mikutano ya kampeni katika mkoa huo akitokea Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Lushoto.

Alisema atakuwa jasiri na hatamwogopa mtu wakati wa kuwawajibisha watendaji ambao wataonekana kujali maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya wananchi walio wengi.

“Unakuta kiongozi kapewa ofisi, gari, mafuta anapewa lakini badala ya kuwatumikia wananchi anajitumikia yeye na tumbo lake, kwa serikali ya Magufuli kiongozi kama huyo akae mguu sawa kwasababu sitavumilia wazembe wa aina hiyo,” alisema.

Alisema kuna watumishi wazembe serikalini ambao wamekuwa wakifanya mambo ya ovyo ovyo na kusababisha wananchi waichukie na kuiona serikali nzima kuwa haifai hivyo alisema watu wa aina hiyo kwenye serikali yake hawatakuwa na nafasi.

“Haiwezekani tukae kimya na tuoneane aibu wakati dawa zinachelewe kufika katika vituo vya afya, zahanati au hospitali na wakati mwingine zinaozea njiani huku wananchi wanataabika, nichagueni mimi niingine Ikulu maana viongozi wa aina hiyo nitalala nao mbele,” alisema Dk. Magufuli akimaanisha kuwa atakula nao sahani moja, usemi ambao huwafanya wananchi kulipuka kwa shangwe kila anapousema.

Mgombea ubunge Jimbo la Bunda (CCM), Steven Wassira, alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amekuwa akitapatapa kwa kusingizia CCM kuwa inaandaa mazingira ya kuiba kura wakati hana uthibitisho wa anayoyasema.

Alisema maneno hayo yanaweza kuligawa taifa na kusababisha vurugu mara baada ya uchaguzi wa Oktoba hivyo aliomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kukemea viongozi wanaotoa maneno ya uchochezi kama hayo.
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

It's the same old story people!!!! Mwinyi, Mkapa na Kikwete walisema kitu hicho hicho hapo nyuma. Mara baada ya kuingia madarakani...... What heppened??? As long as huyu Magufuli yuko ndani ya ccm, hakutakuwa na lolote jipya. Hayo mapya ni story tu ya maombi ya kutaka kupata kura. Too bad for this guy na ccm yake iliyooza. ccm IMECHOKWA NA WENGI!!!! I really don't care who to vote for but am not voting for ccm this time.

Anonymous said...

Mheshimiwa JPM hii itakuwa ni maajabu kama utakiuka ilani ya chama kinachokulinda na kutetea mafisadi. Sidhani kama watakuacha ufanye hayo ndani ya chama chao. Hapo unaomba kura wamekusikia je umewaangalia maisha wanayoishi na mambo yanayotendeka ndani kwa kuwahonga elfu kumi tuuh. Asante tuko pamoja.

Anonymous said...

There are no viable alternatives; UKAWA has ceded to the worst of the CCM cadres!

The beauty of a democratic system is that one can actually vote unwisely or not at all. The downside is that once you vote unwisely you may have to live with the unpleasant consequences of your unwise vote, if the vote if the wise does not shield you. So go ahead, buddy!