ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 14, 2016

MUFTI MKUU WA TANZANIA SHEIKH ABUBAKAR ZUBERI BIN ALLY ARUHUSIWA KUTOKA HOSPITALI BAADA YA AFYA YAKE KUIMARIKA

Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akimualika Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally kuongea na wanahabari katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya madaktari kumruhusu kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.
Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally akizungumza na waandishi wa habari katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya madaktari kumruhusu kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.
Masheikh wakiwashukuru madaktari bingwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya madaktari kumruhusu Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi bin Allykurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.


Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally jana ameruhusiwa kutoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Muhimbili ambako alikuwa amelazwa baada ya kufanyiwa upasuaji. 
Sheikh Abubakar ameishukuru Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na taasisi hiyo kwa kumpatia huduma nzuri za matibabu na kwamba afya yake hivi sasa imeimarika. Pia, amemshukuru Rais John Pombe Magufuli, Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa kufuatilia afya yake kwa karibu, viongozi mbalimbali na watu wengine waliofika kumjulia hali hospitalini hapo. 
“Siwezi kuwasahau madaktari walionipatia matibabu akiwamo Dk Mwanga, Dk Juma Mfinanga ambaye ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya moyo, Profesa Mohamed Janabi na wauguzi kwa kunipatia matibabu mazuri,” amesema Sheikh Abubakar wakati akizungumza katika hospitali hiyo. 
Katika hatua nyingine, Sheikh Abubakar amemuomba Rais Magufuli kuwatazama madaktari wa hospitali hiyo na kuwaongezea vitendea kazi zaidi ili waendelee kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa. 
“Mwanzo nilikuwa siiamini hospitali hii kama ingeliweza kunipatia matibabu bora, lakini madaktari walinihakikishia watanitibu vizuri na kweli sasa afya yangu imeimarika. Kumbe tunaweza kutibiwa vizuri katika hospitali zetu za hapa nyumbani. 
"Kwa kuwa nilikuwa siiamini hospitali zetu nina tiketi ya ndege ambayo nilikuwa nimekata ili nikatibiwe nje ya nchi, lakini baada ya matibabu nimepata imani na hospitali zetu na kumbe Watanzania wanaweza kutibiwa hapa nyumbani badala ya kwenda nje ya nchi", alisema.
Naye Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kwamba serikali itaendelea kufuatilia afya ya sheikh huyo baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani. “Napenda kuwaahidi kwamba tutaendelea kufuatilia afya ya Sheikh Abubakar lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri,” amesema Ummy Mwalimu. 

No comments: