“Tumeshitushwa sana na msiba huu ambao mazingira yake yana utata mkubwa na sisi kama chama hatuelewi kilichotokea lakini tuna imani kuna mipango ya watu waliohusika,” alidai Mluya. Alisema chama hicho kinaiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina, hata ikiwezekana vyombo vingine vya usalama vya kimataifa, kusaidia katika kubaini nini kilichosababisha kifo hicho.
Mluya alisema vitu vinavyofanya wasiamini mazingira ya kifo hicho ni pamoja na picha zilizopigwa na kuwekwa kwenye mtandao, mara tu baada ya tukio la ajali kutokea kuwa zinatia shaka kuwa kuna mtu alikuwa amejiandaa eneo, ambapo walipanga ajali itokee.
“Ajali ni ya kupangwa, haiwezekani picha za ajali zinaonesha kama marehemu tayari alishapatiwa huduma ya kwanza wakati waliokuwa naye wamesema wao ndio waliomhudumia na hakuna aliyempiga picha kati yao,” alihoji Mluya.
Aidha, alisema kutokana na ushujaa wa kiongozi wao, wataendeleza kazi zote ambazo Mchungaji Mtikila alikuwa akizifanya na hivyo yale ambayo alitarajia kuyatekeleza, yatatimia kama ndoto zake zilivyokuwa.
Kwa upande wake, Mchungaji Patrick Mgaya ambaye ni miongoni mwa abiria waliokuwemo ndani ya gari lililopata ajali, alisema kifo cha ajali hii kina utata mkubwa huku akieleza namna ambavyo mazingira yake yalivyokuwa.
Alisema wakati wanaendelea na mkutano wa kampeni huko Njombe, pikipiki iliyokuwa na bendera mbili za vyama tofauti vya siasa, ilikatisha mbele ya mkutano na kuondoka. Mara baada ya kuondoka, waliendelea na mkutano hadi ulipoisha, kisha wakaondoka na kwenda kupata chakula eneo jirani na walipokuwa wakifanyia mkutano, ambapo walipita wafuasi wa vyama vingine vya siasa na kuwauliza, ni muda gani wataondoka kuelekea Dar es Salaam.
“Hiki kifo mimi sikielewi hata kidogo kwasababu kinaonesha dhahiri kuna watu walipanga na kuamua kutekeleza ajali hii kwa mbinu zao wenyewe ikiwemo za kishirikina,” alidai Mgaya. Mgaya aliendelea kueleza kuwa, walipomaliza kupata chakula, waliondoka na kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam, ambapo baada ya muda mfupi, walipata ajali na kuligonga gari lililokuwa mbele yao kutokana na ukungu mkubwa, uliokuwa mbele yao na taa za gari lao zilizimika.
Mara baada ya ajali hiyo, walikwenda Kituo cha Polisi kilichokuwa jirani yake na kufanikiwa kutatua tatizo hilo, kisha kuendelea na safari yao ya kurudi jijini Dar es Salaam. Alidai walipoanza kuondoka maeneo ya Njombe, kwa nyuma waliona gari lililokuwa likiwafuata kwa nyuma ambalo lilikuwa aina ya Toyota Land Cruiser ya rangi ya kijivu, ambalo hakuweza kuzishika namba zake za usajili.
Alidai gari hilo lilikuwa linakuja kwa kasi nyuma yao hadi likawapita kwa mbele, lakini hatua chache baadaye na gari yao pia ilifanikiwa kulipita na kutangulia mbele. Mgaya alidai kuwa magari hayo mawili yaliendelea kukimbizana kwa kasi huku Mchungaji Mtikila akimwambia dereva apunguze mwendo, kwani kasi anayoendesha sio nzuri.
Mgaya alisema walipofika njiani maeneo ya Mikumi, walishuka kuchimba dawa na yeye Mgaya kumshauri Mchungaji kuwa wasubiri kama nusu saa hivi ili gari ile ambayo wana shaka nayo iweze kutangulia zaidi na wasiifikie kwa haraka au wasiikute. Baada ya muda wa nusa saa kupita, walianza safari huku wakimsihi dereva apunguze mwendo.
Alidai kuwa walipokuwa wakiendelea na safari, ghafla lile gari walilokuwa wakifukuzana nalo, waliliona likiwa nyuma yao huku likija kwa kasi kubwa na kuamua kupisha lipite, hivyo likawa mbele yao. Alisema safari liliendelea huku magari yote yakiwa kwenye mwendo wa kasi na walipofika karibu na kituo cha mafuta gari lao, lilipita na kuongeza mafuta kisha kuendelea na safari.
Walipofika mbele kidogo, waliliona hilo gari likiwafuata tena na kuamua kuongozana nalo hadi walipofika mbele na kukuta gari aina ya lori likiwa limepaki pembezoni mwa barabara. Katika kulipita hilo gari, Mgaya alidai gari lililokuwa mbele yao aina ya Land Cruiser, ambalo lilitokea awali lilikuwa mbele ndio ilipaswa kugongana na lori hilo, lakini lilifanikiwa kupita ndio dereva wao aliamua kupeleka gari porini na kuanguka.
Mgaya alidai mara baada ya ajali hiyo, alipozinduka alimuuliza dereva Mchungaji yupo wapi. Alidai Mchungaji alikandamizwa na gari kifuani na walipata msaada kutoka kwa wasamaria, kulisukuma gari lililopata ajali na kumuondoa huku akiwa tayari amefariki.
Maziko Mwili wa marehemu utaagwa leo katika viwanja vya Karimjee kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba na kisha kusafirishwa hadi kijijini kwao Milo wilayani Ludewa mkoa wa Njombe kwa ajili ya maziko siku ya leo au kesho.
Mtikila alifariki kwa ajali ya gari maeneo ya Msolwa wilayani Bagamoyo kwa ajali ya gari aina ya Toyota Corolla, lenye namba za usajili T 189 AGM, akitokea Njombe kuelekea jijini Dar es Salaam.
HABARI LEO
3 comments:
Ni aibu kwa gazeti la serikali kuandika mambo ya mitaani kuonyesha conspiracy theory ili kuaminisha watu kuwa kuna watu Fulani ambao wamehusika na hiyo ajali. Polisi wameeleza ukweli na kila mmoja anafahamu kuwa gari alilokuwamo mtikila lilikuwa linaendeshwa kwa zaidi ya Km 140 kwa saa, kwa barabara zetu huo mwendo ni wa hatari na lolote linaweza kutokea kama vile ambavyo imetokea. Hao waliokuwemo garini walishaona hiyo hatari ya ajali kwanini hawakumwambia dereva asimame washuke au wamripoti polisi huyo dereva asiye na weledi?? Pikipiki za vyama kukatisha mbele ya gari siyo sababu ya ajali hiyo bali hisia tu, Pia kama kuna gari lilikuwa linawafuata kwa nyuma kwa nini hawakusimama au kwenda polisi? Tutumie akili hata kidogo jamani,....msilete conspiracy theory hapa kwa ajili ya kukinufaisha chama tawala ili kishinde...tengenezeni level field na haki kwa kila mmoja. Kwenye nchi yetu uchawi na ushirikina umetamalaki na bado hizi media zinaongezea ili kuendelea kuwaaminisha wananchi lakini hamjui madhara yake ni nini! Hata hivyo hainishangazi nchi yetu inarudi nyuma kwa imani za kishirikina kila mahali.....Leo kutokana na ripoti ya PEW RESEARCH watanzania zaidi ya asilimia 93 wanaamini uchawi na ushirikina.........JAMANI KATIKA KARNE YA 21 BADO TUNAAMINI UJINGA UJINGA HUU? Akifa mtu tunaambiwa siyo bure kuna mkono wa mtu, akipata ajali tunaambiwa siyo bure kuna mkono wa mtu. Kwa hiyo nchi yetu na huduma hizo mbovu kupindukia za afya watu wakifa ni lazima wawe wamerogwa? ACHENI UJINGA NA KUWAPUMBAZA WANANCHI.
Well said mheshimiwa
Unaweza kutoa maoni yako ya busara na kuwashauri Watanzania wakakuelewa vizuri kwa kutumia lugha nzuri lakini ukishatukana tena hata ule ushauri wako unakuwa hauna maana.
Post a Comment