Ibara ya 51 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu nafasi ya Waziri Mkuu inasema, “Kutakuwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano atakayeteuliwa na Rais kwa kufuata masharti ya ibara hii na ambaye kabla ya kushika madaraka yake ataapa mbele ya Rais kwa kiapo kinachohusika na kiti cha Waziri Mkuu kitakachowekwa na Bunge.
Kifungu cha (2) cha ibara hiyo kinasema, “Mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku kumi na nne, baada ya kushika madaraka yake, Rais atamteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika Jimbo la Uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi, anayeelekea kuungwa mkono na wabunge waliowengi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, naye hatashika madaraka hayo mpaka kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za Wabunge walio wengi.”
Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano; atakuwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, na kusimamia utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe.
Kwa kuzingatia ibara hiyo, Rais John Magufuli anatarajiwa kesho kuwasilisha bungeni jina la mbunge anayempendekeza awe Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano ili apitishwe na wabunge kabla ya kuapishwa rasmi.
Tangu Dk Magufuli aingie madarakani watu wamekuwa wakibashiri majina ya wabunge mbalimbali ambao wanaoonekana wanafaa kuteuliwa kwa nafasi hiyo.
Hata katika viunga vya Bunge lililoanza kazi jana, wabunge mbalimbali waliozungumza na Mwananchi kwa masharti ya kutotajwa gazetini wameeleza kuwa bado suala hilo ni siri kubwa, hivyo hakuna haja ya kujisumbua kulitafuta jina kwani wanasubiri hadi litajwe bungeni.
Mmoja wa wabunge hao alisema kuwa huenda waziri mkuu akatoka kati ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini au mikoa ya Kusini.
Mwingine alisema suala la nani atakuwa waziri mkuu ni la kusubiri hadi Alhamisi Rais atakapoliwasilisha jina kwa kuwa hakuna mtu anayelifahamu zaidi ya Rais na wasaidizi wake.
Hata hivyo baadhi ya wabunge walisema kuwa majina ambayo yamekuwa yakitajwatajwa kuingia kwenye nafasi hiyo hayana nafasi kwa kuwa Rais mwenyewe amekuwa msiri na mwenye msimamo.
Kwenye mitandao mbalimbali wamekuwa wakitajwa wabunge wanaofikiriwa kushika nafasi hiyo kutokana na kanda wanazotoka mjadala ambao utaisha kesho kwa kujua nani ni waziri mkuu.
Miongoni mwa wabunge wanaotabiriwa wanaweza kupata uteuzi wa Dk Magufuli kuchukua nafasi hiyo ni Dk Harrison Mwakyembe (Kyela), January Makamba (Bumbuli), William Lukuvi (Isimani), Profesa Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini) na Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi).
Makada hao wamekuwa wakitajwa kuwa wanaweza kuwa chaguo la Rais Magufuli kwani mbali na kuwa na rekodi nzuri ya uchapakazi wana sifa zinazowapa wigo mpana wa mmoja wao kuwa Waziri Mkuu atakayekuwa msimamizi wa mkuu wa shughuli zake.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akizungumzia matarajio yake kwa waziri mkuu mpya alisema wao kama wabunge wanahitaji mtu atakayeweza kusimamia shughuli za Serikali bungeni na kusimamia utekelezaji wake. “Wabunge hawahitaji mtu picha bali mtu anayefaa katika utendaji,” alisisitiza Lissu.
Mbali ya wabunge, watu mbalimbali wana shauku ya kufahamu ni nani atakayepewa nafasi hiyo nyeti na kuitumikia kwa uadilifu, weledi na juhudi kwa miaka mitano ijayo. Kama ilivyo ada, wengi wameendelea kutabiri baadhi ya makada ambao wana sifa ya uchapakazi kama Dk Magufuli, ambayo inakwenda sambamba na kauli mbiu ya Rais huyo wa Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu.’
Inawawia vigumu wabunge kufahamu ni nani kati ya walioshinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 25 atakayerithi mikoba ya Mtoto wa Mkulima, Mizengo Pinda kwani Dk Magufuli siyo mtu wa kutabirika katika uamuzi wake.
Maoni ya wasomi
Baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema kwamba ni dhahiri kuwa Dk Magufuli ambaye katika siku za mwanzo za utendaji kazi wake ameonyesha makeke hakuna shaka kuwa mbunge goigoi hatapewa nafasi kwa sababu yeye (Rais) anaamini katika uchapakazi.
Wamesema hawatarajii kuona Dk Magufuli ambaye hana historia ya ‘kubeba’ watu akimchagua waziri atakayeshusha ari yake ya kuleta mabadiliko ya kiutendaji serikalini na kurejesha matumaini ya Watanzania kwa chama chake.
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Tolly Mbwete wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) alisema, “Tunatarajia Waziri Mkuu atakayechaguliwa awe mchapakazi kweli kweli, asiyechoka kufualitia mambo, siyo kuupuza.”
Profesa Mbwette aliongeza kuwa Waziri Mkuu mtarajiwa lazima awe na uelewa mpana wa masuala mbalimbali na uhusiano mzuri wa kimataifa. “Lakini ukiachilia mbali sifa ya uchapakazi kiongozi huyo anatakiwa kuwa ya uadilifu na uzoefu serikalini,” alisema.
Pia, alisema uwezo wa kuifahamu vizuri Serikali na maeneo mengi nchini utamsaidia kusimamia kikamilifu wizara mbalimbali ikiwamo ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), idara na wakala zote za Serikali zilizo chini yake ambazo baadhi yake hazikufanya vizuri chini ya Serikali iliyopita.
Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema, “Hatutarajii mtu mpya kwa sababu Waziri Mkuu lazima afahamu namna Serikali inavyoendesha shughuli zake.”
Dk Bana alisema mrithi wa mikoba ya Pinda lazima awe mchapakazi ili aendane na falsafa ya Rais Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’ na awe mwadilifu pia.
“Hata yeye (Rais Magufuli) alichaguliwa kuwania nafasi ya urais kwa sababu rekodi yake ni safi ambayo alitoa hamasa kwa wananchi pia. Lazima kiongozi atakayemchagua afanane naye,”alisema.
“Tukirudi nyuma, itakumbukwa kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ilipata dosari baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond iliyogharimu Serikali mabilioni ya fedha.”
Pia, Dk Bana alisema anatarajia Rais Magufuli afanye uteuzi wa mtu ambaye amewahi kufanya kazi pamoja kwani atakuwa anaelewana kuliko mtu tofauti.
Richard Mbunda ambaye ni mhadhiri wa UDSM, alitoa sifa nyingine ambayo anategemea kutoka kwa Waziri Mkuu ajaye, akisema anatakiwa awe kiongozi mwenye busara.
“Atumie busara hizo katika kufanya maamuzi na kuhakikisha mambo yanaenda vizuri,” alisema Mbunda.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment