Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), amewasilisha kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akipinga uamuzi uliompa dhamana mwanafunzi wa Chuo cha Taasisi ya Teknolojia Tanzania (DIT), Benedict Ngonyani.
Ngonyani anakabiliwa na kesi ya kusambaza taarifa katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange amelishwa sumu.
Wakili wa Serikali, Theophil Mutakyawa aliwasilisha jana kusudio hilo la kupinga uamuzi uliotolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Respicius Mwijage wa kumpa dhamana Ngonyani licha ya kuwapo kwa hati ya DPP ya kuizuia dhamana hiyo.
Katika kusudio hilo, DPP anadai kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kutengua hati hiyo ya zuio la dhamana na kwamba mwenye mamlaka hayo ni yeye mwenyewe au kesi inapokwisha.
Novemba 13, Hakimu Mwijage alitengua hati ya DPP ya kuzuia dhamana ya Ngonyani iliyowasilishwa mahakamani hapo kutokana na kutokuwapo kwa sababu za msingi.
Alisema hakuna upande wa mashtaka wala mtuhumiwa ulioeleza kama mtu anayedaiwa kupewa sumu kuwa ni Mwamunyange ambaye ameonekana hadharani.
Pia, alisema mshtakiwa ni mwanafunzi na shtaka analoshtakiwa nalo linadhaminika hivyo haoni haja ya kukosa masomo.
Hakimu Mwijage alisema si kila shtaka linawekewa zuio akisema upelelezi umeshakamilika hivyo haoni haja ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa.
Ngonyani anatakiwa kuwa nje kwa kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika ambao kila mmoja wao atasaini hati ya Sh5 milioni.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Septemba 25 alisambaza taarifa za uongo kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Ngonyani anadaiwa siku hiyo alisambaza taarifa kuwa Mwamunyange amelishwa sumu huku akijua taarifa hizo ni za uongo na zilikuwa na lengo la kupotosha umma. Baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka hilo alikana kuhusika.
No comments:
Post a Comment