Burule akizungumza na Nipashe jana katika wodi aliyolazwa ya Hospitali ya Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, alisema hakutegemea kama ipo siku angeweza kuuona tena mwanga wa dunia akiwa hai baada kufukiwa ndani ya mgodi.
Mchimbaji huyo pamoja na wenzake wanne waliokolewa kutoka katika kifusi cha machimbo ya madini ya Nyangarata, wilayani Kahama juzi baada ya kuangukiwa na kufukiwa na kifusi Oktoba 6, mwaka huu, saa 5 asubuhi baada ya udongo kuporomoka.
Alisema bila maombi waliyofanya kwa Mungu na wenzake, hawaamini kama wangekuwa hai mpaka sasa.
Hata hivyo, alisema baada ya kuokolewa na kupata matibabu katika hospitali hiyo, afya yake inazidi kuimarika tofauti na walivyofikishwa hospitalini hapo juzi.
Naye mchimbaji mwingine aliyenusurika kifo katika tukio hilo, Msafiri Gerald (38), aliyelazwa katika wodi namba 2 hospitalini hapo, alisema kwa sasa amepata nafuu na kuanza kutembea mwenyewe pamoja na kuwatambua watu vizuri.
“Kwa siku ambazo nilikuwa shimoni katika kiza kinene, macho yalipoteza uasili wake wa kuona, sikutegemea kuwaona tena ndugu na jamaa pamoja na mwanga, tulikata tamaa ya kuishi lakini sasa tunasema Mungu mkubwa,” alisema. Gerald alisema kwa siku zote walizokaa shimoni, chakula chao kikubwa kilikuwa wadudu kama mende, mizizi ya mimea, udongo pamoja na nguo zao, hali iliyowafanya kupoteza matumaini ya kuishi.
Alisema anawashukuru wachimbaji wa mgodi wa Nyangarata kwa kufanya kazi kubwa ya kuwafukua ardhini kwa siku 41 na kuokoa maisha yao.
Wachimbaji hao watano baada ya kuokolewa walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama wakiwa hawatembei wala kuongea, lakini kwa sasa wameanza kupata nguvu ya kutembea na kuzungumza na watu wanaoenda kuwajulia hali hospitalini hapo.
Akizungumzia hali za wachimbaji hao, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Jibai Mukama, alisema walipofikishwa hospitalini hapo juzi walikuwa wamedhoofika sana na walikuwa hawana nguvu kutokana na kutokula chakula kwa muda mrefu na kukosa hewa safi na kutumia hewa ndogo kutoka katika nyufa za mashimo hayo.
Dk. Mukama alisema hali waliyokuwa nayo wachimbaji hao ilikuwa ya kukatisha tamaa, lakini hivi sasa wanaendelea vyema baada ya kupata matibabu na kupewa chakula laini.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Haji Kusalawe, alitoa wito kwa serikali kuhakikisha wachimbaji hao wanasaidiwa na kupatiwa huduma nzuri za afya ili waweze kurejea katika hali yao ya kawaida na kufanya kazi zao za kutafuta riziki, kwani familia zao zilishakata tamaa ya kuwaona tena.
Aidha, alishauri umoja wa wachimbaji madini katika mgodi huo kuangalia namna ya kuwasaidia wenzao ili waweze kuwa na uwezo wa kuendesha maisha yao ya kila siku kabla ya kuimarika kwa uchumi wao.
Watu watano kati ya sita waliofukiwa na kifusi hicho waliokolewa, huku mmoja kati yao, Mussa Supana, akifariki dunia.
Ukiacha Burule na Gerald, wengine waliookolewa ni Onyiwa Kanyimbo (55), Amosi Muhangwa (25) na Chacha Wambura (53).
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment