Thursday, November 26, 2015

TUONYESHE YAKO MISULI

By Mohamed Matope

Raisi ni Magufuli, onyesha yako misuli,
Hongera wastahili, taifa halina shari,
Tumekuchagua heri, Raisi usofedhuli
"Hapa kazi tu" iwe kampeni kweli.

Tinga tinga mtamboni,shuhudie ujasiri.
Jina lako asili,kisukuma na Kiswahili.
Litumie kwamakini,vile linavyostahili
John Pombe Magufuli, hakuna wa kusaili.

Usiwe mlevi pombe, lakini shika kufuli.
Ambalo uzitumie, mafisadi kuhimili.
Ahadi utekeleze, muda umeshawasili.
Kufungua mahakama, kuhukumu mafedhuli.

Zulu hospitalini, Bugando na Muhimbili.
Fichua manesi, pamoja na madaktari. 
Nafuu haipatikani, tiba isiyo sahihi .
Tiba haipatikani, mpaka wapewe mali.

Mfagio utumie, serikali ishamiri,
Wazembe uwafagie, na wasioficha siri,
Ofisi zao vijiwe, kama hawana mwajiri,
Mishahara kuchukua, bila kugusa faili.

Uwe pia makini, unapochagua waziri
Uzingatie utendaji, hapana rudisha fadhiri
Uangalie maadili,wananchi watujali
Watuliao nyumbani,si ughaibuni kusafiri

Vamia idara mbili, za kodi na Bandari
Ujionee dhahili,walarushwa mashuhuri 
Wale wenye magari, na majumba ya fahari 
Uwaweke kizimbani, kama Mramba Basili

Twaomba tuondolee, misururu ya magari,
Barabara uzikuze, reli pia nashauri,
Majengo uyahamishe,yaenee miji mbali
Watumishi wapungue, usafiri uwe shwari,

Biashara ndogo sapoti, na ajira za binafsi
Watumie wetu wasomi, nchini tuwahimili,
Dumisha kilimo madini,uvuvi na utalii.
Utumie gasi mali, kwa shule na hospitali

Tusafishie mazingira ili tuishi vizuri
Himiza miti panda, nchi isiwe Kalahari
Mazingira elimisha, kwenye yetu maskuli 
Nchi iwe waridi, kama wenzetu Kigali.

Tamati ndugu raisi,washika hii shughuli
Elfu mbili na ishirini,sisi tutakujadili
Tutakupatia repoti ,kama unayostahili
Hapana usisubiri kuonyesha YAKO MISULI

            

3 comments:

  1. Nice! Yes Onyesha Misuli yako Mhe.Raisi. Kwa sababu za uongozi wako naamka nikitamani kusoma magazeti.BIG UP MR. PRESIDENT

    ReplyDelete
  2. Well done!, Mr. President we all Tanzanians appreciate for what you're doing for our country Keep it up!! & God bless you!

    ReplyDelete
  3. misuli wani mwana riadha mwana masumbwii.its too early to judge tovute time tutakuja kuona hiyo misuli yake isije ikawa nguvu ya soda kwanza uraisi alishinda kweli?

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake