ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 7, 2015

MIKUTANO YA MWAKA YA KUNDI LA BENKI YA DUNIA NA SHIRIKA LA FEDHA LA KIMATAIFA YAANZA RASMI NCHINI LIMA LEO TAREHE 5/10/2015

Dr. Servacius Likwelile Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa serikali wa katikati akiwa pamojana Gavana wa Benki kuu ya Tanzania Prof. Benno Ndulu kushoto na Bi. Natujwa Mwamba Naibu Gavana wa Benki kuu ya Tanzaniakulia, wakiwa katika mkutano wa chombo kinachotoa mafunzo ya kusimamia mambo ya uchumi (MEFMI) nchini Peru – Lima. ( Picha na Eva Valerian, Peru – Lima).

Mikutano ya mwaka ya Bodi ya Magavana ya Shirika la fedha la Kimataifa na kundi la Benki ya Dunia kwa mwaka 2015 imeanza rasmi hapa mjini Lima –Peru na kuhudhuriwa na maelfu ya watu kutoka nchi mbalimbali Duniani ambapo kilele chake kitakuwa tarehe 12 mwezi Octoba 2015.

Bodi ya Magavana wa Shirika la Fedha la kimataifa ( Mfuko) na Bodi ya Magavana wa kundi la Benki ( Benki ) kwa kawaida hukutana mara moja kwa mwaka kujadili kazi za Taasisi ambazo ziko chini yao. Mikutano hii ya mwaka huwa inafanyika mwishoni mwa mwezi Septemba na mwanzoni mwa mwezi Octoba. Mikutano hii hufanyika mjini Washington kwa miaka miwili mfululizo na kwa mwaka wa tatu hufanyika kwa nchi mwanachama ambaye amepitishwa kutokanana na viwango vilivyowekwa.

Mikutano hii ya Bodi ya Magavana ilizinduliwa huko Savannah, Georgia, Amerika mwaka 1946 na ikaanza kufanyika mjini Washington DC mwaka huo huo.

Mikutano hii ya mwaka itaambatana pamoja na mikutano ya kimataifa ya kifedha, kamati za fedha, Kamati za maendeleo, kundi la nchi kumi, kundi la nchi ishirini na nne, na makundi mbalimbali ya nchi wanachama.

Aidha katika kuhitimisha mikutano hii, Shirika la fedha la kimataifa, kamati ya mambo ya fedha, Kamati ya maendeleo pamoja na makundi mengine watapata nafasi ya kuwasiliana na kutoa mapendekezo yao ya kipi kifanyike ili kuhakikisha mambo wanayojipangia yanatekelezwa.

Magavana watakitumia kipindi hiki kwa kuzungumzia masuala ya kibiashara na

kushauriana. Bodi ya Magavana inatumia kipindi hiki kufanya maamuzi ya ni vipi mambo ya Fedha ya kimataifa yanapaswa kuwa na kukubaliana kuhusu maazimio yao.

Mikutano ya mwaka inakuwa na mwenyekiti ambaye ni Gavana wa Benki na wa Mfuko, na uenyekiti huo unakuwa ni wa kupokezana kati ya wanachama kila mwaka. Kila baada ya miaka miwili inachagua Mkurugenzi mtendaji. Kila mwaka wanachama wapya wowote wanakaribishwa katika Benki na mfuko.

Kwa sababu Mikutano hii ya mwaka inakusanya idadi kubwa ya wanachama kutoka

nchi mbalimbali, Shirika la fedha la kimataifa na kundi la Benki ya Dunia inatoa nafasi ya kuwapatia ushauri mkubwa na mdogo, kwa mpangilio wa kuwa na utaratibu maalumu au kutokuwa na utaratibu maalumu alimradi hawavurugi mpangilio uliopo.

Semina mbali mbali zinafanyika na zinaendeshwa na wafanyakazi wanachama kwa waandishi wa habari. Aidha programu za Mikutano ya mwaka zimetengenezwa kwa kuzingatia matakwa ya sekta binafsi, wajumbe kutoka Serikalini na maafisa wakuu wa Mabenki na watumishi wa Mfuko.


Mikutano ya mwaka iliyofanyika nje ya Amerika kuanzia mwaka 1947 hadi 2015.


Mwaka Mahali

1947 London

1950 Paris

1952 Mexico City

1955 Istanbul

1958 New Delhi

1961 Vienna

1964 Tokyo

1967 Rio de Janeiro

1970 Copenhagen

1973 Nairobi

1976 Manila

1979 Belgrade

1982 Toronto

1985 Seoul

1988 Berlin

1991 Bangkok

1994 Madrid

1997 Hong Kong

2000 Prague

2003 Dubai

2006 Singapore

2009 Istanbul

2012 Tokyo

2015 Lima


Magavana wa mikutano hiyo ni Mawaziri wa fedha kutoka nchi mbalimbali, Magavana wa Benki kuu na Makatibu wakuu wa Wizara za fedha.

Mpaka sasa karibu nchi zote zimeshawasili katika mikutano hiyo na hali ya hewa ni mawingu na baridi kiasi.

Imetolewa na:
Ingiahedi Mduma
Msemaji Mkuu
Wizara ya Fedha
Lima - Peru
5/10/2015


No comments: