By Florence Majani, Mwananchi
Dar es Salaam. Kasi ya utendaji kazi aliyoanza nayo Rais John Magufuli katika muda wa siku 20 inaonekana kubwa na ya aina yake lakini hivyo ndivyo ilikuwa kwa mtangulizi wake, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, miaka 10 iliyopita.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba katika muda wa siku 20, tangu alipoapishwa Novemba 5, Rais Magufuli amekonga nyoyo za Watanzania baada ya kufanya ziara za kushtukiza Wizara ya Fedha na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akavunja Bodi ya Wakurugenzi ya Muhimbili na kuzuia fedha kutumika kwa ajili ya sherehe badala yake akaagiza zifanye shughuli za jamii.
Rekodi zinaonyesha kuwa Kikwete, katika siku zake 20 tangu alipoapishwa Desemba 21, 2005 alifanya mambo kadhaa makubwa likiwamo la kuunda Baraza la Mawaziri. Pia, katika kipindi hicho Kikwete aliteua Tume ya Jaji Musa Kipenka kufanya uchunguzi wa mkasa wa kutekwa na hatimaye kuuawa kwa wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi mmoja wa jijini Dar es Salaam katika msitu wa Mabwepande.
Magufuli vs Kikwete
-----> Kuapishwa
Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza Dk Magufuli kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 kwa asilimia 58.46, Novemba 5 aliapishwa rasmi na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande katika sherehe zilizofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kimataifa.
Kwa upande wake Jakaya Kikwete, baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 14, 2005 kwa asilimia 80 aliapishwa Desemba 21 na Jaji Mkuu, Barnabas Samatta ili kuanza ngwe ya kwanza ya urais. Mwaka 2010 Kikwete aliapishwa na Jaji Mkuu, Augutino Ramadhani.
------>Uteuzi
Kazi ya kwanza aliyoifanya Dk Magufuli saa chache baada ya kuapishwa ilikuwa kumteua George Masaju kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilhali Kikwete alimteua Johnson Mwanyika kuwa Mwanasheria Mkuu Desemba 24 yaani siku tatu baadaye.
------>Ziara wizarani
Hata kabla hajaunda Baraza la Mawaziri, Magufuli amefanya ziara mbili kubwa. Novemba 6 ikiwa ni siku moja baada ya kuapishwa alitembea kwa miguu kutoka Ikulu hadi Wizara ya Fedha ambako alipita kwa kushtukiza ofisi moja baada ya nyingine na baadaye alifanya kikao na watendaji.
Novemba 9 alifanya ziara nyingine ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alivunja Bodi ya Wakurugenzi, alimwondoa Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Hussein Kidanto na kuamuru mashine muhimu za vipimo za CT-Scan na MRI kutengenezwa haraka.
Kikwete kwa upande wake alisubiri hadi baada ya kuunda Baraza la Mawaziri ndipo akaanza kutembelea wizara na kuwapa maelekezo maalum. Januari 17 alitembelea Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na kuanika uozo katika wizara hiyo kisha kuamuru wahusika wa rushwa na urasimu wafukuzwe kazi na alimwagiza Magufuli aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, kuwafagia walaji wote katika wizara hiyo.
Halafu alitembelea Wizara ya Elimu ya Ufundi ambako aliagiza mitaala ya zamani irejeshwe, kisha akatembelea Wizara ya Miundombinu.
------->Kuteua wabunge
Novemba 16, Magufuli alimteua Dk Tulia Ackson na hivyo kuwa mteule wa kwanza katika nafasi ya ubunge hali iliyotumiwa na chama chake CCM kumpendekeza agombee nafasi ya Naibu Spika wa Bunge la 11 na akashinda. Kabla ya uteuzi huo, Dk Tulia alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika siku 20 za kwanza, moja ya kazi kubwa alizofanya Kikwete ilikuwa kusuka Baraza la Mawaziri. Alitangaza baraza lake lenye mawaziri 60 Januari 4, 2006 na siyo Januari 6 kama ilivyokuwa imetangazwa awali.
------->Waziri Mkuu
Novemba 19, Dk Magufuli amteua Mbunge wa Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati Kikwete alifanya uteuzi wa Edward Lowassa kuwa Waziri Mkuu Desemba 29, 2005.
------>Ahutubia Bunge
Novemba 20 Dk Magufuli alifanya mambo mawili mjini Dodoma; kwanza, asubuhi katika ikulu ndogo ya Chamwino alimuapisha Majaliwa kuwa Waziri Mkuu, na pili jioni, alilihutubia Bunge. Pamoja na uzuri wa hotuba yake alisusiwa na wabunge wa upinzani waliokuwa wanapinga Rais Magufuli kuingia bungeni Dk Ali Mohamed Shein kwa madai si rais halali wa Zanzibar.
Desemba 30, 2005 Kikwete alifanya kazi mbili; kwanza, asubuhi alimuapisha Lowassa kuwa Waziri Mkuu, na pili jioni alilihutubia Bunge. Hotuba yake ilipokewa kwa shangwe kwa vile alisisitiza kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, kuwapa ajira vijana na utayari wake kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Hotuba za viongozi hao kwa kiasi kikubwa zilionyesha utayari wa kuwahudumia wananchi bila kujali itikadi za vyama, kupiga vita ufisadi, kupambana na majangili na wauzaji dawa za kulevya na kwamba lengo ni kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kimaendeleo.
------->Tofauti zao
Dk Magufuli ameonyesha utofauti kivitendo na mtangulizi wake baada ya kufuta safari za nje, lakini Novemba 20 aliagiza kiasi cha Sh 225 milioni zilizokusanywa kwa ajili ya hafla ya wabunge, zipunguzwe ili zitumike kununua vitanda kwa ajili ya wagonjwa Muhimbili. Ofisi ya Spika wa Bunge ilisema kuwa kiasi cha Sh25 milioni tu kilibakizwa kwa ajili ya hafla hiyo kwa watu wasiozidi 5000.
------>Afuta sherehe
Ukiwa ni msisitizo wa kupunguza matumizi ya fedha, kwa mara ya kwanza hakutakuwa na maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru, Desemba 9, badala yake siku hiyo itatumika kufanya usafi nchi nzima. Tangazo hilo la kufuta sherehe lilitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue Novemba 23 kwamba ufanyike usafi kukabiliana na tishio la kusambaa ugonjwa wa kipindupindu
------->Tume ya Uchunguzi
Moja ya hatua alizochukua na kumpa sifa Kikwete katika siku za mwanzo Ikulu ni kundwa kwa Tume Maalum iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Musa Kipenka iliyopewa kazi ya kuchunguza chanzo cha vifo na waliohusika na mauaji ya waliokuwa wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge wilayani Ulanga, Morogoro na dereva teksi mmoja wa Dar es Salaam. Tume hiyo iliundwa Januari 23 na ilipewa siku 21 kukamilisha kazi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake