Kila ifikapo tarehe 14 Februari nchini Marekani na sehemu nyengine Duniani husherehekewa Siku Ya Wapendanao "Valentine's Day", au kama ijulikanavyo kwa jina jengine "Siku Ya Mtakatifu Valentine" (Saint Valentine's Day). Katika miaka ya hivi karibuni siku hii pia imeanza kusherehekewa katika maeneo ya Afrika Mashariki. Labda shukrani ziende kwa enzi za utandawazi. Lakini je Siku Kuu hii ilianzia lini?
Asili yake
Hakuna chanzo cha uhakika kuhusu asili na chimbuko la Siku ya Wapendanao. Hata hivyo inaaminika kuwa asili yake inarejea katika enzi za Himaya ya Warumi, na baadaye Kanisa Katoliki kuingiza katika Ukristo.
Kuna watu watatu katika historia ya Kanisa Katoliki ambao wanajulikana kama Mtakatifu Valentine au Valentinus, na wote inasadikiwa walikufa kama mashahidi kwa mujibu wa itikadi za Kikatoliki, na kwa hivyo Kanisa likaamua kuiadhimisha siku waliyonyongwa kama kuwaenzi watumishi hao.
Kuna nganu inayodai kuwa Valentine alikuwa ni Mchungaji aliyehudumu Roma katika karne ya tatu. Wakati huo, Mfalme Claudius Wa Tatu, alipitisha amri ya kupiga marufuku ndoa kwa vijana wa Kiume kwa vile alihisi kuwa wanaume wasio na wake au familia walikuwa askari bora zaidi kuliko waliokuwa kwenye ndoa.
Mchungaji Valentine hakukubaliana na amri hiyo ya Mfalme na akawa naendelea kufungisha watu ndoa kwa njia za siri. Mfalme Claudius alipogundua mpango huo, aliamuru Valentine anyongwe.
Simulizi nyengine zinadai kuwa Valentine huenda alinyongwa kwa kosa la kuwasaidia Wakristo kutoroka katika magereza ya Warumi ambako walikuwa wakiteswa vibaya.
Inadaiwa kuwa Valentine ndiye aliyetuma maamkizi ya mwanzo ya mapenzi (valentine) kumpelekea msichana aliyempenda ambaye alikuwa akimtembelea wakti akiwa gerezani.
Inadaiwa kuwa kabla ya kifo chake, aliandika barua na kuisaini "Kutoka kwa wako Valentine". Maneno hayo bado yanaendelea kutumika hadi leo katika kadi za maamkizi ya siku ya Wapendanao.
Kwa upande mwengine, inasadikiwa kuwa kuanzia tarehe 13 hadi 15 Februari, Warumi walikuwa na desturi ya kusherehekea siku iliyojulikana kwa jina la Lupercalia. Miongoni mwa ada za siku hii ilikuwa ni wanaume kuwapiga wanawake.
Mnamo karne ya tano, Baba Mtakatifu Gelasius wa Pili, alikoroga mambo kwa kuichanganya siku ya Mtakatifu Valentine pamoja na ile ya Lupercalia kwa lengo la kuizika ada hiyo ya kipagani ya Warumi.
Kadiri miaka ilipozidi kusonga mbele ndivyo kadiri siku ya Wapendanao ilivyozidi kusherehekewa, mpaka ikafikia enzi za Shakespeare na Chaucer, ambao waliipamba siku hiyo katika kazi zao za sanaa na hivyo kuipatia siku hii umaarufu zaidi. Katika karne za kati, kadi zilizotengenezwa kwa mikono ndizo zilikuwa zikitamba.
Hatimaye, utamaduni huo ukavuka bahari na kunigia nchini Marekani na sehemu nyengine ulimwenguni, na mnamo karne ya 19 mapinduzi ya viwanda yakachapuza katika uchapishaji wa kadi za maakazi na kuipa umaarufu mkubwa zaidi siku hiyo. Katika mwaka 1913 shirika la Hallmark likaanza kuchapisha kadi za Siku ya Wapendao na kubadilisha mkondo wa kihistoria wa kuadhimisha siku hiyo.
Katika enzi za leo
Siku ya Wapendao si Sikuu Rasmi nchini Marekani. Watu huenda makazini kama kawaida, hata hivyo kama zilivyo Siku Kuu nyingi nchini humu, nayo pia imekumbwa na kimbunga cha biashara tangu pale Hallmark walipoanzisha kuzalisha kadi zao kwa wingi. Hii ni siku ya pili kwa ukubwa wa mauzo katika mwaka baada ya siku ya Christmas.
Inakadiriwa kuwa mauzo ya kadi hizo katika siku hiyo hufikia zaidi ya Dola Billioni 15. Baadhi ya watani wanasema kuwa "iwapo sherehe za siku ya Wapendanao zitapigwa marufuku nchini Marekani, basi shirika la Hallmark litafilisika"
Biashara nyengine inayochangamka katika siku hiii ni ya maua. Tani za maua huuzwa katika siku hii, na baadhi ya wauza-maua huajiri wafanyazi wa kiasi wiki moja kabla ya siku hii ili kukabiliana na ongezeko la wateja. Waridi ni nembo ya pili maarufu katika siku hii baada ya ile ya moyo.
Mbali na biashara hizo mbili, kuna zawadi aina kwa aina ambazo watu huwanunulia wale wawapendao, zikiwemo pipi, chakileti, na vitu vyengine vya kula na kunywa ambavyo ama hutengenezwa katika umbo la "moyo" kama ishara ya mapenzi, au kufungwa katika vifurushi vilivyopambwa katika mfumo kama huo.
Siyo Hallmark tu wanaofaidika katika siku hii, bali biashara nyingi mauzo yao huongezeka khususan mikahawa ambayo watu wanaotaka kudhirisha mapenzi kwa wapenzi wao hujazana katika sehemu hizo na kudhihirisha mapenzi ya hali ya juu kwa kuagizisha milo ya fakhari.
Kwa ujumla Waswahili wanasema "Mtu hujikuna ajipatapo". Kwa hivyo, kuna wale ambao huwanunulia wapenzi zawadi khafifu kama vile kadi yenye thamani ya chini, na kendelea mpaka kufikia vito vya thamani, magari, majumba na sema upendavyo.
Nchini Marekani, Canada na kwengineko, baadhi ya maskuli huandaa tafrija maalum za Siku ya Wapendanao ambapo wanafunzi hubadilishana zawadi na marafiki zao ambazo aghlabu huwa ni pipi, chakileti na kadi za maamkizi.
Wanaosherehekea na Wasiosherehekea siku hii.
Ingawaje siku hii huzalisha mabilioni ya Dola nchini Marekani, hata hivyo wako watu ambao hawasherehekei siku hii kutokana na sababu mbalimbali.
Wale wanaosherehekea wanaona kuwa ni siku iliyojaa upendo. "Siku ya Wapendanao ni siku iliyojaa upendo, anga yote huwa imejaa mapenzi", anasema Angie Bradlye, Msimamizi wa Uzalishaji katika kiwanda kimoja nchini Marekani, na kuongeza, "ingawa mume wangu amefariki, lakini katika siku hii hujihisi kama niko pamoja naye na moyo wangu hujaa furaha"
Naye Mae, anaona kuwa ni fursa kwa wanaume kudhihirisha mapenzi kwa wapendanao. "Ni siku muhimu kwa wanaume kudhihirisha mapenzi kwa wanawake wawapendao" alisema.
Kwa upande wa wale wasiosherehekea siku hii nao pia wana sababu zao.
Scotty ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika na anasema "Mimi siadhimishi siku hii kwa sababu ni siku kuu iliyotengenezwa na Wazungu tu kwa ajili ya kujipatia pesa kutokana na mauzo ya biashara zao"
Hata hivyo, Blue, ni mwanamke wa Kizungu, lakini hasherehekei siku hii akisema "Huu ni upuuzi mtupu, si chengine chochote ispokuwa wanawake wasiokuwa na shukurani kujipatia zawadi wasizostahiki kutoka kwa mabwana zao"
Wengine huwa hawasherehekei kwa sababu hawana wapenzi wa kusherehekea nao, kama ambavyo Kendra Simpson kutoka Jimbo la Karolina Ya Kusini aliiambia Swahillivilla : "Mimi sisherehekei kwa sababu sina mpenzi kwa sasa, kama nina mpenzi na anapenda kuadhimisha siku hii, basi nitaingia naye pumbaoni". Hata hivyo alisisitiza kuwa kila siku inapaswa kuwa siku ya mapenzi kwa wapendao, na siyo siku hii moja tu.
Rai hiyo inaungwa mkono na Bi LaToya Bragg wa jimbo la Ohio, ambaye anasema "ni jambo la kushangaza kuona watu wanahemkwa na kupoteza mapesa katika siku hii moja, wakati ambapo mapenzi yanatakiwa kudumu kwa muda wote ambao watu wapendanao huwa pamoja katika uhai wao"
Athari mbaya za Kijamii.
Bi LaToya aliyeandika kitabu kwa jina "The Heart Of Me" pia haoni sababu ya kuadhimisha siku hii katika mfumo wake wa sasa kwa vile unaleta athari mbaya za kijamii. "Kuna watu wengine hali zao za kiuchumi siyo nzuri, kwa hivyo hawawezi kunnuua zawadi kwa wapenzi wao, na hivyo wapenzi wanaokosa zawadi kutoka kwa wapenzi wao, hujihisi duni mbele ya wenzao"
"Aidha huleta athari za kiuchumi kwa watu wenye kipato cha chini kwa kujikalifisha kuwanunulia wapenzi wao zawadi wazipendazo ambazo wakati mwnengine ziko nje ya uwezo wao, almradi tu na wao waonekani ni watu katika jamii"
Mbali na umaarufu wa siku hii, hata hivyo uchunguzi mdogo uliofanywa na Swahilivilla umeonesha kuwa, idadi kubwa ya watu hawajui asili, chimbuko na maana ya Siku ya Wapendanao. Kristy, ni afisa wa mapokezi na usafirishaji katika Shirika moja la vifaa vya magari anasema: "Ninavyojua siku hii ni ya wanaume kuwanunulia zawadi wapenzi wao, na kwa wanaume siku yao ni ile inayoitwa 'sweetest hearts day'.."
Naye Amanda Waleker anasema: "Sijui chochote kuhusu asili ya siku hii, watu wanasherehekea na kuadhimisha, lakini mimi si katika mambo yangu"
No comments:
Post a Comment