
Dar es Salaam. Oparesheni ya bomoabomoa imeendelea kutikisa jijini Dar es Salaam huku ikiacha vilio na simanzi kwa wamiliki wa nyumba, likiwamo ghorofa mali ya mfanyabiashara lililojengwa kwa Sh500 milioni miaka 20 iliyopita.
Bomoabomoa hiyo iliyodumu kwa siku tatu mfululizo katika Manispaa ya Kinondoni, inahusisha ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kwenye viwanja vilivyodhulumiwa, maeneo ya wazi na hifadhi za barabara.
Wakati wamiliki na ndugu wakilia na kuhangaika kuokoa mali zao katika oparesheni hiyo , baadhi ya vijana walionekana wakifurahia huku wakitumia kauli iliyoanzishwa na Rais John Magufuli ya ‘Hapa ni Kazi Tu’.
Mhandisi wa Manispaa hiyo anayesimamia bomoabomoa hiyo, Baraka Mkuya alisisitiza kuwa wataendelea kubomoa nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria kila mwezi.
“Kila anayejifahamu amejenga nyumba kwenye kiwanja kisicho chake, eneo la wazi, kwenye hifadhi ya barabara au lolote lililozuiwa kisheria aondoke kabla hajaondolewa kwa nguvu,” alisema Mkuya.
Mtaa wa Liberman, Mbezi Beach
Katika mtaa huo uliopo eneo la Mbezi Beach, simanzi ilitawala baada ya ghorofa hilo linalomilikiwa na mfanyabiashara huyo, Deosdedit Sisiwe kubomolewa kwa kujengwa kwenye kiwanja kinachomilikiwa na Protas Bilauri.
Mke wa mfanyabiashara huyo, Catherine Sisiwe alidai kushangazwa na hatua hiyo, akisema hana taarifa za nyumba yao kubomolewa.
“Tafadhali naomba tumsubiri mzee aje ndipo mbomoe kwa sababu ameenda mahakamani kufuatilia kesi hii,” alisema Catherine na kuongeza;
“Usiombe likukute jamani, nilidhani utani kumbe kweli wanabomoa nyumba yangu bila huruma, ehee Mungu nisaidie”.
Pamoja na kujitetea, Mhandisi Mkuya aliamuru vyombo kuondolewa kwenye nyumba hiyo kwa dakika 45 ili kupisha bomoabomoa hiyo.
“Hatujaja kusikiliza mashauri, kazi yetu ni kubomoa kama tulivyoagiwa na wizara. Tulishatoa taarifa siku tatu kabla tukiwataka muhamishe vyombo ili kupisha kazi hii, lakini kwa kuwa mlikaidi nawapa dakika 45 muhamishe kila kitu,”alisisitiza.
Alisema nyumba hiyo ilijengwa kwenye kiwanja cha mtu mwingine kinyume cha sheria na kwamba mmiliki halali alishinda kesi mahakamani baada ya kufungua kesi ya kuporwa kiwanja chake.
Alifafanua kuwa nyumba hiyo iliyojengwa zaidi ya miaka 20, iliyopita kwa gharama ya zaidi ya Sh 500milioni na kumtaka Catherine kutoa vielelezo vinavyoonyesha nyumba imejengwa kwenye kiwanja wanachomiliki kihalali, lakini alishindwa kufanya hivyo.
Miongoni mwa mali zilizookolewa kwenye ghoroga hilo ni bunduki aina ya Rife ambayo iliwekwa chini ya uangalizi wa polisi kwa uchunguzi zaidi ili kubaini kama inamilikiwa kihalali. “Tukijua inamilikiwa kihalali basi mwenye nayo atarejeshewa na kama vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema mkuu wa kikosi cha polisi kwenye oparesheni hiyo, aliyefahamika kwa jina moja la Joseph.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment