ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 3, 2015

Vijana CUF wahimiza utulivu utawale Zanzibar

Vijana CUF wahimiza utulivu utawale Zanzibar
CHAMA cha Wananchi (CUF) kupitia Umoja wao wa Vijana (JUVICUF), kimewataka vijana wawe watulivu, wasikilize viongozi wao na juhudi wanazofanya kupatia ufumbuzi tatizo la kisiasa Zanzibar.

Wakati vijana hao wakitoa mwito wa utulivu, wadau wakiwemo viongozi wakuu wa vyama vya siasa nchini, wameeleza imani yao kwa Rais Jakaya Kikwete, kutatua mgogoro huo na kuirudisha Zanzibar katika hali ya kawaida.

Aidha, wengine wamemtaka Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kupunguza jazba na ukali, badala yake asubiri uchaguzi urudiwe, haki itendeke kwa anayestahili, arejeshe amani ya Zanzibar.

JUVICUF na utulivu

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mbatia alisema Rais Jakaya Kikwete ndiye mwenye mamlaka ya kuwakutanisha wanasiasa hao wa Zanzibar, kwa kuwa ndiye anayeongoza dola Tanzania.

Katibu Mtendaji wa Juvicuf, Mahmoud Mahinda alitoa mwito huo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya CUF, Vuga, jana, kuzungumzia hali ya kisiasa visiwani hapa.

Alisema hali ya kisiasa iliyojitokeza kutokana na kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, inashughulikiwa na taasisi pamoja na viongozi kwa njia ya kidiplomasia.

“Umoja wa Vijana wa Chama cha Wananchi (Juvicuf) unawataka vijana wote kuwa watulivu na kamwe wasikubali kuchokozeka wakati suala la kufutwa kwa uchaguzi mkuu likishughulikiwa na taasisi husika,” alisema.

Alisema vurugu za kisiasa haziwezi kuleta ufumbuzi wa matatizo ya Zanzibar kwa njia ya amani.

Alisisitiza, madhara ya vurugu ni maafa kwa wananchi hususani watoto na wanawake. Mahinda alieleza namna umoja huo ulivyosikitishwa na hatua ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (NEC) kufuta Uchaguzi Mkuu. Alisema uamuzi haukufanyiwa tathmini na taasisi hiyo ambayo ndiyo yenye jukumu na dhamana ya kusimamia uchaguzi.

Awali, polisi ilieleza ilivyoimarisha ulinzi katika Mji wa Zanzibar na sehemu za vijijini kutokana na kuwepo kwa taarifa za maandamano ya vijana wa CUF. Polisi katika taarifa yake, iliwataka wananchi, hususani vijana kutojiingiza na kushiriki katika maandamano yasiyo na kibali.

Washutumu jazba, hasira

Katika hatua nyingine, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, walimtaka Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad kupunguza jazba na ukali, asubiri uchaguzi urudiwe ili haki itendeke kwa anayestahili, arejeshe amani ya Zanzibar.

“ Pia Rais (Mohamed) Shein anatakiwa kulinda amani ili watu waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo,” alisema.

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wakulima Tanzania (AFP), Said Soud Said, pamoja na kutoa mwito huo kwa Hamad, pia alishauri iundwe serikali ya mpito visiwani Zanzibar, kurejesha imani na amani kwa Wazanzibari.

Alisema ni vyema ikaundwa serikali ya mpito itakayodumu miezi 18. Alishauri ijumuishe wadau mbalimbali wa siasa na itumike kuunda tume mpya ya uchaguzi itakayosimamia uchaguzi na kurejesha imani kwa wananchi.

“Nashauri iundwe serikali ya mpito na isiwe ya CCM na CUF pekee, bali iwashirikishe wadau wote, kwa kufanya hivyo imani ya wananchi itarejea. Serikali hiyo pia isimamie uundwaji wa tume huru itakayosimamia na uchaguzi ujao ili kuufanya uwe huru na haki,” alisema.

Imani kwa Kikwete

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Tadea, Juma Ali Khatib alimuomba Rais Jakaya Kikwete kushughulikia mgogoro huo kuinusuru Zanzibar “Kwa kipindi chote amefanya juhudi kubwa ya kufikia maridhiano yaliyowezesha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo iliifanya Zanzibar kuwa tulivu katika kipindi chote cha miaka mitano. Kama alivyosema alipokuwa akihutubia Bunge kuwa suala la Zanzibar linamnyima usingizi, basi alishughulikie hili kwa nguvu zake zote,” alisema.

Alisema hakuna haja ya wadau wa maendele,o kuingilia suala hilo kwa kuwa Rais Kikwete ana uwezo na busara za kulimaliza ikizingatiwa alishafanya kazi hiyo awali.

“Hakuna haja ya mtu mwingine kuingilia suala hili, Rais Kikwete ana busara sana, tunaamini ataweza kulitatua kwa falsafa na busara aliyoitumia kipindi kile cha kuwapatanisha Maalim Seif na Amani Karume. Kitendo cha hawa wenzetu kuleta maneno mengi kitavuruga zaidi mambo,” alisema Khatib.

Alisema, upo uzembe uliofanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) katika kusimamia uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu, hivyo kusababisha kutokuwa wa huru na haki. Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, alitaka katiba ifuatwe katika kutatua mgogoro wa Zanzibar.

Alisisitiza haja ya kupitia kwa makini hoja zilizotolewa na ZEC kupata ufumbuzi wa kudumu. Tamko la NCCR-Mageuzi Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema mgogoro wa Zanzibar utatuliwe kwa maridhiano ya kisiasa kati ya Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed Shein na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Sharif Hamad.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mbatia alisema Rais Jakaya Kikwete ndiye mwenye mamlaka ya kuwakutanisha wanasiasa hao wa Zanzibar, kwa kuwa ndiye anayeongoza dola Tanzania.

“Kule Zanzibar kuna serikali tu hawana dola, mwenye dola ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, huyu ndiye mwenye majeshi yote na huyu ndiye anaweza kusaidia kutatua mgogoro wa Zanzibar kwa kuwakutanisha Maalim Seif na Dk Shein,” alisema Mbatia.

Mbatia alisema kwa kuwa Rais Kikwete aliwaahidi Watanzania wakati anaingia madarakani kuwa lengo lake ni kumaliza mpasuko wa Zanzibar, si vizuri akaondoka madarakani na kuuacha tena visiwani humo.

“Meza ya mazungumzo ndio suluhisho la amani duniani kote na ndiyo utaratibu wa dunia, wanasiasa ndiyo wanatakiwa kukaa pamoja kumaliza mgogoro wa Zanzibar na si vinginevyo,” alisema Mbatia.

Mbatia alisema hata serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar ilitokana na maridhiano ya kisiasa kati ya Rais Amani Abeid Karume na Maalim Seif hatimaye, amani ikarejea visiwani humo. Alitoa mfano mwingine kuwa muungano wa Zanzibar na Tanganyika, ulitokana na maridhiano kati ya Abeid Amaan Karume na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Uchaguzi wa Zanzibar ambao ulifanyika Oktoba 25, ulitangazwa kufutwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha kwa maelezo kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa Sheria na taratibu za uchaguzi.

Habari hizi zimeandikwa na Khatib Suleiman, Zanzibar, Shadrack Sagati na Anastazia Anyimike, Dar.

HABARI LEO

No comments: