Monday, November 23, 2015

Kili Stars moto mkali

TIMU ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, jana ilianza vizuri michuano ya Kombe la Chalenji baada ya kuitandika Somalia kwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Matokeo hayo yanaifanya Kili Stars inayofundishwa na kocha mkongwe Abdallah Kibaden, ishike uongozi wa Kundi A ikiwashusha Rwanda waliowafunga wenyeji Ethiopia 1-0 katika ufunguzi wa michuano hiyo juzi.

Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ alipachika mawili katika ushindi huo, huku moja akifunga kwa penalti katika dakika ya 12 baada ya beki wa kulia, Shomari Kapombe kuangushwa na jingine alitupia katika dakika ya 54.

Mshambuliaji mwenzake Elias Maguli naye akafunga mabao mawili dakika ya 17 na 66 kukamilisha kipigo hicho cha uhakika ambacho kinatoa onyo kwa timu zingine za kundi hilo. Kipa Aishi Manula aliyeanza jana alifanya kazi nzuri ya kuokoa michomo mingi ya hatari langoni mwake na kujizolea sifa kibao.

Timu zingine zilizopo katika kundi hilo ni pamoja na Rwanda na wenyeji Ethiopia. Kilimanjaro Stars itashuka dimbani Awassa kumenyana na wakali Rwanda katika mchezo utakaonesha mwelekeo halisi wa Kili Stars.

Timu mbili za kwanza kutoka kila kundi na zile mbili zilizomaliza klatika nafasi ya tatu, zitafuzu kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano hayo. Wakati huohuo, Uganda jana walianza vibaya michuano ya Chalenji baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa wapinzani wao Kenya katika mchezo uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Mabao ya Kenya yalifungwa na Jacob Kheli na mchezaji aliyeingia kipindi cha pili, Michael Olunga katika dakika ya 29 na 50. Nahodha wa Uganda Cranes, Farouk Miya alipiga shuti lililogonga mwamba katika kipindi cha kwanza. Uganda itarejea tena uwanjani Jumanne kusaka pointi tatu muhimu baada ya jana kufungwa.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake