Picha hii ya mvulana
anayeonekana kujiuliza maswali si haba akilini mwake akiwa na Mzungu
imesambazwa mara nyingi sana mtandaoni.
Wengi wamekuwa wakiitumia kukejeli vyombo vya habari, mataifa na
mashirika ya kutoa misaada kutoka Magharibi kwa mtazamo wao kuhusu Afrika.
Kunao wanaoitumia hata hivyo kuuliza maswali ya kijumla tu.
Lakini je, wajua picha hii ilitoka wapi? Mvulana huyu ni nani?
Picha hii ilianza kuenea sana mtandaoni baada ya kupakiwa kwenye
tovuti ya Reddit miaka mitatu iliyopita na mwanamume kutok Texas, Marekani
aliyevutiwa nayo baada ya kuiona kwenye ukurasa wa Facebook wa rafiki yake.
Mwanamke aliye kwenye picha hiyo ni Heena Pranav, daktari mwenye
umri wa miaka 28 anayeishi Chicago.
Mwaka 2012, alipokuwa mwanafunzi, alizuru mji wa Gulu, kaskazini
mwa Uganda kusaidia kwenye mradi wa kuwasaidia wanawake walioathiriwa na vita
vya wapiganaji wa Lords Resistance Army. Mradi huo ulisimamiwa na shirika
laPros for Africa, linaloongozwa na mtawa Mkatoliki, Rosemary Nyirumbe.
Picha hiyo haikuhusiana na mradi huo na Pranav, akizungumza na
BBC Trending radio, amesema alikutana na mvulana huyo sokoni na anakadiria
alikuwa na umri wa miaka miwili au mitatu.
"Nilikuwa na wanafunzi wengine wakati huo, na tulikuwa
tunapiga gumzo na nikaona mvulana mdogo, aliyenivutia sana,” Pranav alisema.
“Mamake alikuwa karibu akifanya kazi sokoni. Nilimwendea mvulana
huyo kumsalimia na kucheza naye … alikuwa mchangamfu sana."
Mvulana huyo hakuzungumza Kiingereza, na Pranav naye haelewi
lugha za wenyeji. Lakini mkutano wao mfupi ulinakiliwa kwenye picha iliyopigwa
na mmoja wa wanafunzi kwenye kundi la Pranav. Binti huyo anasema hakuwa amewahi
kusikitia Reddit hadi pale rafiki yake alipoipakia picha hiyo huko na ikasambaa
sana.
"Sikudhani hili lingelitokea,” anasema. “Kungelikuwa na
uwezekano ningetaka sana mtoto huyu na mamake wajue kuhusu haya na wanufaike
kiasi kutokana nayo, kwa sababu nadhani alitumiwa bila kupata manufaa yoyote.”
BBC Trending inamtafuta mtoto huyu, kwa hivyo iwapo unamfahamu
au unajua familia yake, tutumia barua pepe kupitia trending@bbc.co.uk.
CHANZO: BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment